UWEPO wa watoto katika familia ni furaha kwa wanandoa, wengi huamini kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Wazazi wanawekeza fedha na muda mwingi kuwalinda na kuwakuza katika mwenendo mzuri wa maisha.
Licha ya jamii kufanya jitihada kuwalinda watoto, FikraPevu inafahamu kwamba, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na wengi wao hufariki kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano.
Tafiti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) zinaeleza kuwa kila siku zaidi ya watoto wachanga 100 hufariki nchini Tanzania kutokana na maambukizi, matatizo yanayojitokeza wakati wa kuzaliwa kama vile kupumua kwa shida na matatizo yanayotokana na kuzaliwa kabla ya muda.
Vifo vya watoto wachanga vinachangia hadi asilimia 40 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Watoto wanaozaliwa kabla ya muda (watoto njiti) ni miongoni mwa tatizo kubwa linalowapata watoto wengi ambao hupoteza maisha baada ya kuzaliwa.
Kiongozi wa Wodi ya Kangaroo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Muuguzi Cleopatra Mtei anasema watoto njiti ni wale wanaozaliwa kabla ya muda wao kuanzia wiki 28 hadi 34, uzito wao huanzia gramu 500 hadi 1,500.
“Hawa watoto wanapungukiwa na damu sana kutokana na jinsi wanavyozaliwa. Unakuta ile mifupa ya chembechembe nyekundu inakuwa bado. Hivyo wanapokuwa hapa tunawapa dawa zitakazowawezesha kutengeneza chembechembe za damu na dawa za matunda,” anasema Muuguzi huyo.
“Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa, mfumo wa chakula na mfumo wa fahamu ukilinganisha na watoto waliozaliwa baada ya kutimiza wiki 37 au zaidi wakiwa tumboni mwa mama zao.”
Ripoti ya UNICEF inaeleza kuwa nchini Tanzania, kila mwaka, watoto takribani 213,000 huzaliwa mapema sana kabla ya muda wao (watoto njiti) na zaidi ya 9,000 miongoni mwao hufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa mapema mno.
Idadi hii ni takribani robo ya watoto wachanga 40,000 wanaofariki kila mwaka hapa nchini.
Vifo kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa kabla ya muda kutimia ni sababu kubwa ya pili inayosababisha vifo vya watoto wachanga Tanzania.
Sababu zinazosababisha watoto wengi wazaliwe kabla ya umri ni pamoja na wajawazito kuwa na shinikizo la damu, kifafa cha mimba, upungufu wa damu, maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Pia magonjwa ya zinaa, mama kutokwa na damu kabla mimba haijakomaa, malaria, mimba za utotoni, utumiaji wa vilevi mfano pombe, sigara na dawa za kulevya pamoja na kufanya kazi ngumu wakati wa ujauzito.
Kutokana na idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda, kuongezeka kwa kasi, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza tatizo hilo ikiwamo kujenga wodi ya Kangaroo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuokoa maisha ya watoto hao.
Wodi ya Kangaroo ni maalumu kwa watoto njiti ambapo wataalamu hutumia Njia ya Kangaroo kuokoa maisha ya watoto hao kwa kuwaweka karibu na mama zao ili wapate joto linalohitajika katika miili yao.
“Njia ya Kangaroo ni mwambatano wa ngozi kwa ngozi au mtoto anawekwa ngozi kwa ngozi na mama yake ili apate joto. Kangaroo ni njia ya kuokoa maisha ya mtoto njiti kwa sababu anapata joto halisi la mama,” anaeleza Muuguzi huyo wa Hospitali ya Muhimbili.
“Mtoto anawekwa kifuani kwa mama yake, joto la kifuani ni sawa sawa na joto la tumboni, pia ni rahisi mama kugundua hali ya mtoto kama imebadilika kwa kuwa yuko naye muda wote. Njia ya Kangaroo inapunguza vifo vya watoto njiti.”
Njia ya Kangaroo imesaidia kuokoa maisha ya watoto wengi wanaozaliwa kabla ya muda wao kwa sababu haina gharama na ni rafiki kwa mtoto.
Kutokana na huduma nzuri inayotolewa katika Wodi ya Kangaroo, katika kipindi cha miezi miwili (Januari-Februari) mwaka huu, wodi hiyo imepokea watoto zaidi ya 200 waliozaliwa kabla ya muda wao. Idadi hiyo ya watoto ni kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pekee.
Licha ya watoto hao kuzaliwa wanaweza kupata matatizo ya kiafya katika ukuaji wao na kuathiri uwezo wa kujifunza na kupokea maarifa mapya.
Ripoti ya UNICEF (2014) inaeleza kuwa; “Watoto njiti pia wapo katika hatari ya kupata matatizo ya kuona, kusikia, kutambua/kiakili na moyo yanayoweza kudumu maisha yao yote. Zaidi ya hapo watoto wanaozaliwa njiti katika nchi zilizo na uchumi duni wapo katika hatari ya kufa mara 10 zaidi ya nchi zilizoendelea.”
Wadau wa masuala ya afya wanaishauri serikali kuongeza wigo wa utoaji huduma za afya na kuifikisha elimu ya uzazi kwa jamii ili kuchukua tahadhari za kiafya.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Dk. Jama Gulaid, anasema: “Watoto wachanga wanahitaji kupata huduma muhimu hususan kwa wale ambao wanazaliwa kabla ya muda wao.
“Hii inajumuisha kuwakausha, kuwapa joto na kuwaweka safi, kuwaanzisha kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa na kuhakikisha kwamba watoto wanaopata shida kupumua wanapata huduma na uangalizi wa haraka. Dakika ya kwanza baada ya kuzaliwa ni dakika ya dhahabu (golden minute) kwa kila mtoto mchanga.”
Hata hivyo, sehemu kubwa ya sababu zinazofanya watoto kuzaliwa kabla ya muda wao hazijulikani. Tafiti zaidi zinatakiwa kufanyika ili kupata uelewa na suluhisho la jambo hili nchini Tanzania.