Sheikh Ponda ajisalimisha polisi kujibu tuhuma za uchochezi

Jamii Africa
DAR: Sheikh Ponda aripoti Polisi kama alivyotakiwa kufanya ndani ya siku 3. Aambatana na Wanasheria wakiongozwa na Profesa Safari. . Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar, SACP Lazaro Mambosasa alimtaka Sheikh Ponda kufika Kituo cha Polisi kwa tuhuma za uchochezi na kuikejeli Serikali.

Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amejisalimisha mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano juu ya kauli alizotoa hivi karibuni.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya wito wa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa kumtaka Sheikh Ponda kujisalimisha polisi kwa ajili ya mahojiano juu ya kauli aliyotoa tarehe 11 Oktaba mwaka huu ambayo inadhaniwa kuwa yalikuwa na maudhui ya uchochezi.

Kamanda Mambosasa alinukuliwa jana wakati akiongea na vyombo vya habari kuwa;

“Ametenda makosa ya jinai kama uchochezi, lakini pia amekuwa anatoa lugha ambazo ni za kejeli, dhidi ya serikali, anatafutwa na kama unamjua mwambie ajisalimishe ili tuweze kumhoji, kukimbia hakutomsaidia, tukiona kuna kosa la jinai tutampeleka mahakamani kama hana tutamwachia, mimi nampa siku tatu lakini akija leo ni nzuri zaidi, nampa siku 3 ajitokeze mwenyewe aweze kuhojiwa, vinginevyo hatakuwa salama,”

Juhudi za kumtafuta Sheikh Ponda zilianza juzi wakati akifanya mkutano na waandishi wa habari, ambapo Polisi walivamia mkutano huo lakini hawakufanikiwa kumkamata kwa kuwa alikuwa tayari ameondoka eneo la tukio.

Taarifa zinasema kuwa Sheikh Ponda ametii wito wa Jeshi la Polisi na mapema leo asubuhi amejisalimisha katika Kituo Cha Kati cha Polisi kwa ajili ya mahojiano ambayo kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa yanalenga kubaini kama alitoa kauli za uchochezi wakati akiongea na waandishi wa habari.

Sheikh Issa Ponda

Ikumbukwe kuwa Sheikh Ponda amekuwa mkimya kwa muda mrefu kabla ya kuibuka tena ambapo alianza kwa kumtembelea na kumjulia hali Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu ambaye anapata matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Lisu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, septemba 7 mwaka huu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika makazi yake mjini Dodoma muda mfupi baada ya kumaliziki kwa vikao vya Bunge.

Baada ya kurejea kutoka Nairobi, septemba 11 mwaka huu Sheikh Ponda alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia hali ya Tundu Lisu na kuitaka serikali kuchunguza na kuwachukulia hatua watu wasiojulikana ambao wanajihusisha na matukio ya kupiga watu risasi.

Akitolea mfano wake, Sheikh Ponda anasema alipigwa risasi mwaka 2013 katika mhadhara wa Waislamu ambao ulikuwa unafanyika katika shule ya msingi Kiwanja cha Ndege mkoani Morogoro.

Sheikh Ponda anajulikana zaidi kama mwanaharakati wa dini ya kiislamu. Kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ambayo kwa nyakati tofauti inatajwa kutetea maslai ya waislamu nchini.

Kutokana na misimamo na kauli zake zimemfanya kuingia katika misukosuko na kuvutana na serikali akidaiwa kuchochea wananchi. Mwaka 2012 akiwa na baadhi ya wenzake walianzisha kampeni ya kupinga watu kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi lakini alidhibitiwa na serikali na yeye mwenyewe kushiriki katika zoezi hilo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *