TUMEFURAHIA na kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa taifa letu la Tanzania. Tumejiorodheshea mengi ya kujivunia. Yote yanaonekana. Wengi walifurahia lakini si wote tutanyamaza bila kuyasema mapungufu yanayoonekana.
Hakuna anayepuuza yaliyofanywa tangu uongozi wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye mimi binafsi naamini kuwa bado ‘’anaishi’’ licha ya kufika hivi karibuni Butiama na kufanya sara katika Kaburi lake.
Tangu enzi hizo mpaka sasa serikali tunayoiita kwa mazoea kuwa ni serikali ya awamu ya Nne wakati bado ni serikal ya Tanzania chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, sote tumeendelea kutimiza wajibu wetu katika taifa kwa lengo moja la kusonga mbele kimaendeleo na kukabiliana na ulimwengu unaobadilika.
Shule za sekondari zimeongezeka kwa wingi, vyuo na hata shule za msingi na wanaoendelea kuziongeza ni wananchi wenyewe ambapo wahamasishaji wakubwa ni viongozi wa siasa na serikali.
Ulinzi umeendelea kuhimarishwa mipakani huku baadhi ya wanaopewa dhamana hasa serikalini uzalendo ukizidi kupungua kwa taifa huku wizi na unyonyaji wa mali za serikali na rasilimali za nchi zikiendelea kuwanufaisha wengi lakini si wote.
Sheria na sera za kudhibiti na kutibu mambo hayo zipo vizuri sana, hakika serikali yetu ni moja kati ya serikali bingwa zenye uwezo mkubwa wa kutunga sheria na sera lakini tatizo kubwa ni usimamizi wa dhati na utekelezaji wake.
Kuna sheria za uhujumu uchumi, utaifishaji mali za watu binafsi na kuwa mali za umma, kitengo cha maadili ya viongozi wa umma lakini imefikia hatua hakuna anayeweza hata kuthubutu kuzitekeleza sheria na kanuni hizo kilichobaki ni kutegeana ili atakayeanza kuzitekeleza aibuliwe jambo nna kumalizwa kisiasa na kiutendaji… hayo ni mafanikio mabaya katika miaka hamsini ya uhuru.
Hakuna anayependa kustaafu bila gari, bila nyumba, bila viwanja hata ambavyo hawezi kuviendeleza, bila miradi endelevu na bila kuwa na marafiki ambao ni wafanyabiashara halali na haramu ndani ya serikali na nje ya serikali.
Hakuna anayemaliza elimu yake na kupata ajira serikalini hku akiwaza kufanya kazi kwa uadilifu bali kila mmoja anatamani akipata ajira aibe na kukopa ili akihojiwa aseme kuwa amefanya ‘’maendeleo’’ kwa mikopo, hayo ni mafanikio hasi ya hapa tulipofikia ndani ya miaka hamsini ya uhuru.
Wanapanga mikakati mingi na kuamuru badala ya kukubaliana. Hapa ni muhimu kujenga mashaka na watawala wetu wanaoogopana kuwajibishana kwa dhati kwa manufaa ya taifa letu na vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.
Tunahangaika na kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa kushuhudia kwa macho yetu, kugusa na hata kunusa maiti za ndugu zetu hasa watoto na wajawazito kutokana na ugonjwa wa Maralia ndani ya miaka hamsin ya uhuru.
Ukiuliza na kusoma kidogo tu, siyo mpaka uwe na Digrii hata elimu yetu sisi tulio wengi ya upe unaambiwa na wataalum wa masuala ya afya kuwa kimdudu kinachoambukiza ugonjwa huo wa Maralia kinaitwa mbu!
Ukienda ndani zaidi na kufanya utafiti wa kawaida tu, unagundua kuwa mbu huyo tangu anapozaliwa huwa anaishi siku saba na kufa ingawa hatuelezwi kuwa anazikwa wapi.
Sasa inashangaza sisi kama taifa kuendelea kupambana na ki-mbu chenye uhai wa siku saba kwa miaka hamsini tangu tutangaze maadui zetu watatu akiwemo adui ujinga , maradhi na umasikini.
Je mbu ni moja ya vivutio vya hifadhi za taifa? Je tukiwaua na kupambana nao kikamilifu tutajibu mashitaka? Au tunawaachia ili tuendelee kuneemeka na misaada inayotolewa na wenzetu wa ng’ambo ili waendelee kuuza dawa wanazofanyia utafiti!
Nchi kama Marekani, Sweden na Japan kuna mbu lakini watu wake hawaugui Maralia kwanini sisi Tanzania tuendelee kusulubiwa na mbu na kupoteza nguvu kazi kubwa ya taifa inayoteketea kwa ugonjwa wa Maralia?
Hapana, haikubaliki hata kidogo. Tuanze sasa kuwa na mipango kama taifa ya kushughulikia jambo moja baada ya lingine kuliko ilivyo hivi sasa kuwa na mipango mingi na kuanza kuishughulikia yote kwa pamoja na hatimaye tunashindwa vibaya katika vita hizo huku pesa zikiishia kwa wanaokabidhiwa miradi.
Tugawane kikamilifu kuwa askari kadhaa wanashughulikia kundi fulani kwa uhakika badala ya kuishia kuunda tume kila kukicha bila kupatiwa ufumbuzi wa kisayansi katika masuala ya kitaifa.
Hakuna uchawi wala bali tunaendekeza maneno ya kukatisha tamaa kuwa eti zile ni nchi tajiri na sisi ni nchi masikini. Hicho ni kisingizio bali kinachohitajika hapa ni uadilifu.
Hivi wakati wanapanga kuwa nchi kadhaa ni nchi tajiri na nchi kadhaa ni nchi masikini mimi na wewe tulikuwepo? Kwanini tunaamini zaidi maandishi kuliko uhalisia? Tunapaswa kubadilika na kujenga mashaka.
Mbu anayeishi siku saba anatushinda kupambana naye kiasi cha kuendelea kutuua kila siku je angekuwa anasiahi siku 14 nani angesalia? Umefika wakati tuseme basi kwa kuweka mikakati thabiti ya kutokomeza kwa vitendo ugonjwa huu wa Maralia.
Kama hatutafanya hivyo tupunguze makogo na kujivuna kuwa tumefaikiwa sana kwa miaka hamsini ya uhuru. Endapo afya za watanzania zitaendelea kuwa mashakani sote tushike tama tukitafakari kisha tuinune na majibu muafaka.
Tuwe na jeshi zuri, Rais mzuri, Mawaziri wazuri, wataalam wanaoitwa wazuri lakini bila mawazo chanya sote tutaangamia hata kama tutaenda kutibiwa ng’ambo ya nchi hakuna jiwe litakalosalia na historia itatuhukumu.
Kwasababu tafiti nyingi zinafanyika nje ya nchi yetu na huku zinakuja kutekelezwa, kwanini tunashindwa kutekeleza tafiti zilizofanyika na kuwezesha kudhibiti Maralia nchi hizo tunazosema kuwa ni nchi zilizoendelea badala yake tunaendekeza dili za dawa zinazobadilika kila kukicha bila mafanikio ya kweli kudhibiti ugonjwa huo?
Najua tuna viongozi makini sana, serikali sikivu sana, sheria na sera nzuri sana mpaka wenzetu wa mataifa mengine wanakopa kutoka kwetu.
Hivyo Serikali sikivu chini ya Jemedali wetu Dr.Jakaya Mrisho Kikwete tulione hili na kama hamjajionea uhalisia wa vifo vyenyewe na mnaviona kwenye takwimu naomba tuungane mkaone uchungu wa jinsi watanzania wakiwemo watoto na wanawake wanavyokata roho bila matumaini ya wanaowaacha hai.