Rais John Magufuli amesema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aliyokabidhiwa haionyeshi upotevu wa trilioni 1.5 na kwamba ni upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii una lengo la kuigombanisha Serikali na wananchi.
Kauli ya Rais imekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi kutoa kauli inayofanana na ya Rais kuwa hakuna fedha iliyopotea na kilichopo ni kutokueleweka kwa ripoti ya CAG.
Akizungumza leo muda mfupi baada ya kuwaapisha Majaji wa Mahakama, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema aliwasiliana na CAG, Prof. Mussa Assad na kwamba alikiri kuwa hakuna upotevu wa trilioni 1.5 zinazosemekana hazijulikani zilipo.
“Nilikuwa ninasoma baadhi ya mambo mengine wanasema Serikali imeiba trilioni 1.5. Siku moja nikampigia Controller and General Auditor General (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea hapa Ikulu hukunieleza huu wizi wa trilioni 1.5.” amesema Rais Magufuli.
Amesema kama kweli upotevu wa fedha huo ungekuwa umetokea angechukua hatua mapema za kuwafukuza kazi watendaji waliohusika na ufisadi huo lakini kinachoonekana ni upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii na kuwaaminisha wananchi kuwa fedha zimeibwa na Serikali.
“Kwasababu ungenisomea hapo siku hiyohiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyohiyo kwasababu ya hati chafu, hawa trilioni 1.5 uliwaficha wapi? Nimejaribu kusoma kwenye ripoti yako (ripoti ya Ukaguzi ya CAG) sioni mahali palipoandikwa zimepotea trilioni 1.5. Prof. Assad aliniambia hakuna kitu kama hicho, nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho.” Ameeleza Rais Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli hakufafanua trilioni 1.5 zimetumikaje kama kweli hazijapotea, zaidi ya kuwalaumu watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia uhuru wa kutoa maoni kujadili ripoti ya CAG ambayo inaonesha trilioni 1.5 hazijulikani zimetumikaje.
“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwasababu hii mitandao hatuicontrol (hatuisimamii) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara hawajali madhara mtakayoyapata.” Amesema Rais.
Kauli ya Rais imeungwa mkono na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akiwa bungeni Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali juu kutoonekana kwa matumizi ya trilioni 1.5 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
“Kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki.” Amesema Naibu Waziri.
Amesema wakati CAG akifanya ukaguzi wa mahesabu, Serikali ilikuwa inatekeleza mpango mpya wa kimataifa wa mahesabu katika sekta ya umma (International Public-Sector Accounting Standard IPSAS Accural) na kwamba ndio ulioleta mkanganyiko wa mahesabu.
“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer to Zanzibar).” Amesema Naibu Waziri na kuongeza kuwa,
“Katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79.”
Naibu Waziri amefafanua kuwa Matumizi ya trilioni 23.79 hayakujumuisha bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Pia Matumizi hayo yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika.
Ameongeza kuwa, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4. Amedai kuwa trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo ufuatao;
Katika ripoti ya CAG aliyoitoa hivi karibuni katika ukurasa wa 34 imeelezea kwa undani kuhusu kutoonekana kwa matumizi ya fedha hizo, ambapo aliwataka wabunge kuihoji Serikali ziliko trilioni 1.5 kwasababu katika ukaguzi wake hakubaini zimetumikaje ingawa hakusema zimepotea.
Tangu kutolewa kwa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na mashirika mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha unaoishia June 2017. Mijadala mbalimbali imeendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mambo mbalimbali yaliyoibuliwa na CAG ikiwemo kutojulikana kwa matumizi ya trilioni 1.5.
Baadhi ya vyama vikiwemo vya CCM, ACT-Wazalendo na CHADEMA vilitoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekuwa alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa ukaguzi wa CAG ulihusisha fedha zilizokusanywa na sio za hati fungani ambazo Serikali imezitolea maelezo.