Maendeleo ya nchi za Afrika kwa sehemu kubwa yanategemea misaada kutoka nchi zilizoendelea, lakini suala hilo limeibua mijadala juu ya ufanisi wake katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini wan chi hizo.
Mtaalamu na Mshauri wa Uchumi wa Dunia, Dambisa Moyo kwa nyakati tofauti amekuwa akitofautiana na hoja za wanazuoni ambao wanahimiza nchi za Afrika kupewa misaada ili kukamilisha miradi ya maendeleo, akielezea misaada hiyo kuwa haina matokeo chanya kwenye ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya raia.
Utafiti mpya wa taasisi ya Virginia Tech uliotolewa Desemba 2017 unaeleza kuwa misaada inayotolewa na nchi wahisani haiwafikii maskini katika maeneo ya vijijini bali huishia mjini kwa watu ambao wamepiga hatua ya maendeleo.
Utafiti huo uliangazia miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kutoka mwaka 2009 hadi 2010, umebaini kuwa miradi hiyo ilielekezwa kwenye miji iliyoendelea na kuachana na lengo la kupunguza umaskini katika nchi za Afrika.
Uchambuzi huo unadhihirisha wazi tofauti iliyopo kati ya utolewaji na ufanisi, usawa wa utolewaji wa misaada hiyo kati ya maeneo ya vijijini na mjini. Kwenye utafiti huo, Prof. Ryan C. Briggs anasema alichunguza takwimu kwa kuigawa ramani ya bara la Afrika katika seli 10,572 kwa kuangalia miradi, idadi ya watu na kiwango cha umaskini kwa kila seli.
Baada ya uchambuzi huo alibaini kuwa maeneo ambayo yanapokea misaada mingi, “Yana nishati, umbali mfupi kwenda mjini, hutumia muda mfupi kwenda kwenye miji mikubwa na kiwango kidogo cha utapiamlo”. Upendeleo huo sio kwasababu maeneo mengi ya mjini yana watu wengi wenye uwezo.
Hali hiyo inaenda kinyume na utaratibu wa kusambaza misaada ambayo huelekezwa kwenye kuboresha elimu, huduma za afya, miundombinu na zaidi kwa watu wamaskini. Ikiwa misaada inakusudia kupunguza umaskini, Briggs anasema, “Inatakiwa ilenge maeneo ambayo yameathirika zaidi na umaskini”.
Mathalani, nchini Kenya katika majimbo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki yana miradi michache ya maendeleo kuliko mikoa yenye utajiri na mtandao mzuri wa barabara. Na wakati mwingine suala hilo la kufadhili miradi ya wahisani huchukuliwa kisiasa ambapo majimbo yanayounga mlengo fulani hupendelewa kuzidi yale yenye itikadi tofauti na viongozi wenye mahusiano ya karibu na wahisani.
Utafiti huo unaeleza kuwa misaada hiyo haiwafikii moja kwa moja walengwa na kwamba hawawezi kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Pia unaonyesha kuwa hata misaada inayoelekezwa mjini inatolewa kwa upendeleo na kuendeleza dhana ya kutokuwa na usawa katika matumizi ya rasilimali za nchi.
Hata hivyo, kumaliza umaskini serikali za Afrika na wafadhili wanashauriwa kutathmini usambazaji wa miradi na kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa nchi.
“Nafikiri misaada inalenga maeneo yaliyoendelea kwasababu wanaweza kuwafikia watu wengi”, amesema Prof. Briggs na kuongeza kuwa misaada hiyo iwafikie wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu.