USULI:
Gazeti tando la FikraPevu limefanikiwa kupata ushahidi unaoonyesha kwamba, pamoja na nia njema ya serikali ya awamu ya tano katika kuijenga “Tanzania ya viwanda,” bado dhamira hiyo inabaki katika karatasi kuliko kwenye vitendo, kwa saabu kadhaa, zikiwemo hujuma.
Kwa mujibu wa takwimu zinazohusiana na zao la korosho linalowapatia Watanzania wapatao milioni tano, bado asilimia 85 ya mavuno yote ya korosho isiyobanguliwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi, na hasa India.
Wakati huo huo, FikraPevu imebaini kuwa, baada ya India kubangua korosho ghafi ilizozinunua kutoka Tanzania, inaiuzia Tanzania mafuta ya ganda la korosho, na hivyo Tanzania kuporeza fedha za kigeni kununua bidhaa ambayo inaweza kuzalishwa hapa nchini.
Pamoja na sababu nyingine, ni hitimisho la FikraPevu kwamba, viwanda vya korosho vilivyopo hapa nchini vimelazimika kubaki kama “tembo weupe” kwa sababu India inatoa kamisheni ya dola 80 kwa kila kontena la korosho ghafi zinazoingizwa nchini humo kutoka Tanzania na kwingineko.
FikraPevu inauona utaratibu huu kama mkakati wa kimataifa wa kuhujumu jitihada za serikali za kujenga “Tanzania ya viwanda,” na hivyo kuitaka serikali ya Rais Magufuli kuchukua hatua stahiki.
Utangulizi
Hofu na mashaka ya wakulima wapatao asilimia 80 ya raia wote wa Tanzania huanzia katika bei duni ya mazao ya biashara wanayoyavuna na kuyauza ama kwa serikali au kwa wanunuzi wengine. Na kwa upande mwingine, bei bora ya mazao haya huwa chimbuko la furaha na matumaini yao, kwani, kazi ya mikono yao huwawezesha kupata mkate wao wa kila siku na akiba juu.
Kimsingi, furaha yao huwa ni matokeo ya ongezeko la thamani katika namna ambayo inawapatia bei kubwa zaidi katika soko la ndani na nje ya nchi. Kazi ya kuyaongezea thamani mazao huweza kufanyika kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuyakoboa, kuyabangua, kuyachakata na kuyafungasha vizuri zaidi kabla ya kuyafikisha sokoni. Kwa mfano, kahawa iliyokobolewa huwa bei kubwa kuliko kahawa yenye maganda.
Kwa kuutambua ukweli huu, serikali ya Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati anuai ya kuleta mapinduzi ya viwanda katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.
Kuna mkakati wa kuleta mapinduzi ya viwanda katika sekta ya kilimo ulioasisiwa mwaka 2001 kupitia waraka uitwao “Agricultural Sector Development Strategy (ASDS).” Mkakati huu umehuishwa mwaka 2010 kupitia waraka uitwao “Integrated Industrial Development Strategy 2025(IIDS).”
Kwa mujibu wa nyaraka hizi za kiserikali, mikakati hii inao msingi wake katika dhana iitwayo “Agricultural Development Led Industrialisation (ADLI),” kwa Kiingereza.
Kwa ujumla, kupitia mikakati ya aina hii, serikali inalenga kuleta mapinduzi ya viwanda kwa kufungamanisha shughuli za sekta ya viwanda na kilimo katika namna ambayo itawezesha kuongezeka kwa tija inayomaanisha mauzo makubwa ya bidhaa zenye ubora kwenda nchi za nje.
Kielelezo namba 1.0 hapa chini ni njia rahisi ya kueleza muundo wa mkakati wa mapinduzi ya viwanda katika sekta ya kilimo katika Afrika.
Kielelezo Na.1.0: Muundo wa mkakati wa mapinduzi ya viwanda katika sekta ya kilimo. Kielelezo hiki kimeandaliwa na kitengo cha utafiti cha Mtandao wa FikraPevu
Kupitia mikakati hii, mazao ya kilimo yaliyopewa kipaumbele na serikali ni mafuta ya mbegu za alizeti na pamba, korosho, maziwa ya ng’ombe, ngozi za wanyama, na nguo za pamba. Katika makala hii, FikraPevu inatumia zao la korosho ili kuchunguza ni kwa kiasi gani serikali ya Tanzania inafanikiwa katika kutekeleza mikakati yake ya mapinduzi ya viwana kupitia sekta ya kilimo.
Zao la korosho limechaguliwa kwa sababu kuu nne:
Kwanza, ni zao ambalo linawawezesha wakulima wapatao nusu milioni huko kusini mwa Tanzania, kupata mkate wao wa kila siku. Korosho zinalimwa zaidi katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam. Kielelezo namba 2.0 hapa chini kinaonyesha mikoa hiyo.
Kielelezo Na.2.0: Ramani ya Tanzania ikionyesha mikoa ambako korosho inalimwa
Pili, ni zao ambao linafahamika vema kwa Rais Magufuli kama mwanasiasa. Aliliongelea siku ya kutathmini utendaji kazi wake ndani ya mwaka mmoja, alipokutana na waandishi wa vyombo vya habari. Siku hiyo, alisema kwamba, uchumi wa Tanzania sasa unapaa, na kutumia mfano wa kuongezeka maradufu kwa bei ya korosho huko Mtwara kama ushahidi.
Tatu, zao la korosho linafahamika kwa Rais Magufuli kwa sababu za kitaaluma. Katika masomo yake ya shahada ya tatu, aliandika tasnifu ya uzamivu inayohusu mafuta ya ganda la korosho. Kulingana na aina husika, mafuta haya yanaweza kutumika kama kizuizi cha kutu katika vyuma au vanishi ya kuhifadhi mbao.
Jina kamili la andiko la Rais magufuli kuhusu mafuta haya ni, “The potential of anacardic acid self-assembled monolayers from cashew nut shell liquid as corrosion protection coatings,” alilolikabidhi katika Idara ya Kemia ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, hapa Tanzania, mwaka 2009.
Na nne, eneo kubwa waliko wakulima wa korosho ndiko nyumbani kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa. Waswahili husema “ibada njema huanzia nyumbani.” Kwa hiyo, ni vizuri kumkumbusha Waziri Mkuu kutembea maili moja kwa kutatua matatizo ya majirani zake kabla ya kutembea maili kumi kwenda mbali nao.
Zao la korosho na bidhaa zitokanazo na mti wa mkorosho
Korosho ni zao linalotokana na mti wa mkorosho. Korosho inaliwa kama kitafunwa sawa na karanga zinavyotafunwa. Korosho zinaweza kutafunwa bila kukaangwa au baada ya kukaangwa. Pia, korosho zikisagwa zinatumika katika kutengeneza pipi, chokoleti.
Kielelezo Na. 3.0: Picha za mti wa mkorosho, maua ya mkorosho, matunda machanga ya mkorosho na korosho zilizo tayari kwa ajili ya kutafuna
Ndani ya korosho kuna vitamin A, D, na E. Pia kuna madini kama vile Kalsiamu, fosforasi, na chuma. Kwa sababu hii, korosho huwa na bei kubwa, na hatimaye kuwa chakula cha “vigogo” kitokanacho na kazi za mikono ya “walalahoi.”
Tukiweka kando korosho, mti wa mkorosho pia huzalisha matunda ya mkorosho ambayo huweza kutumika kutengeneza bidhaa anuai kama vile kinywaji kikali kiitwacho “gin,” juisi, mvinyo, siagi, na mafuta ya ganda la korosho yaani Cashew Nut Shells Liquid (CNSL).
Wakati wa kuchakata matunda ya mkorosho, maganda yake huzalisha mafuta. Mafuta haya ndiyo yanaitwa “Cashew Nut Shell Liquid” ambayo hutumika kupunguza misuguano, kuzuia kutu, kutengeneza rangi na vanishi ya mbao.
Kielelezo Na. 4.0: Zao la korosho likiwa limepevuka tayari kwa ajili ya kuvunwa
Kwa sababu ya ukosefu wa viwanda bidhaa hizi kutokana na mti wa mkorosho hazijavunwa hata siku moja hapa ndani ya Tanzania. Badala yake zinaagizwa kutoka soko la nje. Hii maana yake ni kwamba bado tunasuasua katika menejimenti ya mnyororo wa thamani ya zao la korosho.
Historia ya viwanda vya kubangua korosho Tanzania
Kazi ya kubangua korosho Tanzania ilianza miaka ya 1960, kupitia kampuni binafsi iliyoitwa African Cashew Processors Company Ltd. Kampuni hii ilisimika kiwanda chake jijini Dar es Salaam mwaka 1965.
