Licha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kupokea wanachama kutoka upinzani ambapo leo chama hicho kimempokea Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Muslim Hassanali kimeshauriwa kutathmini faida na hasara zinazoweza kupatikana katika mchakato wa kujipatia wanachama wapya.
Ushauri huo umetolewa na aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Sanaa, Nape Nnauye wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari cha kimataifa juu ya CCM kuendelea kuwapokea wanachama wapya kutoka upinzani ambao wanahamia kwenye chama hicho ili kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli katika kupambana na ufisadi amesema hatua hiyo ni nzuri lakini ni vyema kupima faida na hasara za mapokezi hayo.
“Ni vizuri tukajiridhisha, tukapima faida na hasara na mwisho wa siku kila chama kinahitaji wafuasi. Siyo jambo ambalo tunapaswa kuwekeza katika hilo, kwamba ni jambo kubwa sana halina tija vile kwa vyama vyote kuweza kuhama na kuhamia matokeo yake ni kuleta mvurugano”, amesema Nape.
Amesema sababu kubwa ya wanachama kuhama kwenda vyama vingine ni athari baada ya uchaguzi ambazo huaacha majeraha kwa baadhi ya wanachama na hutumia fursa hiyo ya kuhama kama nia ya kujiimarisha kisiasa.
Ameongeza kuwa kila chama kina utaratibu wake wa kupokea wanachama wapya na kabla hakijafanya maamuzi kinafanya tathmini juu ya faida zinazoweza kupatikana katika ujenzi wa chama husika.
“Nimesema kuna faida na hasara lazima ziangaliwe, kuna taratibu inawezekana wamepima wameona ni vizuri lakini kitaalamu kisiasa ukifanya uchaguzi kuna faida na hasara zinapatikana. Sasa inategemeana madhara ni kiasi gani na faida ni kiasi gani na matokeo yake hayaendi mbali utaona tu kwasababu kwa vyovyote vile kuna faida wanataka wazipate pengine waliopo wanaweza kuridhika,” amesema Nape.
Amebainisha kuwa hasara ambayo chama inaweza kupata kwa kupokea wanachama wapya na kuwapa fursa ambazo wanachama waliopo hawajizipata ni kuleta mgawanyiko ndani ya chama. Akitolea mfano wa kuhama kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowass kutoka CCM na kwenda CHADEMA kuliibua mgongano katika chama hicho na kusababisha Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa kuondoka na baadhi ya wanachama.
“Mtakumbuka Edward Lowassa alitoka CCM na kwenda UKAWA wakati ule alipofika kule ndio kikawa chanzo cha kutoka kwa Dk. Slaa ilikuwa ni pigo kubwa. Lakini kuna faida na hasara zake,” amesema Nape.
Akizungumzia mtazamo wa wanaCCM ambao wamekitumia chama kwa muda mrefu juu ya ujio wa wanachama wapya amesema suala hilo linaweza kuleta manung’uniko hasa pale wanachama wapya wanapopewa kipaombele au nafasi za uongozi.
“Wanaweza kunung’unika kwamba sisi tumekuwapo humu ndani kwa muda mrefu lakini faida wanazozipata watu wengine wanaokuja sisi hatuzipati. Lakini kama faida ni kubwa kuliko malalamiko hakuna shida,” amesema Nape.
Hassanali ambaye amewahi kuwa mgombea ubunge katika jimbo la Ilala amejiunga leo na CCM na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Philip Mangula katika ukumbi wa Checkpoint uliopo Pugu jijini Dar es Salaam.
Kuondoka kwa Hassanali kunaendeleza mapigo ya CCM dhidi ya vyama vya upinzania baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu kutimkia CHADEMA kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake katika kulinda utawala wa sheria, uwazi na uwajibikaji katika maendeleo ya taifa.
Kuondoka kwa Nyalandu kulifungua mlango kwa wanachama, madiwani na wabunge wengine wa upinzani wakiwemo Dkt. Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulya (Kinondoni) kuviama vyama vyao na kujiunga na CCM.
Hamahama hiyo hasa kwa madiwani na wabunge kujiuzuru nafasi zao za uongozi na kuingia CCM imeibua mjadala juu matumizi ya rasilimali za nchi na mwenendo wa siasa za Tanzania ambazo hubadilika kulingana na maslai ya wanasiasa kutafuta kuungwa mkono na wananchi wengi.