KIGOMA IJUMAA APRILI 6, 2012. Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyankwi kilichopo katika Kata ya Busunzu Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma Tora Muhoza(42), amesalimisha silaha moja ya kivita aina ya SMG ikiwa na sirasi mbili kwenye magazine yake.
Silaha hiyo yenye namba BA 178645 ilisalimishwa kwa Mtendaji wa Kata ya Busunzu na baadaye kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma SSP Kihenya wa Kihenya, amesema ya kuwa kusalimishwa kwa silaha hiyo kunatokana na msako mkali unaoendeshwa na Jeshi hilo baada ya muda uliotolewa na serikali wa kusalimisha silaha kumalizika.
Kamanda Kihenya amesema kuwa pamoja na kumalizika kwa muda huo, lakini Jeshi la Polisi limeacha kumchukulia hatua mwananchi huyo kutokana na kuamua kujitokeza hadharani kwa hiari kuisalimisha silaha hiyo kwa mtendaji wa kakta hiyo.
Katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inaendelea kudumu mkoani Kigoma, Jeshi la Polisi limeendelea kufanya operesheni ya kupambana na vitendo mbalimbali vya kihalifu vikiwemo vya kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Kamanda Kihenya amesema kuwa hiyo ni silaha ya tatu kusalishwa mkoani humo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Amesema pamoja na kusalishwa kwa silaha hizo aina ya SMG pamoja na risasi kadhaa, Polisi pia imewakamata watuhumiwa 11 wakiwemo wa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.
Jeshi la Polisi mkoani humo limeendelea kutoa wito kwa wananchi mkoani humo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi mara wanapobaini kuwepo kwa makundi ya wahalifu ama mhalifu mmoja mmoja ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Imeandikwa na Pardon Mbwate na Felister Elias, wa Jeshi la Polisi Kigoma na kupitiwa na Mohammed Mhina, Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar