TANZANIA imeteuliwa kuwa moja ya nchi tano katika kamati ya Umoja wa Afrika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Ivory Coast kati ya Rais anayemaliza muda wake Bwana Laurent Gbagbo na Bwana Alassane Outtara, taarifa ya Ikulu imeeleza.Nchi zingine kaatika kamati hiyo ni Chad, Mauritania, Nigeria na Afrika ya Kusini, nchi hizi zitaungana na nchi ya Burkina Faso ambayo tayari inashughulikia mgogoro huo.
Kamati hiyo imefanya mkutano wake wa kwanza jana jioni tarehe 31, Januari 2011 mjini Addis Ababa ambapo imekubaliwa kuwa kila nchi itachagua mwakilishi wake katika kamati ndogo ya wataalamu ifikapo tarehe 3 Februari ambao watakwenda nchini Ivory Coast kuangalia na kutathmini hali ilivyo.
Baada ya hapo Kamati ya wataalamu watatakiwa kutoa taarifa na ushauri kwa viongozi ambao hatimaye watakwenda Ivory Coast na kukutana na viongozi hao wawili wanaogombea madaraka.
Wakati huo huo Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa Bwana Adrew Mitchell.
Katika mazungumzo yao Bwana Mitchell amemhakikishia Rais Kikwete kuwa Uingereza itaendelea kuisaidia Tanzania katika bajeti yake na pia katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kwa pamoja kufanya kazi itakayoonyesha mafanikio na majibu yatakayoleta manufaa kwa watu wake.
Rais Kikwete amemweleza Waziri Mitchell dhamira yake ya kuongeza jitihada katika kukuza elimu nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi karibu na makazi yao.
Waziri Mitchell amesema Uingereza itamsaidia na kushirikiana na Rais Kikwete katika kutimiza azma yake hiyo ambapo wataongeza msaada zaidi katika sekta hizo muhimu za elimu na afya nchini Tanzania.
Rais Kikwete anatarajiwa Kurejea nyumbani leo mchana.