OFISI ya Mkurugenzi Mtendaji katika Halmashauri ya wilayani ya Ukerewe mkoani Mwanza inadaiwa kupuuza maelekezo yaliyokuwa yametolewa na ofisi ya Mkuu wa mkoa ili kufanikisha zoezi la uuzaji wa sembe iliyotokana na msaada wa mahindi yaliyoagizwa na serikali kuu kwa ajili ya kupunguza makali ya njaa wilayani humo.
Madai hayo yametolewa na wananchi huku, wilaya hiyo ikitajwa kuwa miongoni mwa wilaya zingine 50 nchini ambazo wakazi wake wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na ukame uliojitokeza wakati wa msimu wa kilimo, 2010/2011.
Vilevile, ofisi hiyo inadaiwa kugawa zabuni ya uuzaji wa mahindi hayo kwa wafanyabiashara zaidi ya wale walioteuliwa
Habari za uhakika zimeliambia gazeti hili kwamba zoezi la uuzaji wa sembe kwa bei nafuu kama ilivyoagizwa na serikali ya mkoa wa Mwanza katikati ya mwaka huu limepuuzwa wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kitendo cha ofisi ya Mkurugenzi Mtendeji wilayani humo kuwaagiza wazabuni kuuza mahindi badala ya sembe.
Inadaiwa kwamba wananchi wakiwemo, Maafisa Watendaji wa Kata( WEOs) pamoja na madiwani wilayani humo hawakutaarifiwa kuhusu kuwasili kwa mahindi hayo na kwamba wengi hawana taarifa za kutolewa kwa msaada huo.
” Kinachotushangaza ni kwamba mahindi hayo yanauzwa kwa bei ya shilingi 600 kwa kila kilo moja. Wao(wazabuni) walikuwa wameagizwa kuza sembe kwa shilingi 600; sasa kwa nini wanatuuzia mahindi kwa bei ile ile ya sembe!” alihoji mkazi wa kijiji cha Hamkoko katika kata ya Ngoma, tarafa ya Mumbuga, huku akiomba jina lake lisitajwe gazetini kwa kuhofia uhasama na watendaji wa Halmashauri.
Inadaiwa kwamba tofauti na wazabuni wanne waliopendekezwa na kamati ya chakula na maafa , ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wilayani humo ilichukua jukumu la kutangaza nafasi zingine za uzabuni wa kuuza mahindi hayo katika ngazi za kata.
Habari zinadai wafanyabiashara waliopatikana katika ngazi za kata hawamo kwenye orodha ya majina ya kampuni nne ambazo zilipendekezwa kusambaza na kuuza chakula hicho.
Madai hayo ambayo yamethibitishwa na taarifa iliyotolewa katikati ya mwaka huu kwa vyombo vya habari na Mhandisi wa Kilimo mkoani hapa, Mhandisi wa Kilimo mkoani hapa, Ackley Chotta , ambapo aliwataja wazabuni wanne waliokuwa wamependekezwa wilayani humo kwamba ni Tualib Nasor, Misana Mtaki, Leonard Mtesigwa pamoja na Bukiko Magula.
“ Mimi sina taarifa kwamba kuna sembe inayouzwa kwa bei nafuu ambayo imeletwa katika eneo la kata yangu kwa ajili ya kuwauzia wananchi kwa bei nafuu; isipokua ninasikia tetesi tu” alisema diwani wa kata ya Kagunguli wilayani humo, Gatawa Misana( Chadema), wakati alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu.
Alidai kuwa suala hilo ambalo ni muhimu na la kijamii halijawahi hata kujadiliwa katika mikutano ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Diwani huyo alikiri kwamba kata ya Kagunguli ni miongoni mwa maeneo mengi ambayo yanahitaji msaada wa haraka wa chakula wilayani humo.
“ Ni kweli tumeshapokea chakula cha msaada katika kata yangu; tumepokea mahindi na wala siyo sembe” alikiri diwani wa kata ya Ngoma, Theresecia Mkwaya Meyado( Chadema) ingawa hakuwa tayari kutoa ufafanuzi kwa madai kuwa alikuwa kwenye kikao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt Donald Masale hakupatikana kwa njia ya simu ili aweze kutoa ufafanu ufafanuzi kuhusiana na madai hayo; simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo , Quine Mlozi alikiri kwa njia ya simu kuhusu uuzwaji wa mahindi badala ya sembe huku akidai kuwa limetokana na maamzi ya wananchi wenyewe.
Hata hivyo, alisema kuwa ofisi yake haina mihutasari ya vikao vilivyobadilisha maelekezo ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alikiiri pia kwamba baadhi ya maeneo wilayani humo hayajapokea msaada huo kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wake.
Awali Mhandisi Chotta katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema wazabuni 40 ndio waliokuwa na haki ya kununua mahindi kutoka Ghala la Taifa (SGR) lililoko mkoani Shinyanga na kuyasaga kabla ya kusambaza na kuuza sembe katika maeneo yote ya halmashauri ya wilaya ya mkoani Mwanza.
Alifafanua kuwa Maafisa Watendaji wa Kata walikuwa wameagizwa kuwatangazia wananchi katika vituo vyao vya kazi ili waweze kujitokeza kwa ajili ya kununua chakula chakula hicho.
Alisema jumla ya wazabuni 40( majina tunayo) walikuwa wameteuliwa na mkoa wa ajili ya kusambaza sembe katika wilaya zote saba za mkoa wa Mwanza.
Chotta alizitaja Halmashauri za wilaya huku mgawo wa tani za mahindi zikiwa kwenye mabano kwamba ni Geita(tani 300), Kwimba(tani 300),Sengerema(tani 250), Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo inajumuisha wilaya ya Ilemela na Wilaya ya Nyamagana(tani 400),Misungwi(tani 300), Magu(tani 300) pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe(tani 150).
Alisema sembe hiyo ingeliuzwa kwa bei ya shilingi 600 kwa kilo na kwamba lengo la kuuza sembe ni pamoja na kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Na. Juma Ng’oko, Mwanza