UNAWEZA ukawa mwendo wa saa 3 na dakika 39 tu kwa gari ndogo kutoka Songea hadi Mbamba Bay kwenye makao makuu ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambako ni umbali wa kilometa 168.2 tu, lakini kwa hali ilivyo sasa, unaweza kutumia hadi saa saba ndipo ufike.
Waandishi wa FikraPevu wakipita kwenye tope katika barabra ya Mbinga-Mbamba Bay kutokana na ubovu wa barabara.
Na kwa kipindi hiki cha masika, unapaswa kuwa tayari kuogelea tope katika maeneo kadhaa kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay, yapata kilometa 67.8, kutokana na ubovu wa barabara.
Kuteremka na kusukuma gari, ama kupiga chepe kujaza udongo barabarani kuyanasua magari ni mambo ambayo yeyote anayetaka kwenda Nyasa anapaswa kujiandaa nayo.
FikraPevu imeshuhudia magari mengi yakiwa yamekwama kwa saa kadhaa kutokana na ubovu wa barabara, utelezi na tope wakati mvua zimenyesha, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa inakwamisha maendeleo kutokana na kukatisha mawasiliano baina ya wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa na maeneo mengine kama Mbinga na Songea.
Hali halisi katika eneo la Mto Lumeme kwenye barabara ya Mbinga-Songea.
“Wakati wa kiangazi walau hali inakuwa nafuu kwa sababu licha ya kuwa barabara ni ya vumbi, lakini huwa kunakuwepo na magari mengi ya abiria tofauti na ilivyo sasa,” anasema Martha Haule, mkazi wa Nangombo Mission wilayani Nyasa.
Martha anasema kwamba, hivi sasa kuna mabasi mawili tu ya abiria yanayopishana ambayo yanafanya safari zao kati ya Mbinga – Mbamba Bay – Liuli, idadi ambayo haitoshelezi mahitaji kwa kuwa abiria ni wengi.
FikraPevu imeelezwa kwamba, zamani kabla ya kuwekwa lami kwa barabara ya Songea-Mbinga yenye urefu wa kilometa 100.4, hali ilikuwa mbaya zaidi, lakini angalau hivi sasa usafiri ni mwingi na wa uhakika.
Aidha, FikraPevu inafahamu kwamba, kilometa 78 kati ya hizo, yaani kutoka Makutano ya Peramiho hadi Mbinga, zilijengwa kati ya mwaka 2010 hadi 2012 na kampuni ya Sinohydro kutoka China kwa gharama ya Dola 48.444 milioni, ukiwa ni msaada wa Watu wa Marekani.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, barabara yenye urefu wa kilometa takriban 125 kutoka Unyoni kupitia Tingi hadi Darpori kwenye machimbo ya dhahabu nayo iko katika hali mbaya ambapo katika kipindi hiki cha masika magari yanashindwa kupita kwa urahisi.
Usafiri wa bodaboda
Kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa magari ya abiria, maeneo mengi hasa ya Wilaya ya Nyasa yamekuwa kama kisiwa wakati wa masika kwa vile hakuna miundombinu bora inayoweza kuyaunganisha na maeneo mengine ili wananchi waweze kujiletea maendeleo.
Mwandishi wa FikraPevu aliyebebwa kwenye bodaboda akiwa anavushwa kwenye daraja la miti kuelekea Kijiji cha Malungu wilayani Nyasa.
FikraPevu imeshuhudia wananchi wakitumia zaidi usafiri wa bodaboda au kutembea kwa miguu umbali mrefu, hatua inayoelezwa kuwa changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo.
“Kukodi pikipiki kutoka hapa Mbamba Bay hadi Darpori ambako ni mpakani na Msumbiji gharama yake ni Sh. 50,000, sasa nani anayeweza kumudu?
“Ikumbukwe kwamba, kule kuna wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali hapa halmashauri au kwenda Mbinga na Songea, lakini kwa changamoto hii wanashindwa,” anasema Sixtus Mhagama.
Kukwamisha utalii
Ukosefu wa miundombinu bora hasa ya barabara unaelezwa kukwamisha pia juhudi za utalii wa fukwe ambao umeanza kushika kasi katika Mwambao wa Ziwa Nyasa.
FikraPevu imeelezwa kuwa, serikali ya Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla imehamasisha utalii wa fukwe ambapo hivi sasa watalii mbalimbali wa kutoka nje wamekuwa wakimiminika kujionea mandhari nzuri ya fukwe hizo.
Uwepo wa samaki wa mapambo katika ziwa hilo nao umeongeza kasi ya wageni wakiwemo watalii na wafanyabiashara wanaokusanya samaki hao na kuwasafirisha nje ya nchi ingawa unaathiriwa na ukosefu wa barabara za uhakika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa, Oscar Mbyuzi, anasema utafiti umebaini Ziwa Nyasa lina aina 503 za samaki wa mapambo ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani.
Anasema uwepo wa idadi kubwa ya samaki wa mapambo unaweza kukuza uchumi kwa kasi kwa kuwa samaki hao wanaweza kuvutia watalii na wawekezaji ambao watanunua samaki kwa bei kubwa na wananchi na serikali kupata kipato na kukuza uchumi kutokana na kodi wanayolipa.
Utafiti umebaini kuwa samaki wengi wa mapambo kwenye maji baridi ni jamii ya Cichlids.
Ziwa Tanganyika lina spishi zaidi ya 200 lakini wanaosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya mapambo ni wastani wa spishi 30, Ziwa Nyasa lina spishi zaidi ya 750 lakini wanaosafirishwa nje ya nchi kama samaki wa mapambo ni takriban spishi tano tu.
Kulingana na utafiti huo, ziwa Victoria lilikuwa na spishi zaidi ya 300 katika miaka ya 1970 kabla samaki aina ya Sangara aliyepandikizwa hajasambaa na kula jamii ya Cichlid.
Taarifa ya Wizara ya Uvuvi inaonesha kuwa samaki wanaovuliwa kwa ajili ya biashara ya samaki wa mapambo kutoka Ziwa Nyasa wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni samaki wanaoishi kwenye mawe au miamba ambao wapo wa aina 250.
Kundi la pili ni samaki ambao wengi wao hutumika kwa kitoweo ambao wapo chini ya koo (genera) 38.