Marekani, China zaingia vita mpya ya soya. Tanzania kunufaika na vita hiyo?

Jamii Africa

China imethibitisha kusitisha uagizaji  wa maharage aina ya soya kutoka Marekani ikiwa ni hatua inazozichukua kujibu mapigo kwenye vita ya kibiashara inayoendelea baina ya mataifa hayo mawili.

China ambayo ni mtengenezaji  mkubwa wa mafuta ya mbegu duniani imesitisha uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Marekani baada ya nchi hiyo kupendekeza ushuru mpya kwenye bidhaa zinazotoka China.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari cha kimataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bunge Limited ya Marekani, Soren Scroder alisema kwasasa China haiagizi bidhaa kutoka Marekani ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari ya afya na usalama.

“Chochote wanachonunua hakitoki Marekani,” alisema Schroder na kuongeza kuwa wamehamishia soko katika nchi za Amerika ya Kusini ambako kuna uzalishaji mkubwa wa soya. “Wananunua maharage kutoka Canada, Brazili, zaidi sana Brazil, lakini hawanunuia chochote kutoka Marekani.”

Uamuzi huo wa China umekuja kwa mshangao dhidi ya sekta ya kilimo ya Marekani, ikizingatiwa kuwa Aprili mwaka huu ilitangaza ushuru mpya wa soya inayosafirishwa kutoka Marekani.

Wafanyabiashara wa soya nchini Marekani walitarajia kuwa mgogoro huo wa kibiashara  ungetatuliwa na kuisha mapema ili usafirishaji wa bidhaa za kilimo uendelee kama ilivyokuwa awali. Lakini kinachonekana ni kwamba vita hiyo inazidi kuimarika na hakuna dalili za kufikia muafaka.

Maharage ya soya yakiandaliwa kwajili ya kusafirishwa

Schroder alisema  kutokana na mtikisiko wa kibiashara, ni wazi kuwa China tayari imesitisha ununuzi wa bidhaa kutoka Marekani. “Ni kwa muda gani utadumu, nani ajuaye? Lakini kwasababu kuna wingu kubwa la sintofahamu, utaendelea kuwepo.”

Mfumko wa bei za bidhaa za kilimo umeongezeka katika maeneo mbalimbali duniani katika wiki za hivi karibuni wakati vita ya kibiashara ya mataifa hayo makubwa ikiendelea. Bidhaa zingine za kilimo ambazo zimeingia kwenye vita hiyo ni mahindi, muhogo na nyama ya nguruwe.

Uzalishaji wa Maharage ya soya  unashika nafasi ya pili kwa mazao nchini Marekani na soko lake linategemea zaidi nchi za bara la Asia ambazo ndiyo waagizaji wakubwa.

Kulingana na data za Idara ya Kilimo ya Marekani, wiki mbili za mwisho zilizoisha Aprili 19 mwaka huu, China ilizuia manunuzi ya tani 62,690 za soya kutoka Marekani ambayo ingesafirishwa Agosti, 2018.

Katika kipindi hicho cha Agosti, nchi za Amerika ya Kusini zitakuwa zinakamilisha mavuno ya soya. Kutokana na hali iliyopo sasa zitapata soko kubwa la kusafirisha zao hilo nchini China.

Brazil ndiyo inaongoza duniani kwa usafirishaji wa soya na mauzo yake yanaweza kuongezeka maradufu, ikizingatiwa kuwa katika msimu wa 2017/2018 itauza tani milioni 73.1 kwenye soko la kimataifa dhidi ya tani milioni 56.2 za Marekani.

                    Soya inazallishwa kwa kiwango kidogo nchini Tanzania

Hata hivyo, Marekani nayo imeanza kuchukua hatua za kukabiliana hali hiyo ambapo inafanya mashauriano na nchi za Amerika ya Kusini ili zinunue soya yao.

“Ninaweza kusema kwamba tunapendelea biashara huria isiyo na vikwazo kwasababu jambo ni jema kwa mtu yoyote,” alisema Schroder. “Tumejipanga kukabiliana na hali inayoendelea.”

 

 Tanzania inaweza kunufaika na vita hiyo?

Kumekuwa na mjadala juu ya vita ya kibiashara baina ya mataifa hayo mawili na jinsi nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinavyoweza kufaidika na soko la China ambayo imesitisha uagizaji wa zao hilo toka Marekani.

Baadhi ya wataalamu wa uchumi wamesema Afrika bado haina nguvu ya kusafirisha soya nje ya bara hilo kwasababu  inakabiliwa na matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa na usalama mdogo wa chakula.

Mtafiti wa Kitengo cha Masoko na Biashara katika Shirika la Chakula Duniani (FAO), Thoenes P ameeleza katika utafiti wake wa hivi karibuni kuwa soya inayozalishwa Afrika ni asilimia 5 tu ya soya yote inayopatikana duniani.

“Ulimaji wa maharage ya soya imejikita zaidi kwenye nchi nne- Marekani, Brazil, Argentina na China na zinazalisha asilimia 90 ya soya yote ya dunia. Asia ukiondoa China, na  Africa zinachangia asilimia 5 ya uzalishaji wote,” ameeleza Thoenes.

Katika hali hiyo, Marekani ina nafasi kubwa ya kutumia soko ililopoteza China kwa nchi za Afrika ili kujiweka katika nafasi nzuri kibiashara.

Akizungumza katika kongamano la mwaka la wabia wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Machi 2017, Waziri wa Kilimo na Chakula, Dk. Charles Tizeba alikiri kuwa uzalishaji wa soya nchini bado ni wa kiwango cha chini na viwanda vya usindikaji vinaagiza kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa bidhaa.

“Hiki kiwanda kinahitaji tani 7,000 kwa ajili ya kutenegeneza chakula cha kuku, lakini hadi sasa wanapata tani 2,000 tu  maana yake kiasi kilichobaki wanalazimika kuagiza kutoka nje,” alinukuliwa Tizeba alipotembelea kiwanda cha Silverland kilichopo Iringa.

Serikali inashauriwa kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji  na  kunufaika na soko la soya nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *