Pamoja na Tanzania kufaidika kiuchumi kutokana na ujenzi wa bomba la Mafuta toka Kabaale, Uganda hadi jijini Tanga, bado itapata hisa za asilimia 8 katika uendeshaji wa shughuli za uzalishaji mafuta..
Mradi huo wa bomba la mafuta ambao una urefu wa kilomita 1,445 ambao umeanza kujengwa umetajwa kuwa na manufaa kwa pande zote mbili ikizingatiwa kuwa mafuta hayo yatasafirishwa kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga kabla ya kuuzwa katika nchi nyingine.
Kulingana na Jarida la The Guardian linaeleza kuwa uchimbaji wa mafuta katika mji wa Kabaale uliopo Wilaya ya Hoima unatarajiwa kuanza 2018 baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba hilo ambalo litagharimu Dola za Marekani bilioni 4 mpaka kukamilika kwake.
“Kenya imesema itachukua hisa za 2.5% za uchimbaji mafuta , Tanzania itachukua 8%. Mtambo wa kusafisha mafuta unatarajia kuanza 2018 na kuzalisha mapipa 60,000 ya mafuta kwa siku na Uganda itaanza kusafirisha mafuta mwaka 2020”, linaeleza jarida hilo.
Licha ya Tanzania kuwa sehemu ya wadau wa uzalishaji mafuta hayo ambayo yanapatikana katika Ziwa Albert nchi Uganda, itafaidika na ujenzi wa bomba la mafuta ambapo mradi huo utazalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira za muda mfupi 20,000.
Ujenzi wa bomba hilo kwa upande wa Tanzania ulizinduliwa na Rais John Magufuli na kwa Uganda, Yoel Museveni mwezi Agosti mwaka huu. Marais hao wamekutana tena mwezi huu Novemba katika mpaka wa Tanzania na Uganda Mutukula ili kuzindua mradi huo na kuziwezesha nchi hizo kuongeza Pato la Taifa kutokana na shughuli ya uchimbaji na usafirishaji wa mafuta ghafi.
Katika uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema ataendelea kushirikiana na Uganda kujenga mradi huo kwa upande wa Tanzania ili ukamilike kwa wakati na atahakikisha unalindwa wakati wote ili kuanza kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
“Ilibidi tuende bungeni tukafanye mabadiliko ya sheria za rasilimali asilia na Bunge letu liliupitisha mradi huu. Huu mradi utakuwa muarobaini wa uchumi wa Afrika ya Mashariki na Dunia”, amesema Rais Magufuli
Amewataka wataalamu wa Uganda na Tanzania kushirikiana na wawekezaji wanaojenga mradi huo kufanya kazi kwa bidii ili mradi huo ukamilike mapema.
“Wawekezaji mmekuja kwa wakati muhimu tuendelee mbele. Wataalamu wa Tanzania na Uganda mkae pamoja na wawekezaji mradi huo ukamilike kabla ya 2020”, amesema Rais Magufuli.
Ramani ya Bomba la mafuta litakalojengwa toka Tanga hadi Kabaale nchini Uganda
Kwa upande wake, rais Yoel Museveni amesema ataendelea kushirikiana na Tanzania ili kufanikisha mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, ambao utawezesha taifa la Uganda kuwa miongoni mwa wazalishaji wa mafuta duniani.
Bomba hilo linajengwa kwa hisani ya Kampuni ya Total na kwa upande wa Tanzania bomba hilo litapita katika Wilaya 26 hadi kufika katika mpaka wa Uganda ambako nchi hiyo itawajibika kujenga bomba hilo mpaka katika mji wa Kabaale.
Ikumbukwe kuwa Uganda ilichukua uamuzi huo wa kujenga bomba la mafuta kupitia katika Bandari ya Tanga baada ya kufanya tathmini ya kina juu ya gharama na umbali ikilinganishwa na nchi ya Kenya ambayo ina bandari ya Lamu. Awali iliingia makubaliano na nchi ya Kenya ili bomba hilo lipite katika nchi hiyo hadi katika bandari ya Lamu iliyopo Pwani ya Kenya.
Lakini suala la usalama lilikwamisha Kenya kufaidika na mradi huo kwasababu Bandari ya Lamu haikuwa salama kutokana na Mashambulizi ya wanamgambo wa Al-shabab ambao wamekuwa wakiendesha mashambulizi nchini Kenya na maeneo ya Somalia.
Pia Kenya inatajwa kuwa na urasimu katika upatikanaji wa ardhi ambapo ingechukua miaka miwili kuwalipa wananchi fidia ambako bomba linapita lakini kwa Tanzania mchakato huo ulikuwa rahisi kwasababu ardhi yote ni mali ya serikali.
Licha ya mradi huo kuitenga Kenya lakini nchi zote za Afrika Mashariki zinaendelea kujenga mradi mkubwa wa reli ya kisasa (standard Gauge) ambao utaunganisha nchi hizo na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na uwekezaji wa rasilimali