Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Jijini Mwanza(Mwauwasa) inatekeleza mradi utakaogharimu Euro 900,000 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, ikiwemo ufungaji wa mita kubwa ya kisasa itakayosaidia kupunguza upotevu wa maji yanayozalishwa na mamlaka hiyo.
Taarifa hiyo ilitolewa Jijini Mwanza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo , Mhandisi Mashaka Sitta, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
“ Tatizo lipo, ingawa kusema kweli linaendelea kupungua; isitoshe muda siyo mrefu tatizo hilo litabaikia historia mara baada ya kukamilikakwa mradi mkubwa ambao utagharimu Euro 900,000,” alisema Mhandisi Sitta na kuongeza;
“Kupitia mradi huo, Mwauwasa itanunua mita za kisasa kwa ajili ya kudhibiti upotevu wa maji”.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema fedha hizo zitatumikika katika ununuzi wa vifaa ikiwa ni pamoja na mita za kisasa pamoja na magari kwa ajili ya usafiri wa wataalamu watakaotekeleza mradi huo.
Alisema kupitia mradi huo, Mwauwasa inatarajia kufunga mita moja kubwa ya kieliktroniki katika ofisi ya makao makuu ya mamlaka, ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti tatizo sugu la upotevu wa maji.
Alisema mita hiyo iitwayo bulk (bulk metre) ina uwezo wa kutoa taarifa juu ya upotevu wa maji katika mita ndogondogo zilizounganishwa kwenye mtandao wa mamlaka.
Mhandisi huyo alisema kwa kutumia mita hiyo, mamlaka itakuwa na ushahidi ambao utaiwezesha Mamlaka kuchukua hatua dhidi ya visababishi vya upotevu wa maji ya bomba jijini hapa.
“ Uholanzi imekubali kutusaidia fedha kupitia EU ( Jumuia ya nchi za Ulaya). Kwa ajili hiyo, ndio watakuwa consultant (washauri),” alisema Sitta.
Kwa mujibu wa Sitta, tayari washauri hao wapo Jijini hapa kwa ajili ya kuendelea na awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Alisema mradi huo utaanza kutekelezwa ifikapo Aprili mwaka huu na kwamba unatarajiwa kukamilika baada ya miaka miwili.
Hata hivyo, alisema kwa sasa upotevu wa maji yanayozalishwa na mamlaka hiyo umepungua kutoka wastani wa asilimia 48 kufikia mwishoni mwa mwaka jana hadi asilimia 41.6 Januari mwaka huu.
Alisema upungufu huo umetokana kuimarika kwa usimamizi katika kitengo cha usomaji mita pamoja na udhibiti wa vitendo vya kujiunganishia mita za maji kiujanja ujanja.
Alisema lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha upotevu wa maji unazidi kupungua hadi asilimia 38 ifikapo Juni mwaka huu.
“ Mitambo yetu ina uwezo wa kuzalisha maji ya kiwango cha mita za ujazo 108 kwa siku, ingawa hadi sasa tunazalisha mita za ujazo 72,000 tu kwa siku. Tofauti hii inatokana na ukweli kwamba bado tunakabiliwa na changamoto kwamba maeneo mengine jijiji bado hayajafikiwa na mtandao wa maji,” alisema.
Alisema hali hiyo inasababishwa na jiografia ya Jiji la Mwanza, ikiwa ni pamoja na miamba,milima pamoja na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kutengeneza njia ya kupitishia mabomba ya maji.
Imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza