Mtwara: Wanafunzi Mtiniko Sekondari wafeli kabla ya mtihani. Miaka 10 hawana walimu wa Hisabati na Fizikia

Jamii Africa

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Mtiniko, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara huanza kufanya mitihani wakiwa tayari wamefeli masomo mawili kati ya saba yanayohitajika.

Kimsingi, wanafunzi hao huingia katika vyumba vya mitihani ya masomo ya Hisabati na Fizikia wakiwa tayari na majibu ya kufeli kutokana na kukosa walimu tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2007.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa hiyo ni moja ya sababu zilizofanya shule hiyo ya Kata ya Mtiniko kufanya kushika mkia katika matokeo ya mtihani wa kipimo wa kidato cha pili taifa mwaka 2016.

Wanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Mtiniko mkoani Mtwara wakiwa darasani.

Shule hiyo ambayo iko zaidi ya kilometa 45 kusini-mashariki mwa Mji wa Mtwara ilikuwa na watahiniwa 144 kati ya wanafunzi 150 waliosajiliwa, ambapo 55 pekee ndiyo walioweza kufaulu.

Uongozi wa shule walonga

Jengo mojawapo katika Shule ya Sekondari Mtiniko mkoani Mtwara.

“Tangu shule ianze mwaka 2007 haijawahi kuwa na mwalimu wa Hisabati na Fizikia, hii ndiyo kusema kabla ya mtihani wanafunzi tayari wanakuwa wamefeli masomo hayo mawili, shule ina walimu 19 lakini watatu kati yao wapo masomoni, tuna upungufu wa walimu watano, kati yao watatu wa Hisabati na wawili wa Fizikia,” Lwitiko Mwakabende, Makamu Mkuu wa Shule hiyo aliiambia FikraPevu.

Mwalimu Mwakabende anasema kuwa, changamoto nyingine iliyosababisha shule hiyo kuingia katika shule 10 zilizofanya vibaya ni wanafunzi 22 ambao walifanya mitihani hiyo wakiwa hawajui kusoma wala kuandika Kiswahili, wakiwa ni miongoni mwa wanafunzi 89 ambapo kati yao 43 wavulana na 49 wasichana waliofeli mtihani huo.

“Unaweza kujiuliza inawezekanaje mwanafunzi asiyejua kusoma na kuandika Kiswahili alifaulu mtihani wa darasa la saba…tuliwapokea wanafunzi 150, baada ya upembuzi tukagundua kuwa 22 kati yao walikuwa mbumbumbu, lakini tuliendelea kuwafundisha.

“Kama alishindwa kujua kusoma na kuandika Kiswahili kwa miaka saba, hivi kweli tunataraji ndani ya miaka miwili ajue kusoma na kuandika Kiingereza? Sidhani kama kuna muujiza wa kufanikisha hilo,” anasisitiza Mwakabende.

Mwalimu huyo anaongeza kwamba, katika wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016, kulikuwa na watoro 75, ambapo 45 kati yao ni watoro wa kudumu na 30 watoro wa rejareja, lakini walifanya mtihani huo na kufeli.

“Wanafunzi sita walishindwa kufanya mtihani kutokana na utoro, watatu kati yao walipata mimba… kuna wanafunzi ambao utayari wao ni mdogo kuendelea na shule lakini wazazi nyumbani ni wakali, na katika hali ya ya kuwakomoa wazazi walichokifanya ni kuunda makundi ya kufanya vibaya mtihani ili wasiendelee na shule, na kweli kundi hilo lote limeanguka,” anasisitiza.

Ameieleza FikraPevu kwamba, walimu waliyabaini hayo baada ya mtihani kumalizika na wao kupata taarifa kutoka kwa wanafunzi wengine juu ya uwepo wa kundi la wanafunzi lililojipanga kufanya vibaya ili wasiendelee na shule.

“Shule hii inahudumia wanafunzi wa kata mbili ya Mtiniko na Mtimbwilimbi, wapo wanafunzi wengine wanatoka mbali sana, kwahiyo utakuta mwanafunzi hafiki shule kwa madai baiskeli iliharibika.”

Aidha, aliiambia FikraPevu kwamba, umbali huo pia unagharimu wanafunzi kwa sababu hata wakitoka shule saa nane mchana, hadi kufika nyumbani ni jioni huku wakiwa wameshinda na njaa.

Wanafunzi nao wazungumza

Sharafi Lihundu, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo anakiri kuwa ukosefu wa walimu wa Hisabati na Fizikia umechangia shule hiyo kufanya vibaya.

“Hatuna mwalimu wa Hisabati na Fizikia lakini tunalazimika kufanya mitihani ya masomo hayo, ni vigumu kufaulu,” anaeleza Lihundu.

Mwanafunzi mwingine, Zulepha Mjinga, ambaye ni mmoja wa waliofeli, anasema utoro ndio uliomfanya akafeli huku akibainisha kwamba, hali hiyo ilisababishwa uduni wa maisha nyumbani kwao.

“Kuna wakati nililazimika kutokwenda shule kwa sababu nilikosa chakula nyumbani, ninaishi na bibi hivyo nilikuwa nafanya vibarua ili tupate chakula,” aliiambia FikraPevu.

Uongozi wa Kijiji unasemaje?

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtinikio mkoani Mtwara wakitoka darasani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbambakofi ilipo shule hiyo, Hamis Dadi, anasema sababu za kufanya vibaya zinatokana na shule za msingi kushindwa kuwajengea msingi imara wanafunzi hao.

“Matokeo mabaya yanachangiwa na wanafunzi kukosa msingi imara katika shule za msingi kutokana na changamoto lukuki zinazozikabili shule hizo, zikiwemo uhaba wa walimu,” anasema mwenyekiti huyo.

Wazazi nao wakiri

Rehema Ismail ni mmoja wa wazazi wenye watoto waliopo sekondari, lakini anakiri kwamba hajawahi kufuatilia maendeleo ya mwanaye kutokana na kulelewa na baba yake.

“Matokeo mabaya yanasabishwa na watoto kulelewa na mzazi mmoja, mfano mimi mwanangu simfuatilii kwa sababu anakaa na baba yake baada ya kuachana,” anasema Rehema.

Kwa upande wake, Mohamed Hamad, anasema kama mzazi akielimishwa kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto ni rahisi kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni.

“Wazazi mkituelimisha sasa tunaelimika, siyo kama miaka ya 1980, sababu za utoro ni wazazi hatujawa tayari, na wanafunzi wenyewe ukiwaambia wasome wanasema ‘kichwani hamna kitu’ na hata wale wanaokwenda hatujui kama wanafika shuleni,” anasema Hamad.

Mkurugenzi azungumza

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ambaye pia ni Ofisa Elimu Sekondari, Bumi Kasege, anakiri kwamba wamekuwa wakikumbana na chagamoto ya wanafunzi wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika huku baadhi wakisoma neno moja moja na wengine wakishindwa kabisa.

Aliiambia FikraPevu kwamba, sababu hiyo inachangiwa na aina ya mtihani wenyewe kutokana na kuwa na maswali ya kuchagua na kuweka kivuli pekee, hivyo mwanafunzi mwingine anaweza kuibia kwa wenzake au kubahatisha na kufaulu.

“Inatokana na aina ya mtihani, mtoto anaweza akawa amekaa karibu na wenye uwezo sababu unakuta maswali yote ni ya kuchagua na kuweka kivuli, kwahiyo anaweza akaangalia kwa mwenzake na pengine ikawa ni bahati yake anabahatisha akapatia,” anasema Kasege.

Aidha, alikiri uwepo wa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, kama Hisabati, Kemia na Fikizia pamoja na Biashara.

Ameiambia FikraPevu kwamba, halmashauri hiyo inahitaji walimu wa sayansi wapatao 86 lakini waliopo ni 31 na walimu wa masomo ya biashara wanaohitajika ni wanne.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *