Serikali inajali thamani ya fedha kuliko damu salama

Gordon Kalulunga

Thamani ya vifo vya watu vinavyotokana na kukosa damu haithaminiki. Bali thamani ya fedha za posho kwa watumishi wa kitengo cha damu salama ndiyo serikali inaona ni hasara kubwa.

Hali hiyo inajidhihilisha katika kitengo cha damu salama kanda ya nyanda za juu kusini inayounganisha mikoa mitano ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi.

Damu inasafirishwa kwenye magari ya abiria kutoka katika benki ya damu iliyopo katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha wazazi maarufu kama Meta tofauti na tamko la sera ya afya ya mwaka 2007.

Sera hiyo ya afya katika kipengele chake namba 5.4.6 kinachohusu damu sama kinasema kuwa mfumo wa damu salama unaotumika kwa sasa nchini ni ule wa kila hospitali kuwa na utaratibu wake wa kukusanya, kupima na kutumia damu.

Aidha, mfumo huu unategemea zaidi ukusanyaji wa damu kutoka kwa ndugu wa wagonjwa kuliko kwa watoa damu wa kujitolea kwa hiari.

Mfumo huu unasababisha kuwepo kwa uhaba wa damu na uwezekano wa maambukizo ya magonjwa yanayotokana na kuongezewa damu yenye matatizo au ugonjwa kama vile; UKIMWI, Kaswende, Homa ya Ini “Hepatitis B na Hepatitis C”.
(b) Madhumuni
Kuimarisha mfumo wa kitaifa ambao unasimamia ukusanyaji, upimaji, utunzaji, usambazaji na matumizi ya damu salama nchini.
(c) Tamko la sera
Serikali itaandaa na kusimamia sheria, kanuni, miongozo na taratibu (i) za upatikanaji na matumizi ya damu salama.
Serikali itaboresha mazingira kwa wananchi, kuwawezesha kutoa (ii) damu kwa hiari.

Serikali kwa kushirikiana na wadau itaimarisha miundombinu ya (iii) upatikanaji, utunzaji na usambazaji wa damu salama.

Wananchi watahamasishwa, ili kuchangia huduma za upatikanaji wa (iv) damu salama.

Hali ilivyo kwa sasa katika kanda hiyo ya nyanda za juu kusini ni kwamba baada ya kupata damu hizo kutoka kwa watu waliojitokeza kuchangia kwa hiari, inapopelekwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa, damu hiyo inasafirishwa kwa basi la kampuni ya Sumry kwa kulipa Sh. 10,000 kwa mujibu wa viongozi wa benki kuu kanda ya nyanda za juu kusini.Tofauti na sera inavyosema.

Damu hiyo ya binadamu hasa iliyopimwa na kuthibitika kuwa ni salama na kupangwa katika madaraja yake ikiwemo group A, O,… inapakiwa kwenye chupa kisha chupa hizo hupangwa kwenye maboksi (Pichani) kama yanayouziwa barafu mahala pengi nchini hasa mijini.

Ili kujua wahusika wanasemaje, nimetembelea katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha wazazi Meta Jijini Mbeya ili kuhojiana na viongozi wa benki ya damu salama kanda ya nyanda za juu kusini.

Mtu wa kwanza kukutana naye ni afisa tawala wa kitengo hicho katika kanda hiyo (Zonal Administrator) Sariah Kundael ambaye kwanza ananiomba kitambulisho ili anitambue na anapiga simu kwa Meneja wake.

Nilimpatia kitambulisho changu na alipokisoma na kujibiwa na meneja wake kuwa anaweza kuhojiana nami kwasababu anafahamu jina langu na kazi yangu, anaanza kwa kusema kuwa kitengo hicho kipo chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii na kilianzishwa mwaka 2005.

Anasema kitengo cha damu salama kinahusika katika kukusanya damu, kuipima, kusambaza na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wananchi kujitolea damu.

Damu hiyo inapimwa kwa kuangalia magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa homa ya Ini, kaswende na virusi vya Ukimwi (VVU).

‘’Damu inahitajika kwa wingi sana kutokana na mahitaji ya wagonjwa wenye uhitaji wakiwemo wanaopata ajali na wengine’’ anasema Kundael.

Anaeleza kuwa kikosi kinachohusika katika kutoa elimu kwa wananchi ili wahamasike kujitolea damu kinakuwa na wataalam wasiopungua saba ambao mmoja wapo ni mtaalam wa kutafuta mishipa, takwimu, ubora/wingi wa damu katika mwili wa anayetaka kutoa damu na mtu wa ushauri nasaha.

Nilipotoka katika ofisi ya afisa tawala huyo, alinisindikiza mpaka katika ofisi ya meneja wa kitengo hicho kanda hiyo Dr. Baliyima Lelo.

Dr. Lelo ananipokea vizuri sana na tunaanza mahojiano naye ambapo anakiri kuwa damu hiyo baada ya kupimwa na kuthibitika kuwa ni salama katika benki hiyo ya damu salama, husafirishwa kwa mabasi.

Kwa upande wa kupeleka mkoa wa Rukwa wanatumia basi za kampuni ya Sumry na kwenda mikoa ya Iringa na mingine mara nyingine anasema hutumia mabasi madogo ya abiria maarufu kama Coaster.

Je damu hiyo inaposafirishwa kunakuwa na usimamizi wowote?
‘’Hakuna mtaalam yeyote anayesindikiza damu hiyo kutokana na gharama kubwa za kuwalipa wataalam hao’’ anasema Dr. Lelo.

‘’Tunaamua kusafirisha damu hiyo kwa kutumia mabasi kutokana na gharama kubwa za kumlipa dereva, mtaalam na ununuzi wa mafuta na hatujawahi kupata tatizo lolote kuhusu damu hiyo’’ anaeleza Meneja huyo wa damu salama kanda ya nyanda za juu kusini.

Namuuliza kuwa ni mkoa gani kati ya mikoa hiyo yenye matumizi makubwa ya damu na matumizi makubwa ya damu hiyo ni kwa wahitaji wepi, waliopata ajali, wajawazito, upungufu wa kawaida au upasuaji?

Dr. Lelo anasema kuwa mkoa unaoongoza kwa matumizi makubwa ya damu ni mkoa wa Mbeya na kundi kubwa linaloongoza kwa kutumia damu hiyo salama ni wajawazito, watoto wadogo huku wakifuatia watu wanaopata ajali.

‘’Matumizi makubwa ni kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano wanaoumwa Maralia na watu wanaopata ajali kisha upasuaji wa kawaida’’ anasema Dr. Lelo.

Anasema watu wanaopaswa na kuruhusiwa kuchangia damu ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 18-65 na jambo hilo analitaja kuwa ni la kizalendo kwasababu damu ya kuongezewa mwanadamu haipatikani kwenye miti bali kwa watu wenyewe.

Namuuliza kama kanda hiyo inatimiza malengo ya shirika la afya duniani WHO ambayo yanataka kila mwaka damu ikusanywe unit 45,000.

Anafafanua kuwa kwa mwaka 2012 malengo hayo hayajaweza kutimia kwa kanda hiyo ambapo walikusanya unit 18,000 tu.

Anataja baadhi ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo katika upatikanaji wa damu kuwa ni pamoja na misingi ya imani ambapo baadhi ya imani za dini haziruhusu waumini wake kutoa wala kuogezewa damu.

‘’Tuhuma za kuwauzia damu salama baadhi ya wagonjwa/ndugu zao zinazoelekezwa kwa baadhi ya watumishi wa hospitali nchini zinazohusika kutoa huduma za kuwaongezea wagonjwa damu salama ni kikwazo cha wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari’’anasema Dr. Lelo.

Mmiliki wa mabasi ya Sumry High Class Salum Sumry anakiri kuwa hapo awali mabasi yake yalikuwa yakisafirisha damu kutoka Mbeya hadi Sumbawanga kwa matumizi ya Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga .

Anasema damu hiyo ilikuwa ikisafirisha katika hali ya usalama wa hali ya juu licha ya ufungaji wa damu hiyo lakini mabasi yake katika buti zake kuna chumba maalumu kwa ajili ya kuhifadhia damu hiyo ambapo inasafirishwa na kufikishwa salama.

“Tangu tuanzze kusafirisha damu hatujawahi kupatikana na dosari yoyote au tuhuma ya kuwa imesafirishwa katika mazingira mabaya “ alisisitiza .

Kuhusu malipo : Anakiri kuwa hapo awali kulikuwa na gharama ya kuisafirisha damu hiyo hadi pale Uongozi wa Msalaba Mwekundu alipopewa jukumu na Serikali la kusafirisha damu hiyo ambapo baadaye uliwasiliana nae na kukubaliana kuwa Sumry ataendelea kuisafirisha damu hiyo ila sasa inasafirishwa bure.

Kupitia makala haya naamini kuwa serikali itatimiza wajibu wake kuhakikisha damu inasafirishwa kwa gharama yeyote kutokana na unyeti wake maana damu haipatikani kwenye miti bali kwa binadamu na wazalendo wanaojali maisha yaw engine

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749, barua pepe;[email protected] na WEB; www.kalulunga.com

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *