Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amekutana na waandishi wa habari mjini Beijing kuelezea utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ya China katika mwaka uliopita na mipango ya mwaka huu ya utekelezaji wa sera hiyo.
Waziri Wang amesema katika mwaka uliopita Rais Xi Jinping akiwa msanifu mkuu wa sera ya kidiplomasia ya nchi hiyo, alihusika moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza diplomasia “makini” ya kiongozi wa nchi.
Ameeleza kuwa Rais Xi alitembelea nchi 57, na mpaka sasa amekutana na wakuu 110 wa nchi mbalimbali duniani.
Ziara zake na za wakuu wa nchi waliotembelea China, sio tu zimeimarisha uelewa wa dunia kuhusu China, bali zimeimarisha sifa ya China na ushawishi wake duniani, na kuchangia kwenye utatuzi wa matatizo yanayoikabili dunia.
Waziri Wang amebainisha kuwa, mwaka huu mbali na shughuli za kawaida za kidiplomasia, serikali ya China itaandaa baraza la BOAO la Asia litakalofanyika mwezi April katika kisiwa cha Hainan, kusini mwa China ambapo ajenda kuu itakuwa ni mageuzi na kufungua mlango kwa nchi wanachama.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi (kushoto) akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje ya Tanzania, Agustine Maiga alipotembelea nchini.
China pia itaandaa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. Vilevile kutakuwa na shughuli mbili kubwa zitakazozihusisha nchi za Afrika, ambazo ni mkutano wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika utakaofanyika mwezi Septemba na Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa yatakayofanyika mjini Shanghai mwezi Novemba.
Mbali na mikutano hii, Waziri Wang ametaja shughuli nyingine kubwa ikiwa ni pamoja na Rais Xi Jinping kuhudhuria mkutano wa kundi la nchi 20 zililizoendelea duniani ambao atafanyika nchini Argentina. Pia mkutano wa viongozi wa uchumi wa nchi za Asia na Pacific (APEC) utakaofanyika nchini Guinea na mkutano wa nchi za BRICS utakaofanyika nchini Afrika Kusini.
Wanahabari wengi wa Afrika wamefuatilia zaidi maelezo ya waziri Wang kuhusu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kwa kuwa ametaja kwamba kazi yao muhimu katika mkutano huo itakuwa ni kushughulikia mpango wa “Ukanda mmoja, Njia moja” mpango ambao una miradi mbalimbali ya kuzinufaisha nchi za Afrika.
Amesisitiza kuwa nchi za Afrika zitapewa nafasi ya kutumia mkutano huo kuongeza nguvu mpya ya uhai kwenye uhusiano kati ya pande hizo mbili, ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa yatakayofanyika mjini Shanghai yametajwa kuwa yatatoa fursa kwa nchi za Afrika kuonyesha bidhaa zao na kutafuta soko nchini China.
Akimnukuu Rais Xi Jinping, Wang amesema urafiki kati ya China na nchi za Afrika utaendelea kuwa imara na China haiwezi kuwasahau marafiki zake wa Afrika. China inatambua kuwa changamoto mkubwa kwa nchi za Afrika kwa sasa ni kulinda amani na usalama.
Amehitimisha kwa kusema China itashirikiana na nchi za Afrika kukabiliana na matishio ya usalama kama ugaidi, uharamia na majanga ya asili, na itahimiza ushiriki wake kwenye utatuzi wa migogoro.