Kati ya mwaka 1968 na miaka ya 1970 serikali ya Tanzania, kupitia Bodi ya Korosho ya Tanzania ya wakati huo (Cashewnut Authority of Tanzania (CATA)), ilipata fedha kutoka Benki ya Dunia na kujenga viwanda 12 vyenye uwezo wa kuchakata tani 116,000 kwa siku. Kielelezo namba 5.0 hapa chini kinaonyesha orodha husika.
Kielelezo Na. 5.0: Viwanda vya korosho vilivyoanzishwa na serikali na baadaye kufungwa miaka ya 1970 kwa sababu mbalimbali
Katika miaka ya 1980 uzalishaji wa korosho ulishuka sana kwa sababu mbalimbali. Hivyo, serikali ikaamua kuvifunga viwanda vyote 12. Na baadaye, katika miaka ya 1990, serikali iliamua kubinafsisha viwanda hivyo ili kuona kama vinaweza kufanya kazi kwa ufanisi na kuiwezesha Tanzania kuuza korosho tena katika soko la dunia.
Matarajio ya serikali hayakutimia, kwani mpaka leo ni viwanda vichache tu vinavyofanya kazi, vikiwa vinachakata tani 90 kwa siku, wakati uwezo wake halisi ni kuchakata tani 2,000 kwa siku. Kielelezo namba 6.0 hapa chini kinaonyesha orodha ya viwanda hivyo na uwezo wake wa kubangua korosho.
Na. |
JINA LA KIWANDA |
UWEZO ASILIA (TANI KWA SIKU) |
UWEZO WA SASA (TANI KWA SIKU) |
HALI YA SASA
|
1. |
Olam Tanzania Ltd, P.o. Box 71062 DSM |
16 |
8 |
Kinafanya kazi |
2. |
Mohamed Enterprises (T) Ltd, (Mbagala Cashew Project), P.o.Box 20660 DSM |
8 |
3 |
Kinafanya kazi |
3. |
Korosho Africa Ltd, (Export Trading Co. Ltd), P.o. Box 14301 DSM, P.o.Box 211 TUNDURU |
10 |
3 |
Kinafanya kazi |
4. |
Agro Focus (T) Ltd, (Newala II Factory), p.o.box 32 DSM |
10 |
2 |
Kinafanya kazi |
5. |
Mtwara Cashew Company Ltd, (MCC Factory), P.o.Box MTWARA |
2 |
0.5 |
Kinafanya kazi |
6. |
High Grade Cashew Ltd, P.o.Box 2031 DSM |
2 |
1 |
Kinafanya kazi |
7. |
Uvuki Cashew Processing Ltd, P.o. Box 30880 KIBAHA |
0.6 |
0.5 |
Kinafanya kazi |
8. |
Masasi High Quality Farmers Ltd (Maugula Factory), P.o.Box 136 Masasi |
2 |
1 |
Kinafanya kazi |
9. |
Masasi Processing Factory, P.o.Box … Masasi |
10 |
NILL |
Kimefungwa |
10. |
Ikwiriri Processing Factory, P.o.Box 62 Ikwiriri – Rufiji |
0.3 |
NILL |
Kinajengwa |
11 |
Premier Cashew Industries Ltd, P.o.Box 816 DSM |
NILL |
NILL |
Kimefungwa |
12. |
Cashew Company (2005) Ltd (EOTF LTD), P.o.Box 203 Mtwara |
1.5 |
0.5 |
Kinafanya kazi |
13.
|
Bucco Investment Holdings (T) Ltd, (Lindi Factory), P.o.Box 12806 DSM |
10 |
NILL |
Kimefungwa |
14. |
Bucco Investment Holdings (T) Ltd, (Masasi Factory), P.o.Box 12806 DSM |
10 |
NILL |
Kimefungwa |
15. |
Lindi Farmers Company Ltd, (Mtama Factory), P.o.Box 1024 Lindi |
5 |
NILL |
Kinakarabatiwa |
16.
