Serikali yadaiwa kuibagua Musoma misaada ya Mafuriko; Kisa kuchagua CHADEMA?

Jamii Africa

Waziri Mkuu Mizengo PindaOFISI ya Waziri Kuu kitengo cha Maafa, imetupiwa lawama nzito na wananchi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara, wakiwemo waathirika wa mafuriko katika manispaa hiyo, kwa kile kinachodaiwa kushindwa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Imeelezwa kwamba, licha ya ofisi ya Waziri Mkuu kupewa taarifa rasmi kuhusiana na maafa hayo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha Novemba 25 mwaka huu, hadi sasa haijapeleka msaada wowote kwa wananchi hao, na kwamba hiyo huenda inatokana na Serikali kutaka kuwakomoa wananchi wa Musoma kutokana na maamuzi yao ya kuwachagua viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wakizungumza leo kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wakiwemo waathirika na viongozi wa Manispaa ya Musoma walieleza kusikitishwa kwao na kitendo cha Serikali kushindwa kupeleka haraka misaada kwa waathirika hao wa mvua, na wamesema kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na jamii yote.

“Tunashangaa sana kuona Waziri Mkuu anashindwa kuleta misaada kwa waathirika wa mafuriko Musoma!. Hiki ni kitendo kibaya sana na tunakilaani. Kama Pinda alikimbia haraka haraka kwenye mafuriko huko Monduli kwa Lowassa, iweje ashindwe kuja Musoma?. Kashindwa nini hata kututumia misaada?.

“Haiwezekani Serikali ikatae kusaidia wananchi wake. Au inafanya hivyo kwa kutukomoa kwa maamuzi yetu ya Kikatiba kuchagua viongozi wa Chadema?. CCM hapa imekufa, tunamtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais walitutangazie hili ili kama tunakufa tufe huku tukiwalaani”, alisema mmoja wa waathirika aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwita.

Hata hivyo, wananchi na waathirika hao wa mafuriko Musoma, waziomba Jumuiya za Kimataifa, taasisi, mashirika na makampuni mbali mbali kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wananchi hao, kwani wapo katika hali mbaya, na wanaendelea kuishi kwenye madarasa ya shule na ofisi za Kata.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Musoma mjini, Vincent Nyerere (Chadema), alisema: “Hata mimi nasikitika sana kuona Serikali inashindwa kuwaletea misaada wananchi wa jimbo langu waliokumbwa na maafa ya mvua. Na hii ni mara ya pili Serikali kufanya hivyo, maana hata maafa ya mwezi wa tatu pia Serikali haikuleta msaada wowote Musoma.

Hata hivyo, Nyerere alisema kitendo kinachofanywa na Serikali si cha kiungwana hata kidogo, na kwamba inaonekana huenda inafanya hivyo kwa makusudi kutokana na mambo ya kisiasa, na alimuomba Waziri Mkuu, Pinda kuhakikisha ofisi yake inatuma misaada kwa waathirika hao ambao hali zao siyo nzuri.

Mbunge huyo alimlaumu pia Mkuu wa Wilaya ya Musoma kwa kitendo chake cha kuchelewa kupeleka taarifa za maafa hayo kwa ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwa ni pmoja na kuonekana kushindwa kufuatilia na kutia msukumo kuwahishwa misaada hiyo, na kwamba hali hiyo inawaumiza sana wananchi, na kamwe suala hilo lisichukuliwe kisiasa.

Naye Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kisurura (Chadema), alisema Manispaa imelazimika kujitolea kugawa tani 7 na nusu za unga wa sembe na tani moja na kilo 250 za maharage kwa zaidi ya familia 300 zilizoathirika mafuriko ya mvua iliyonyesha Novemba 25 mwaka huu na kusababisha miundombinu yote kuharibika vibaya.

Kwa mujibu wa Meya huyo wa Musoma, misaada hiyo ya chakula yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni tano waliisambaza juzi kwa kutumia fedha za mfuko wa ndani wa maendeleo, na kwamba kitendo cha Ofisi ya Waziri Mkuu kukaa kimya katika hilo kinasikitisha mno!.

Meya Kisurura alisema: “Kata zilizopewa msaada huo wa chakula kupitia waathirika hao wa mafuriko ni pamoja na Bweri, Kitaji, Iringo, Mwigobero, Mwisenge, Makoko, Buhare, Nyamatare, Kigera na Kata ya Nyasho. Kata za Kamunyonge na Mkendo hazikuthiriwa na mvua hiyo kubwa”.

Na Sitta Tumma.

2 Comments
  • kwa uchungu mkubwa na penda kutoa pole kwa aathirika wote wa mafuriko hapo musomo”pia kwa uchungu mkubwa na ionya serikali kwa kuendeleza siasa za ubaguzi ktk mikoa na majimbo kwani kamwe hatuwezi pata maendeleo yenye usawa kwa hali ya kuendeleza chuki na uhasama baada ya siasa,jipeni moyo mkuu viongozi wa chadema mkoani hapo hakika ukombozi/mwanga upo karibu kuimulika tz yote na kamwe Nuru hauwezi shindwa na giza’serikali ijue halimbaya ya afya au kifo chochote wao pia ndiyo watakuwa wahusika kwa uzembe”mbona huyu Pinda na mkulo Kilosa walisaidia sana tu na kwa haraka?
    Tunaona hata mkoa wa Moshi maendeleo yake yanenda taratibu sababu ya wao kuchagua Chadema,hii ni hatari kwa kweli kuongozwa na serikali yenye hila na chuki kwa wasema kweli na watetea haki”Siasa za Tz zimeharibiwa na ccm kwani tumesha shuhudia hata wafanyabishara wakubwa wasio ccm huwa wakichangia upinzani wanatishiwa na hata kufilisiwa”serikali gani inayo jifanya inaleta demokrasia ya usawa kumbe ni unafki ulio wazi”Ni onyo natoa kwa serikali kuacha giliba hizo wasicheze na uhai wawatu na maendeleo ya watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *