Serikali kutoa chanjo kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya kizazi

Jamii Africa

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani 50,000 huku Saratani ya mlango wa kizazi ikiongoza ikifuatiwa na saratani ya matiti na saratani ya ngozi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu wakati wa mkutano na viongozi wa dini, uliofanyika jana jijini Dar es salaam ambapo amesema wagonjwa wa saratani wameongezeka huku saratani ya shingo ya kizazi ikishika nafasi ya kwanza.

“Kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wa Saratani wapya 50,000, katika kila wagonjwa 100 wanaokwenda katika Hospitali ya Ocean Road, wagonjwa 32 wana saratani ya mlango wa kizazi, inafuatia saratani ya matiti ambayo takribani wagonjwa 12 katika wagonjwa 100, saratani ya tatu ni saratani ya Ngozi” alisema Waziri Ummy..

Ameongeza kuwa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinachukua takribani asilimia 45 ya wagonjwa wote wa saratani nchini, huku Saratani ya tezi dume ikiwa na asilimia 2.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy Mwalimu amewaomba viongozi wa madhehebu ya dini kuwahimiza wananchi kuwapeleka wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kupata chanjo ya kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 10 Aprili, 2018 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam

Waziri Ummy amesema kwamba “kama viongozi wa dini ni vyema kufikisha ujumbe huu kwa waumini wao na kuwaunga mkono ili kuweza kuwafikia wasichana laki 6 nchi nzima ili kuweza kuwaokoa na vifo vipatavyo asilimia 50 vitokanavyo na saratani nchini. Idadi hii ni kubwa sana,hivyo juhudi na ushirikiano zaidi vinahitajika katika kupunguza vifo hivi”

Hata hivyo aliwatoa hofu viongozi hao pamoja na wananchi kwa ujumla kwamba chanjo hii haimzuii msichana kutopata watoto katika maisha yake ya baadae bali ni kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi. “Kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni vyema tukashirikiana kuweza kuwaokoa mabinti zetu na vifo”.


Hali ilivyo sasa.
Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani nchini. Takwimu za mwaka 2016/2017 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kwamba Saratani zinaoongoza nchini ni: Saratani ya Kizazi (32.8%), Matiti (12.9%), Ngozi (Kaposis Sarcoma) (11.7%), Kichwa na Shingo (7.6%), Matezi​(5.5%), Damu (4.3%), Kibofu cha Mkojo (3.2%), Ngozi (Skin) (2.8%), Macho (2.4%) na Tezi Dume (2.3%)

Takwimu zinaonesha kuwa wagonjwa wa saratani walioripoti katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI) waliongezeka kutoka 3,776 mwaka 2013 hadi 4,195 mwaka 2014 ambapo mwaka 2015 walifikia 5,529 na mwaka 2016 walifikia 6,340.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Taasisisi ya Kansa ya Ocean Road, Dkt. Chrispin Kahesa wakati akihojiwa na shirika la habari la BBC kuhusu Saratani kuwa tishio kwa watu wengi hasa nchi zinazoendelea alisema, “Sababu ya kwanza inaweza kuwa mabadiliko ya tabia za maisha kwa wananchi wa nchi zinazoendelea ni kwamba watu wengi hawafanyi mazoezi na wanakula vyakula vinavyoongeza uzito na pia kuongeza maambukizi ya saratani ikiwemo matumizi ya pombe”.

Ameongeza kwa kusema kuwa, “Pia saratani ya shingo ya kizazi imeshamiri sana kwa akina mama na kuongezeka kwake ni kutokana na maradhi yanayopatikana kwa njia ya zinaa kutoka kwa kirusi cha ‘papiroma’ na maradhi haya yameshamiri sana kwenye nchi za ukanda wa Afrika ambapo maambukizi ya UKIMWI ni makubwa sana”.

Akizungumzia juu ya dezi dume kwa wanaume amesema, “Na kwa upande wa tezi dume kwa wanaume ni saratani ambayo inawashika watu wenye umri mkubwa yaani miaka zaidi ya 50 na kuendelea”.

Saratani inachukua nafasi ya 5 kwa nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania katika maradhi yanayosababisha vifo vingi vya watu. Na kwa Tanzania saratani ya mlango wa kikazi ndio inashika nafasi ya 2 kwa kusababisha vifo vingi.

“Karibu asilimia 38 ya wagonjwa wanapokelewa katika kituo hiki wanaugua saratani ya mlango wa kizazi hivyo ni saratani ambayo ipo kwa kiwango cha juu sana nchini Tanzania”. amesema Dkt. Kahesa.

Mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri Ummy alipokea mashine 100 za tiba mgando (cryotherapy), mashine 9 za upasuaji mdogo (LEEP) kwa matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake na mitungi 173 ya gesi ya ukaa (carbondioxide) itakayowezesha mashine hizo kufanya kazi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *