Moshi Vijijini: Wananchi wagomea mradi wa maji. Harufu ya ufisadi yanukia

Jamii Africa

DHANA kwamba Watanzania wengi ni watu wanaoumia “kimoyomoyo” hata kama wanaumizwa, imeanza kutoweka.

Idadi yao kubwa; wale walioko vijijini na mijini, wasomi na wale walioshindwa “kukanyaga” madarasa, wameanza “kufunguka.” Hawadanganyiki tena kirahisi.

Hali hii inadhihirishwa na msimamo wa wanakijiji wa Kata ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi Vijijini, Kilimanjaro, ambapo pamoja na kukabiliwa na shida kubwa ya majisafi na salama, wamekataa mradi wa maji unaodaiwa kujengwa chini ya kiwango.

Tangi la mji la mradi wa Korini.

Wananchi hao wanapiga hatua kadhaa mbele, wakifunguka kuwa mradi huo umejaa harufu ya ufisadi.

Mradi huo ulifadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na kugharimu Sh. bilioni 1.3 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na ulianza kujengwa mwaka 2013  na kukamilika mwaka 2014.

Kutokana na “mgomo” huo wa wananchi, hadi sasa haujakabidhiwa rasmi kwao kutokana na madai yanayohusiswa na ufisadi.

FikraPevu iliyotembelea eneo hilo la mradi, imebaini kuwepo kwa madai kuwa, licha ya mradi huo kujengwa chini ya kiwango, mkandarasi alilipwa fedha zake zote.

Wananchi wanahoji, “uadiifu wa viongozi waliosimamia mradi huo uko wapi? Au nao ni mingoni mwa wanufaika wa njia ovu?”

Kinacholalamikiwa na wananchi ni fedha iliyotumika katika mradi haiendani na thamani ya mradi, ramani ya mradi inaonesha chanzo ambacho kingetumika kuchukua maji kipo ndani ya msitu, lakini kilichotumika ni chanzo kilichopo mtoni.

Kama mradi huo ungekamilika kwa kiwango stahiki, zaidi ya kaya 3,000 katika vijiji vya Korini Juu, Korini Kati na Korini Kusini wangenufaika kwa kupata huduma ya majisafi na salama.

FikraPevu imeshuhudia usumbufu, hasa unaowahusu wanawake – wa kutembea umbali mrefu wa kati ya saa moja na moja na nusu kusaka maji .

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rau KDC, kilichopo Kijiji cha Korini Kusini, Joseph Lema amesema licha ya mradi huo kutokabidhiwa rasmi, wapo baadhi ya watu wanachota maji hayo yanayotoka kwenye baadhi ya mabomba.

Kituo cha maji.

FikraPevu ilishuhudia machafu yakitiririka kwenye moja ya mabomba yaliyounganishwa kwenye mradi huo.

“Tangu mwaka 2014 wananchi hawajakabidhiwa mradi huu licha ya wananchi kutumia muda wao mwingi kuchimba mitaro kwa ajili ya kutandaza mabomba na wale ambao hawakushiriki walitozwa faini na ya 5,000 kila mmoja,” anasema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mpirani, Joseph Kimath, ameiambia FikraPevu kuwa hawapo tayari kuupokea mradi huo hadi hapo kasoro zilizopo kwenye mradi huo zitakapofanyiwa kazi .

FikraPevu imeona kuwepo kwa vituo (virura) zaidi ya 50 vya kuchotea maji ambavyo mpaka sasa havitoi maji, huku vingine vikiwa havina hata mabomba wala pampu za kusukuma maji .
Wananchi wacharuka

Livingstone Nderaio Macha, mkazi wa Kitongoji cha Rau KDC ni mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Korini Kusini ambaye alitoa ardhi yake kwa ajili ya kuruhusu kujengwa kwa kituo cha kuchotea maji .
Katika mazungumzo na FikraPevu, anasema  tangu kujengwa kwa kituo hicho hakuna mabomba yaliyoingizwa ndani wala pumpu za kusukama maji, huku akiitaka Ofisi ya Mhandisi wa Maji Wilaya ya Moshi Vijijini kukiondoa kituo hicho kwa madai kuwa hakina msaada wowote kwake.
“Tangu mwaka 2014 walipojenga hiki kutuo, sijawahi kuwaona, ukiangalia huku ndani hakuna bomba wala pampu ya kusukuma maji, huu ni ubabaishaji mkubwa, kumbuka wananchi walishurutishwa kuchimba mitaro kutoka huko juu hadi chini, lakini hakuna maji,” anasema.
Macha anaiambia FikraPevu kuwa wananchi wengi walijikuta wakichukuliwa mali zao na hata kushambuliwa kutokana na kushindwa kushiriki katika shughuli za kuchimba mitaro, huku wengine walitozwa  faini ya Sh. 5,000 ikiwa ni adhabu kwa kutoshiriki kazi za kujitolea.
Mkazi mwingine wa kitongoji hicho, Jackson Omar Moshi ambaye pia ndani ya ardhi yake pamejengwa kituo cha maji, anasema tangu kujengwa kwa kituo hicho hakuna kiongozi yoyote aliyefika katika eneo hilo kuelezea juu ya kukwama kwa mradi huo.
Kama ilivyokuwa kwa Macha, FikraPevu ilishuhudia ilishuhudia kituo hicho kilichopewa namba 0304302516WP39 (Water Pipe) kikiwa hakina mabomba wala pampu za kusukuma maji, huku wananchi hao wakidai hawajui hatima ya mradi huo ni lini utaanza kutoa maji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Maji aibuka

Mwenyekiti wa bodi ya maji ya mradi huo- uliopewa jina la ‘mradi wa maji Korini’, Willbart Kisanga amesema tangu hatua za awali za ujenzi wa mradi huo, wananchi hawajawahi kushirikishwa.
Ameiambia FikraPevu kuwa bodi haijawahi kuoneshwa hata ramani ya ujenzi wa mradi huo na licha ya kuulalamikia katika ngazi mbalimbali ikiwamo ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi ya mkuu wa wilaya na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Vijijini. Huko “hakuna hatua zilizochukuliwa.”
Mwenyekiti huyo wa bodi anasema mwaka 2014 mradi huo ulikuwa miongoni mwa miradi iliyozinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, lakini siku mbili baada ya uzinduzi huo, kibao cha uzinduzi kiliondolewa “chapchap” na kufichwa kusikojulikana.
Utata mwingine unaodaiwa kugubika mradi huo ni pamoja na kutumika matanki ya zamani badala ya kujengwa matanki mapya, huku baadhi ya matanki yakiwa machakavu.
FikraPevu imebaini kuwa matanki ya zamani yaliyopigwa rangi kuonesha kuwa ni mapya, yapo katika maeneo ya Sahoni Gulio, Masanga – Kwa Msendo na Machadi Juu.

Mwenyekiti huyo akatoa masimamo wa bodi kwamba hawataupokea mradi huo hadi hapo mapungufu yaliyobainika kwenye mradi huo yatakapopatiwa ufumbuzi, ikiwamo kuwekwa kwa mabomba na pampu za kusuka maji kwenye virura vilivyojengwa kulingana na ramani ya mradi huo.
Hofu ya magonjwa ya mlipuko

Mwenyekiti huyo wa bodi ya maji anasema maji yanayotoka katika mabomba ya mradi huo ni machafu na yanatishia mlipuko wa magonjwa ya kuhala kutoka na kutowekwa dawa, huku chanzo cha maji kinachotumika kusambaza maji hayo kikiwa hakina uzio.
FikraPevu imeona maji hayo yanatoka kwenye mfereji wa maji wa Mrambo na kuelekezwa kwenye mabomba yanayokwenda kwa wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ikiwamo kunywa.

Mhandisi atetea

Mhandisi wa Maji Wilaya ya Moshi Vijijini, Elifadhili Mrutu, ametetea mradi huo akidai hauna kasoro yoyote huku pia akitupilia mbali madai ya wananchi kuwa maji ya mradi huo ni machafu na kuongeza kuwa ni hivi karibuni tu maji hayo yamewekewa dawa.
 

FikraPevu ilichoshuhudia

Pamoja na kuwepo malalamiko na kauli ya “wakubwa” wa maji wa halmashauri hiyo, ni dhahiri kuwa maji hayo ni mchafu.

Kwa macho tu ya kawaida, uchafu unaonekana na yakikaa ndani ya chombo kwa muda wa siku mbili au zaidi, hutoa harufu na utando wa njano, hivyo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *