Tanzania yaijia juu EU, Marekani mauaji ya raia wasio na hatia nchini

Jamii Africa
Serikali imesema Meli mbili zilizokuwa na bendera ya Tanzania wakati zikielekea Korea Kaskazini zilifutiwa usajili miaka 2 iliyopita - Taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Augustine Mahiga mbele ya Mabalozi wa nchi 5 ambazo ni Wajumbe wakudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - Januari mwaka huu Serikali ilizifutia usajili Meli 450 zilizokuwa zinapeperusha bendera ya Tanzania baada ya kukamatwa kwa Meli iliyobeba shehena ya silaha nchini Ugiriki na #DawaZaKulevya iliyokamatwa nchini Italia - Wiki iliyopita Marekani ilitishia kuyawekea vikwazo Mataifa yatakayokiuka vikwazo vya UN dhidi ya Korea Kaskazini

Serikali ya Tanzania imekanusha tuhuma kwamba inaminya demokrasia nchini na kusema kuwa imesikitishwa na matamko yaliotolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na kuungwa mkono na baadhi ya balozi wa nchi za Magharibi wanaofanya kazi Tanzania.

Taarifa ya serikalli ya Tanzania imefuatia matamko yaliyotolewa na nchi za magharibi wiki za hivi karibuni yakielezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya kushambuliwa na kuuawa kwa wananchi wasio na hatia ambayo wameeleza yanatishia utawala wa kisheria na maadili ya kidemokrasia nchini Tanzania.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imeeleza kuwa suala la utawala wa sheria na demokrasia katika tamko hilo la mabalozi linaonyesha sintofahamu iliyoko juu ya usalama na changamoto za kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliwa nazo kwa kipindi cha miezi 18 na kwamba matamko hayo yamekuwa sio tafsiri sahihi ya hali ya kisiasa na usalama iliyopo Tanzania.

“Ni kawaida kwa wanadiplomasia wa kigeni kufuatilia na kuripoti hali ya kisiasa na usalama inayoendelea katika nchi walizotumwa. Lakini tunashangazwa na ukimya uliowazi katika kipindi cha nyuma wa mabalozi hawa juu ya vitisho vya uvunjifu wa amani uliokuwa haujawahi kutokea na changamoto nyingine ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliana nazo katika maeneo matatu ya Kibiti-Mkuranga –Rufiji yanayopakana,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pamoja na kuwepo taarifa za matukio haya ya uvunjifu wa amani yalitolewa na vyombo vya habari nchini, hakukuwa hata na tamko lililolaani vitendo hivyo kutoka kwa mabalozi hao na kuonekana kuwa EU ina maslahi binafsi katika matukio ynayotokea nchini. 

 

Tamko la Umoja wa Ulaya na Marekani

 Mnamo Februari 23 mwaka huu, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) iliitaka serikali ya Tanzania kudumisha amani, utulivu na misingi ya demokrasia kwa kuhakikisha inawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika na utekaji na mauaji ya raia wasio na hatia.

Tamko hilo lilitolewa na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na Mabalozi wa Norwei, Kanada na Uswisi ambapo wameshtushwa na matukio ya hivi karibuni ya raia na viongozi wa kisiasa kutekwa, kuteswa na kuuawa na watu wanaodaiwa ‘wasiojulikana’.

"Tunashuhudia kwa wasiwasi muendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya kidemokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru”, ilieleza taarifa ya EU.

Wito huo wa EU ulikuja siku chache baada ya kifo cha mwanafunzi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati wa maandamano yanayodhaniwa yaliwakuwa ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) siku ya ijumaa ya Februari 15 mwaka huu.

Mabalozi hawa walimwomba rais John Magufuli kuanzisha uchunguzi wa matukio yote ya kushambuliwa na kuuawa kwa raia na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria mara moja.

"Tumesikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi mwisho wa juma lililopita Akwilina Akwilini Bafta, anayeombolezwa nchi nzima. Tunakaribisha wito wa Rais Magufuli wa uchunguzi wa haraka. Vilevile, tunatoa wito wa uchunguzi wa kina katika vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu.

"Tuna wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni, kama vile: jaribio lililohatarisha maisha ya Mbunge Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa Habari Azory Gwanda; pamoja na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa serikali, wawakilishi wa vyombo vya usalama na wananchi yaliyotokea Mkoa wa Pwani ndani ya miaka miwili iliyopita”. walisema Mabalozi hao katika taarifa yao.

 Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania siku za hivi karibuni ulitoa tamko la kulaani matukio yanayoendelea nchini na kueleza kuwa, ‘’Tunatoa wito kwa vyama vyote kulinda amani na usalama wa mchakato wa kidemokrasia, taifa na wa watu wa Tanzania’’,

 ‘’Tunaungana na Watanzania katika kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wenye uwazi ili kuwawajibisha wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya kikatili kwa mujibu wa sheria za Tanzania’’.

Kabla ya kifo cha Akwilina na Luena, kumekuwa na mfufululizo wa matukio ya maiti za watu kukutwa kwenye fukwe za Coco  jijini Dar es Salaam zikiwa zimefungwa kwenye viroba ikiwemo ya aliyewakuwa Katibu wa CHADEMA kata ya Hananasif, Daniely John.

Lakini bado jamii ya kitanzania inashuhudia idadi ya raia wasio na hatia na waandishi wa habari kupotea katika mazingira yasiyoelezeka. Mpaka sasa waliopotea kusikojulikana ni mwanachama wa CHADEMA, Ben Saanane, Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na Emmanuel Kibiki (Raia Mwema).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *