MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kabalenzi wilaya ya Bukoba vijijini Twinayesu Emmanuel (8) ameuwawa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili,kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake.
Wilaya ya Bukoba vijijini kwa miaka ya karibuni imegubikwa na matukio yanayohusishwa na imani za ushirikina ambapo mwaka jana mtoto Anord Ezekia(3)wa kijiji cha Karonge pia alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na mwandishi wa FikraPevu na Ofisa mtendaji wa Kata ya Kaibanja Projestus Mwombeki mwili wa mwanafunzi huyo uligundulika juzi ukiwa umetelekezwa vichakani na watoto waliokuwa wanachanja kuni.
Alisema kabla ya kugundulika kwa mwili huo,mtoto huyo aliyekuwa anaishi kijiji cha Kaibanja kitongoji cha Kahyoro alipotea katika mazingira ya kutatanisha April 8 na baadaye mwili kukutwa kichakani.
Mtendaji huyo amebainisha pia kuwa mazingira ya tukio hilo yanaonyesha mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeanza kuharibika ulipelekwa eneo hilo na watu wasiojulikana baada ya kuuwawa kikatiri.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Vitus Mlolele alipoulizwa kwa njia ya simu ya kiganjani kuhusu tukio hilo alisema angelitolea ufafanuzi baadaye kwani alikuwa anaendelea na kikao.
Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa tayari watuhumiwa watatu wa mauwaji hayo wanashikiliwa kwa uchunguzi akiwemo mwananchi mmoja anayedaiwa kuandaa mpango wa kuua na kunyofoa viungo vya mtoto huyo.
Habari hii imeandikwa na mwandishi wetu Phinias Bashaya, Bukoba