ASASI inayojishughulisha na utoaji elimu, haki za watoto, utunzaji wa mazingira, haki na wajibu kwa wanawake hapa nchini (TABCO), imesema ipo haja kwa Serikali kupitia Bunge kuangalia upya namna ya kutunga sera na sheria mpya zinazomlinda mwanamke katika kupata haki za mirathi, ili kuisaidia jamii hiyo kuzulumiwa haki zake.
Imesema, kulingana na matatizo mengi yanawayokumba wanawake hasa katika kupewa haki za kumiliki mirathi, Serikali kupitia mamlaka zake inao wajibu wa kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa, ikiwa ni pamoja na wahusika wote wanaoonekana kuvunja na kukiuka sheria za mirathi wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ombi hilo limetolewa hii leo jijini Mwanza na Mkurugenzi Mtendaji wa TABCO, Irene Kyamba, wakati alipokuwa akizungumza na FikraPevu muda mfupi baada ya kumalizika semina ya mafunzo juu ya haki na wajibu kwa wanawake katika kumiliki mirathi, katika ukumbi wa PK Hoteli jijini hapa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa TABCO, uwepo wa sera na sheria hiyo mpya dhidi ya wanawake na urithi wa mirathi ni muhimu sana katika kuwasaidia wanawake, ambao kwa sasa bado wengi wao wananyanyasika na kukosa haki zao za msingi, hivyo ni vema serikali ikatilia mkazo kutunga sheria hiyo kwa faida ya taifa.
“TABCO tunaiomba sana Serikali iangalie upya sera ya wanawake. Hasa upande wa kumiliki mirathi, maana wanawake wengi kwa sasa bado wanakumbana na tatizo kubwa la kupoteza haki zao za umiliki wa mirathi. Kwa maana hiyo, TABCO inalishauri Bunge na Serikali yote kwa ujumla ihakikishe haki za watoto na wanawake zinalindwa kisheria. Hii itasaidia sana watu wanyonge kupata haki zao”, alisema Mkurugenzi huyo wa TABCO, Kyamba.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, FikraPevu – Mwanza