|
Lindi Farmers Company Ltd, (Nachingwea Factory) – P.o.Box 1024, Nachingwea, Lindi |
5 |
NILL |
Kinakarabatiwa |
17. |
Micronix System (Sindimba Cashewnut Company, Ltd/ Likombe Factory), P.o.Box 40345 DSM |
10 |
NILL |
Kimefungwa |
18. |
Damros Cashew Factory, P.o.Box …. Tanga |
0.3 |
0.1 |
Kinafanya kazi |
19. |
Sonel Cashew Company Ltd, P.o.Box …. Mtwara (Shared with OLAM) |
NILL |
NILL |
Kinafanya kazi |
20. |
Safa Petroleum & Minerals Co. Ltd, (Kibaha Cashew Factory), P.o.Box 110046 DSM |
10 |
NILL |
Kimefungwa |
21. |
Zinga Cashew Factory, P.o.Box … Bagamoyo.
|
0.1 |
NILL |
Kinafanya kazi |
22. |
Perfect Kernels Cashew Factory, P.o.Box … Masasi |
0.3 |
NILL |
Kinajengwa |
23. |
Kitangali Cashew Processing, (UNIDO Cashew Factory) |
2 |
NILL |
Kimefungwa |
24 |
River Valley Food (T) Ltd, (Tandahimba Factory) – P.O.Box 997, Dar es Salaam |
5 |
NILL |
|
25. |
Nariendele Cashew Company Ltd, P.o.Box … Mtwara |
0.3 |
NILL |
Kinafanya kazi |
26. |
Chakama Cashew Company Ltd, |
5 |
NILL |
|
27. |
Southern Jumbo Cashew Ltd, P.o.Box 10832 DSM |
4 |
NILL |
Kinajengwa |
28. |
Newala I Cashew Factory |
10 |
Machine uprooted |
|
29. |
Agro Processing Co. Ltd, P.o.Box 4322 DSM |
2 |
1 |
Mzalishaji wa CNSL |
|
Jumla |
1,929.6 |
89.0 |
|
Kielelezo Na.6.0: Vianda vya korosho vilivyopo leo hii na uwezo wa kila kimoja
Utafiti wa FikraPevu unaonyesha kwamba, sababu zinazokwamisha viwanda hivi ni pamoja na: Teknolojia iliyopitwa na wakati; ukosefu wa mtaji wa kifedha kwa ajili ya kununulia mitambo mipya; ukosefu wa mtaji wa kifedha kutoka katika benki za ndani kwa ajili ya kujenga viwanda vipya; ukosefu wa utaalam stahiki katika menejimenti ya mnyororo wa thamani wa korosho; ukosefu wa taarifa sahihi za wapi vifungashio vya korosho vinapatikana; na ushawishi kutoka masoko ya nje wenye kutoa kamisheni ya dola 80 kwa kila kontena kwa korosho ghafi inayosafirishwa na kupelekwa nchini India.
Mfumo wa taasisi, sera na sheria za kusimamia sekta ya zao la korosho
FikraPevu imebaini kuwa menejimenti ya mnyororo wa thamani wa zao la korosho inajumuisha wadau wengi, kama kielelezo namba 7.0 hapa chini kinavyoonyesha.
Kielelezo Na. 7.0: Mfumo wa wadau muhimu katika menejimenti ya mnyororo wa thamani ya zao la korosho
Wadau hawa wanatajwa na sheria zifuatazo: sheria za kodi, sheria ya usalama wa makazi (OSHA) namba 5 ya 2003; sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6/2004 na kanuni zake za mwaka 2007; sheria ya mazingira; sheria za uwekezaji; sheria za kuingiza ndani na kutoa nje bidhaa; sheria ya kusimamia sekta ya korosho ya mwaka 2009; na sheria ya stakabadhi ghalani namba 10 ya 2005.
Kwa mujibu wa sheria hizi, sekta ya korosho inahusisha sekta ya umma, sekta binafsi, kaya, watu binafsi, vyama vya ushirika wa wakulima wa korosho (AMCOS), viwanda, watafiti, taasisi za fedha, taasisi za bima, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, na Bodi ya Korosho Tanzania, kila mdau akiwa na majukumu yake ya kisheria.
Kwa mfano, wakulima hupanda, kupalilia, kuvuna, kukausha na kukusanya korosho katika maghala yaliyo chini ya vyama vya ushirika (AMCOS). Hapa hulipwa kwa bei ya shambani (farm gate price), ambayo huamuliwa kwa pamoja kupitia utaratibu wa mnada. AMCOS hufanya malipo haya kwa kutumia mikopo kutoka kwenye mabenki.
Vyama vya ushirika (AMCOS) hupeleka korosho viwandani, kusimamia ubanguaji, na kulipa gharama za ubaguaji kwa kwenye viwanda. Viwanda hupanga korosho katika madaraja tofauti, chini ya usimamizi wa Bodi ya Korosho. Aidha, viwanda husambaza mbegu kwa wakulima.
Hali ya sasa ya uzalishaji wa korosho kusini mwa Tanzania
Kwa mujibu wa taarifa rasmi zinazopatikana katika maktaba ya Bodi ya Korosho Tanzania, huko mkoani Mtwara, Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa watatu wa zao la korosho katika Afrika.
Kwa kipindi cha miaka kumi na mbili iliyopita, yaani kati ya msimu wa 2004/5 na msimu wa 2014/15, Tanzania ilizalisha tani za korosho 1,386,582. Asilimia 88 ya mavuno haya imeuzwa nje ya nchi, na kuchangia wastani wa asilimia 15 katika mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa za kilimo katika soko la nje.
Kielelezo namba 8.0 hapa chini kinaonyesha mavuno husika kwa kila mwaka, na kiwango cha korosho hiyo kilichouzwa nchi za nje kama korosho ghafi (raw cashew nut), sehemu kubwa ikiwa imeuzwa nchini India.
Kielelezo na 8.0: Tani za mavuno ya korosho kwa miaka 12 kati ya mwaka 2004/5 na 2015/16 kutoka kwenye mikoa sita yenye mchango mkubwa.
Kwa mujibu wa chanzo cha FikraPevu katika makao makuu ya Bodi ya Korosho Tanzania, wastani wa asilimia 85 hadi 90 ya korosho hii iliuzwa nje ya nchi. Asilimia hii ni sawa na tani za korosho zipatazo 1,247,924.
Kwa wastani, mauzo haya yalichangia asilimia 15 katika mapato ya serikali yenye kutokana na bidhaa za kilimo zinazouzwa nje ya nchi. Mnunuzi mkubwa wa korosho yetu ni taifa la India.
Tanzania inanunua mafuta ya ganda la korosho kutoka India
Pamoja na kwamba Tanzania inauza korosho ghafi kwa India, bado inanunua mafuta ya ganda la zao hilo yanayozalishwa na India kutokana na bidhaa iliyonunuliwa Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania, wastani wa kilo 180,600 za mafuta ya ganda la nazi (“cashew nut shell liquid [CNSL]”), yajulikanayo kama “base phenolic resin,” zinaagizwa na Tanzania kila mwaka kutoka India. Hii ni sawa na rupia 10,389,995 kila mwaka, sawa na shilingi za Kitanzania zipatazo 342,869,835.
Kwa mujibu wa takwimu za mafuta ya ganda la korosho yaitwayo “Cashew Nut Shell Liquid Base Phenolic Resin,” meli zilizoyapakia na kuyaleta Tanzania zilipakiwa kupitia katika bandari mbili huko India, yaani, bandari ya “Nhava Sheva Sea” na bandari ya “Sabarmati ICD.”
Katika mwaka wa 2014, kilo 152,600 zenye thamani ya rupia 9,848,551, zilipakiwa na kuletwa Tanzania, kupitia bandari ya Nhava Sheva Sea.
Kwenye mwaka wa 2015, kilo 146,000 zenye thamani ya rupia 8,697,848, zilipakiwa na kuletwa Tanzania, kupitia bandari mbili za Nhava Sheva Sea na Sabarmati ICD.
Na kwa mwaka 2016, kilo 243,200 zenye thamani ya rupia 12,623,587, zilipakiwa na kuletwa Tanzania, kupitia bandari mbili za Nhava Sheva Sea na Sabarmati ICD.
Kwa ujumla, ndani ya miaka mitatu, kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016, kilo 541,800 zenye thamani ya rupia 31,169,986, zilipakiwa kwenye meli na kuletwa Tanzania, kupitia bandari mbili tofauti za huko India.
Kielelezo namba 9.0 hapa chini kinafupisha takwimu hizi mwaka hadi mwaka, kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016.
Kielelezo Na.9.0: Takwimu za mafuta ya “cashew nut shell liquid” (CNSL) zikiwa zimechujwa kwa mujibu wa mwaka wa kupakiwa na kisha kuchujwa kwa mujibu wa bandari yalikopakiwa mafuta haya
Kwanini tunashindwa kuongeza thamani ya korosho kupitia viwanda vya ndani?
Kwa kuzingatia yote yaliyosemwa hapo juu, FikraPevu ilisumbuliwa na swali moja kubwa: kwa nini tunashindwa kuongeza thamani ya korosho kupitia viwanda vya ndani? Gazeti la FikraPevu lilibaini sababu zifuatazo:
Mosi, teknolojia kongwe katika viwanda vilivyopo nchini kwa sasa.Vilisimikwa siku nyingi, kiasi kwamba, ufufuaji wake leo unamaanisha gharama kubwa karibu sawa na kuanzisha kiwanda kipya.
Pili, ni ukosefu wa mtaji wa kutosha katika mabenki ya ndani kwa ajili ya kuanzisha viwanda vyenye uwezo unaotosheleza mahitaji. Kwa mfano, pesa ya mbegu (seed money) iliyo benki ya TIB ikichukuliwa itajenga kiwanda kimoja tu cha kubangua korosho na benki inakauka.
Tatu, ni ukosefu wa wataalam wenye ufundi wa kufanya menejimenti ya mnyororo wa thamani wa zao la korosho. Kwa mfano, Tanzania ni nchi pekee inayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani. Na mwasisi wa mfumo huu ndani ya Bodi ya Korosho ya Tanzania ni Mohammed Hanga, ambaye aliondoka kwenda masomoni. Mtoa taarifa kutoka kwenye Bodi hii, anaamini kwamba kuondoka kwa mtaalam huyu aliyekuwa Mkuu wa Idara ya TEHAMA na Masoko kumeacha pengo kubwa.
Nne, ni wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalam. Msemaji mmoja kutoka ndani ya Bodi ya Korosho anasema kuwa, japo majukumu ya wadau yapo kisheria, lakini bado baadhi ya wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndani ya mikoa inayolima korosho wanaingilia mamlaka ya Bodi ya Korosho, kiasi cha kuiyumbisha.
Na tano, wafanyabiashara walionunua viwanda vya kubangua korosho, hawataki kuvifufua kwa sababu ya kurubuniwa na India. FikraPevu imeambiwa kwamba, huko India, kuna kamisheni ya dola 80 kwa kila kontena ghafi la korosho linaloingizwa kutoka Tanzania au sehemu nyingine yoyote. Kwa hiyo, ni wazi kwamba ili kupata kamisheni hii, lazima viwanda vya ndani vifungwe milele.
FikraPevu imeambiwa kwamba, hujuma hii inafanikiwa kirahisi kwa kuwa, kuna viwanda sita vikubwa vilivyonunuliwa na mfanyabiashara mmoja tu. Badala ya kubangua yeye na wenzake wanavusha korosho ghafi kwenda India.
Hitimisho, majadiliano na mapendekezo
Kutokana na yaliyojadiliwa hapo juu kuna majumuisho matatu makubwa yako wazi:
Kwanza, ni wazi kwamba sehemu kubwa ya korosho tunayozalisha inauzwa nje ya nchi bila kubanguliwa, kwa kiasi cha asilimia 85 hadi 90.
Na pili, pamoja na kwamba viwanda vya kubangua korosho vilivyopo hapa nchini havina uwezo wa kutosha kuibangua korosho yote inayozalishwa nchini, lakini bado uwezo wake wa kubangua haujatumika kikamilifu katika kuongeza thamani ya zao hilo.
Na tatu, mtaji wa kifedha katika mabenki ya ndani hautoshelezi mahitaji ya kuanzishwa kwa viwanda vya kutosha. Kwa mfano, FikraPevu imeambiwa kwamba, fedha ya mtaji (seed money) iliyoingizwa na serikali katika benki ya TIB, inatosheleza ujenzi wa kiwanda kimoja pekee cha kubangua korosho kwa kasi inayohitajika. Hii maana yake ni kwamba, kuna tatizo la watu kulazimika kufuata mitaji ya kifedha kutoka nchi za nje.
Hivyo basi, ulinganisho wa takwimu za mauzo ya korosho ghafi kutoka Tanzania kwenda India na manunuzi ya mafuta ya ganda la korosho kutoka India kuja Tanzania unazo maana kadhaa kiuchumi.
Kwanza, ukosefu wa viwanda vya kubangua korosho hapa Tanzania unatufanya kupoteza fedha za kigeni kupitia ununuzi wa mafuta ya ganda la korosho.
Pili, kwa kuwa tunauza korosho ghafi, tunauza korosho ambayo haijaongezewa thamani, na hivyo kupata bei ndogo kuliko juhudi ya mkulima inayoingizwa katika uzalishaji kwa mwaka mzima.
Na tatu, usafirishaji wa korosho ghafi kwenda India, unaua ajira hapa Tanzania na badala yake kuzifufua nchini India.
Kwa ujumla, tatizo kubwa ni menejimenti mbaya ya mnyororo wa thamani ya zao la korosho, yenye kutokana na ukosefu wa viwanda imara vya kuongeza thamani ya zao.
Tatizo hili lilichunguzwa kwa kina na Dakta Blandina Kilama, mwaka 2013, alipokamilisha tasnifu yake ya uzamivu yenye jina, “Tofauti za Kiuchumi Kusini mwa Ikweta: Ushahidi Kutoka Sekta za Korosho katika Tanzania na Vietnam,” kupitia Chuo Kikuu cha Leiden, huko Netherlands.
Hii ni tafsiri ya FikraPevu ya maneno ya Kiingereza yafuatayo, “The Diverging South: Comparing the Cashew Sectors of Tanzania and Vietnam.”
Dk. Blandina anaonyesha kwamba, kihistoria, nchi zote mbili ni za kijamaa, zilizofungua milango ya soko huria kuanzia mwaka 1986. Zote pia zinao udongo unaostawisha korosho vizuri.
Kwa sababu hizi, alitarajia wakulima wa korosho nchini Tanzania na Vietinam wawe na hali ya maisha inayoendana. Lakini, akakuta hali ni tofauti sasa. Kwa mshangao akajiuliza, “Ni kwa vipi wakulima wanaolima zao lile lile katika nchi zinazofanana kihistoria na kijiografia kuwa na tofauti kubwa katika viwango vya maisha?(uk. 2).”
Hatimaye, utafiti ukampa Dk. Blandina jawabu lifuatalo: “Attempts at industrialization failed in Tanzania, which led to deindustrialization. Reforms did not allow Tanzania to add value but rather turned the country into a raw cashew exporter without improving the competitiveness of the sector. With reforms that resulted in deindustrialization of the sector, Tanzania lost control of its leading position (uk.147).”
Yaani, (kwa tafsiri isiyo rasmi): “Jitihada za kujenga viwanda nchini Tanzania zilifeli, jambo hili likaleta kifo cha viwanda vingi. Mageuzi yaliyofanyika hayakuweza kuvifufua wala kuongeza thamani ya korosho isipokuwa kuigeuza nchi kuwa mwuuzaji wa korosho ghafi nchi za nje bila kuziongezea thamani. Kufeli kwa mageuzi haya katika sekta ya viwanda kulimaanisha Tanzania kupoteza usukani katika soko la korosho duniani (uk.147).”
Hivyo, Dk. Blandina anahitimisha na kupendekeza jambo, kati ya mengine: “The lack of processing capacity has seen Tanzania continue to be a net exporter of raw cashew, which significantly reduces the sector’s competitiveness… The [crop] value chain needs to be enhanced (uk.148,49).”
Yaani, (kwa tafsiri isiyo rasmi): “Ukosefu wa viwanda vyenye nguvu za kuchakata zao la korosho umeifanya Tanzania kubaki mwuuzaji wa korosho ghafi na hivyo kuifanya msindikizaji katika sekta ya korosho… Kwa vyovyote vile, mnyororo wa thamani wa zao la korosho lazima kuhuishwa (uk.148,149).
Maneno “mnyororo wa thamani,” yanamaanisha mlolongo wa hatua anuai zinazowahusisha wadau mbalimbali katika kubuni, kuzalisha, kuvuna, kukausha, kukusanya, kuchakata, kufungasha, kupanga bei, na kuzisafirisha mpaka kwa wanunuzi na watumiaji.
Hivyo, angalau kwa kuanzia, FikraPevu inawakumbusha Rais wa Tanzania, John Magufuli na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kuchukua hatua za haraka ili kuwapa matumaini “Wamakonde” wa kusini, kwa kufufua viwanda vyao vilivyokumbatiwa na wafanyaiashara wanaofukuzia kamisheni ya kupelekea korosho ghafi huko India badala ya kuzibangulia hapa hapa ndani.
Ripoti hii imekujia kwa kuandaliwa na kitengo maalum cha FikraPevu kilichoamua kufuatilia suala hili kwa karibu.