HAKUNA huduma inayotolewa bure katika hospitali teule ya Mtakatifu Francisco iliyopo mjini Ifakara mkoani Morogoro pamoja na kwamba ni mshirika wa serikali katika kutekeleza sera ya afya ya mwaka 2007.
Sera hiyo inatoa upendeleo kwa makundi maalumu wakiwemo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma ya afya bure ili kufikia Lengo namba tano la Mpango wa Millenia wa kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.
Mjamzito anayetaka kujifungua katika hospitali hiyo anatakiwa kulipa Sh 70,000 kama atafanyiwa upasuaji na Sh 40,000 endapo atajifungua kwa njia ya kawaida.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilorombero, Dk Awami Magwira anasema ipo haja kwa uongozi wa hospitali hiyo kuzingatia utekelezaji wa sera hiyo kwa kuwa inapata ruzuku toka serikalini.
PICHA: Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Dk Awami Magwira
“Huduma zote ni za malipo bila kujali makundi maalumu ambayo kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007 yanatakiwa kupata huduma bure,” anasema na kuongeza kwamba gharama ya kumuona daktari ni Sh 5,000.
Monica Malela (31) ameiomba serikali kuinunua hospitali hiyo kwa kuwa inatoa huduma bora na kuwafanya wajawazito wengi akiwemo yeye kusita kwenda kwenye vituo vya serikali na kukimbilia hapo.
PICHA: Hospitali Teule ya Rufaa ya Mtakatifu Francisco inavyoonekana kwa mbele
“Tatizo pekee lililopo katika hospitali hii ni gharama, wapo wanaoshindwa kumudu gharama zake, vinginevyo pangekuwa kimbilio la wengi,” anasema.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Anjelo Nyamtema anasema “inawezekana kabisa kutoa huduma bure kwa makundi maalumu wakiwemo wajawazito, lakini hilo litawezekana pale serikali itakapokamilisha vifungu vya mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa hospitali hii.”
PICHA: Mkurugenzi wa Hospitali Dk Angelo Nyamtema
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero anakiri kuwepo na upungufu wa utekelezaji wa makubaliano ya ubia huo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Kwa kupitia makubaliano maalumu na serikali, Dk Nyamtema anasema hospitali hiyo ilipewa hadhi ya kuwa hospitali teule ya wilaya ya Kilombero mwaka 1976 na mwaka 2010 ikapandishwa hadhi kuwa hospitali teule ya rufaa ngazi ya mkoa.
Katika makubaliano hayo, serikali ilikubali kugharamia ununuzi wa dawa, vifaatiba na kulipa mishahara ya wafanyakazi wake wote huku Jimbo likiwa na jukumu la kugharamia miundombinu yake.
Hata hivyo anasema kati ya wafanyakazi 350, serikali inawalipa wafanyakazi 40 tu walioajiriwa hospitalini hapo wakitokea serikalini.
“Kwa mwezi tunatumia zaidi ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wengine, huu ni mzigo mkubwa kwa hosptali kwahiyo hatuna budi kuendelea kutoza gharama kwa wagonjwa wote wanaokuja kupata huduma bila kujali wanatakiwa kupata msamaha,” anasema.
Wakati mkataba huo unaeleza kwamba hospitali hiyo inatakiwa kupata ruzuku ya Sh Milioni 200 kwa ajili ya dawa kila mwezi, Dk Nyamtema anasema inatakiwa kupata pia asilimia 30 ya fedha za Mfuko wa Pamoja (Busket Fund) zinazopelekwa katika wilaya hiyo.
“Julai hadi Novemba mwaka jana hatukupata fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia tatu, na zile za dawa tuliambulia mwezi Agisti tu mwaka jana, napo tulipewa shilingi milioni kumi na mbili badala ya shilingi milioni 200” anasema.
Anasema pamoja na kulipa mishahara, hospitali hiyo inabeba mzigo mwingine wa gharama ya umeme; kwa wastani hospitali hiyo inalipa sh Milioni 7 kwa mwezi huku serikali ikiwapa Sh Milioni tatu tu kutoka katika mfuko wa matumizi mengineyo (Other charges).
“Na wakati ule wa mgao wa umeme tulikuwa tunatumia zaidi ya shilingi milioni nane kwa mwezi kwa ajili ya mafuta ya jenereta,” anasema.
Alisema pamoja na juhudi za serikali za kutaka makundi maalumu yapate huduma bure, aliomba Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uwasaidie kugharamia huduma wanazostahili.
Mfuko wa Afya ya Jamii, ulioanzishwa kisheria kupitia Sheria Na 1 ya mwaka 2001 (Sura 409 ya Sheria za Tanzania) ili kutoa huduma za matibabu kwa jamii iliyopo katika sekta isiyo rasmi mijini na hasa vijijini katika ngazi ya halmashauri, tarafa kata na kijiji.
Ni utaratibu wa hiari unaoiwezesha kaya kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima kwa kuchangia kiasi cha Sh 5,000 au Sh 10,000 kwa kadiri jamii yenyewe katika Halmashauri husika itakavyoamua.
PICHA: Muuguzi wa wodi ya wazazi katika hospitali Teule ya Rufaa ya Mtakatifu Francisco Prisca Asenga akitoa huduma kwa mjamzito Halima Kiswambe
Serikali kwa upande wake inachangia kwa kiwango ambacho kaya inachangia hivyo kuufanya Mfuko huu kujulikana pia kwa jina la Tele kwa Tele.
Uamuzi huu unalengo la kuwezesha kutekeleza kwa kasi Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM 2007-2017), kuongeza uwigo na kuenea kwa CHF katika Halmashauri mbalimbali na pia kuboresha huduma katika ngazi zote.
Mfuko huu ulianza kwa majaribio wilayani Igunga mwaka 1996 na baadaye kuenea katika Halmashauri mbalimbali nchini ijapokuwa kasi yake imekuwa sio ya kuridhisha. Mwaka 2007 Serikali iliamua kuwa Shughuli za Mfuko huu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ziwianishwe.