WANAFUNZI kusomea katika madarasa yaliyoezekwa kwa nyasi, huku katika shule nyingine ikiwa na walimu wawili tu na wanafunzi 195 ni baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu mkoani Ruvuma.
FikraPevu imebaini kwamba, sekta ya elimu mkoani humo licha ya kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu, lakini pia miundombinu mibovu inadaiwa kuchangia kudumaza elimu na kwamba endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa, hali itakuwa mbaya baadaye.
Mkoa huo wenye jumla ya shule za msingi 783, na wanafunzi 276,964 wakiwemo wavulana 136,563 na wasichana 140,401 bado uko nyuma kielimu ambapo shule za vijijini ndizo zina hali mbaya zaidi.
FikraPevu inatambua kwamba, Mkoa wa Ruvuma una shule za sekondari zinazofikia 145, lakini nyingi hazina mazingira mazuri kwa kusoma wala kufundishia kwa ufanisi.
Ukosefu wa mabweni, maabara, walimu hasa wa masomo ya sayansi ni changamoto ambayo imesababisha wanafunzi wengi kufeli huku wengine wakishindwa kufanya mitihani kwa baadhi ya masomo.
Huduma za maji ambazo zinahitajika na kila mtu kwa maisha ya kila siku, hazipo vizuri kwa karibu wilaya zote ikiwemo Songea Mjini, hali inayowafanya watumishi wengi kutokuwa na mwamko wa kufanya kazi maeneo hayo.
Lakini mbali na hilo, mkoa umepiga hatua katika kuongeza idadi ya shule za sekondari, kwa mfano, mwaka 2005 Wilaya ya Namtumbo ilikuwa na shule 16 tu za sekondari lakini hadi mwaka 2016 zimefikia shule 23.
Hata hivyo, kuongezeka kwa shule hakukuendana na uboreshaji wa mazingira ya eneo kubwa la mkoa huo ili wanafunzi waweze kupata elimu ipasavyo.
Kwa mujibu wa Mtaala wa Elimu Tanzania na utaratibu ambao upo sehemu nyingi, kiwango cha chini cha mwalimu kufundisha kwa wiki ni vipindi 6 na kiwango cha juu ni vipindi 16.
Hii inampa mwalimu muda wa kutosha kupumzika na kufanya kazi kwa ufanisi, lakini hali iko tofauti katika baadhi ya wilaya na shule nyingi za Mkoa wa Ruvuma.
Mkoa huo una jumla ya walimu 3,065, ambapo kati yao 2105 ni wanaume na 960 wanawake, huku shule nyingine zikiwa hazina hata mwalimu mmoja wa kike.
Kutokana na idadi hiyo ya walimu, inaonyesha kwamba, kama uwiano ungekwenda sawa, basi kila shule ilipaswa kuwa na walimu 21, lakini FikraPevu inafahamu kwamba, uwiano huo hauko sawa kwani kuna shule zenye walimu 9 tu wakati shule nyingine ina walimu 57.
Hali hiyo inaashiria mzigo mzito ambao walimu mkoani humo wanakabiliana nao katika kufundisha, hali inayoleta ugumu kwa mwanafunzi kuweza kupata alama za juu, kwani baadhi ya masomo hayana walimu kabisa.
Kwa mfano, matokeo ya shule tatu za sekondari Mikalanga, Maguu na Mkuwani yanathibitisha hali mbaya ya kielimu inayoukabili mkoa huo huku hatua stahiki zikishindwa kuchukuliwa kwa wakati.
Takwimu zinaonyesha kwamba, mwaka 2016 Shule ya Sekondari Maguu ilikuwa na wanafunzi 204 na walimu 18 tu, na kwa wastani wa masomo tisa inamaanisha kila somo lilikuwa na walimu wawili tu.
Kwa bahati mbaya zaidi, kati ya walimu hao hawakuwepo wa kutosha wa masomo ya sayansi, hususan Fizikia, hali ambayo iliwafanya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2016 washindwe kufanya mtihani wa Fizikia.
Hali hiyo ilichangia shule ya Maguu kupata matokeo mabovu kupindukia, ambapo hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja la kwanza na la pili, huku wanafunzi wawili wasichana wakiambulia daraja la tatu kati ya wanafunzi wote 23 waliohitimu.
Aidha, wanafunzi 18 walipata daraja la nne na watatu walipata daraja la sufuri.
Kulingana na takwimu hizo, ni wanafunzi watatu tu waliomepata alama “D” ya somo la Hisabati huku wengine wakipata alama “F”.
Ikumbukwe kwamba, daraja la tatu ndilo angalau linamuwezesha mwanafunzi kusonga mbele.
Hata kwa wanafunzi ambao watabahatika kusonga mbele watakumbwa na ugumu katika masomo ya sayansi, ambayo ndiyo yanayopewa kipaumbele katika mikopo ya elimu ya juu kwa sasa.
Kwamba wanafunzi hao walikosa kabisa mwalimu wa Fizikia kiasi cha kushindwa kufanya mtihani wa somo hilo ni swali ambalo linapaswa kujibiwa na mamlaka husika kwani siyo kiashiria kizuri cha kuwapata wataalam wa siku zijazo kama wahandisi na madaktari.
Pengine wanafunzi hao walikuwa na ndoto za kuwa wanasayansi, lakini kwa hali ilivyo wamelazimika kuachana na ndoto hizo kutokana na ukosefu wa walimu wa masomo hayo.
Je, ikiwa watoto hao watafanikiwa, baada ya kumaliza vyuo vya ufundi ama kidato cha sita, na kufuzu kwa elimu ya juu na kunyimwa mikopo kwa sababu ya kusoma sanaa au biashara, itakuwa haki kwake kunyimwa mkopo kwa sababu tu hakuchukua masomo ya sayansi?
Maguu ni mfano tu kati ya shule nyingi zilizo na mazingira mabovu ya kujifunza na kufundisha zinazopatikana mkoani humo.
Tamko la Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako, la kwamba kila mwanafunzi lazima asome masomo ya sayansi halitakuwa na maana yoyote ikiwa serikali haitaajiri walimu wa sayansi ili kuepukana na aibu kama iliyotokea kwenye Shule ya Maguu.
Adha ya ukosefu wa maji katika shule za sekondari mkoani Ruvuma nayo inachangia matokeo mabovu ya ufaulu, kwani katika baadhi ya maeneo inaelezwa kwamba wanafunzi wanalazimika kuhangaika mitaani kutafuta maji.
Hali ni mbaya zaidi kwa shule za msingi, ambapo wilayani Namtumbo baadhi ya shule zimejengwa kwa nyasi, jambo ambalo linaonyesha mazingira ambayo siyo rafiki kwa mwanafunzi kuweza kujifunza wala mwalimu kufundishia.
Aidha, baadhi ya shule wanafunzi wa madarasa tofauti wanachangia darasa.
Ni jukumu la serikali na wadau wa elimu kutatua changamoto hizi na nyingine nyingi ili kuwapa watoto haki yao ya msingi ya elimu katika mazingira bora, lakini wakati huo huo kuboresha mazingira ya kufundishia kwa walimu ili kuwahamasisha kwenda hata shule za vijijini kama Sera ya Taifa ya Elimu inavyoelekeza.