TUHUMA nzito za ufisadi katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, zimeanza kuingia katika hali ya hatari zaidi, ambapo waandishi wa habari watatu akiwemo mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, FikraPevu na Sayari mkoani Mwanza, Sitta Tumma inadaiwa wameanza kuundiwa njama chafu za kutaka kuuawa.
Mbali na njama hizo za kutaka kuuawa, waandishi hao inadaiwa wameanza pia kuandaliwa njama za kukamatishwa rushwa kwa nguvu pamoja na kubambikizwa kesi mbaya, ili kuwakomesha zaidi.
Hatua hiyo mbaya na inayokiuka kabisa sheria za nchi, haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari, imeelezwa kuanza kuandaliwa mwishoni mwa mwezi uliopita na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni vigogo wa halmashauri hiyo.
Majina ya vigogo wanaodaiwa kuanza kupanga njama hizo chafu tunayo, lakini kwa sasa tunayahifadhi.
Inadaiwa kwamba, chanzo cha waandishi hao kuanza kuandaliwa njama hizo za kutaka kuuawa, kubambikizwa kesi mbaya katika maisha yao pamoja na kukamatishwa rushwa kwa nguvu, inatokana na msimamo wao wa kuandika habari za uchunguzi na kufichua tuhuma za ufisadi wa fedha za miradi mbali mbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Mbali na mwandishi huyo wa FikraPevu mkoani Mwanza, Sitta Tumma kuanza kuundiwa njama za kutaka kuuawa, waandishi wengine wanaodaiwa kuundiwa njama hizo chafu ni pamoja na mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoani humo, Fredrick Katulanda pamoja na Peter Katulanda anayeandikia magazeti ya Uhuru na Mzalendo mkoani Mwanza.
“Februari 28 mwaka huu, nilipata taarifa za siri kutoka kwa mtu mmoja ambaye aliniambia kuwa tumeanza kuandaliwa njama za kutaka kuuawa. Mipango mingine inayoandaliwa ni kubambikizwa kesi mbaya au kukamatishwa rushwa kwa nguvu.
“Niliambiwa kuna watu ambao wanasadikiwa kuwa ni vigogo wa halmashauri ya Misungwi wamekutana Februari 28 mwaka huu na kupanga njama hizo za kutaka kutudhuru mimi na waandishi wenzangu wawili. Lakini tayari tumesharipoti kwenye vyombo vya dola”, alisema Sitta Tumma.
Januari 20 mwaka huu, mwandishi Sitta Tumma kutoka Mwanza aliripoti habari moja ya uchunguzi juu ya jumla ya sh. milioni 335,518,939, ikiwa ni fedha za Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), kudaiwa kutojulikana zilipo, ambapo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Xavier Tilweselekwa alipoulizwa na mwandishi wetu alikanusha kuwepo kwa ubadhilifu huo, akisema: “Huo ni uzushi tu wa watu”.
Mbali na habari hiyo, Februari 26 mwaka huu mwandishi wetu huyo aliripoti habari nyingine pia juu ya tuhuma hizo nzito za ufisadi, zinazoikabili halmashauri ya wilaya hiyo, ambapo katika habari hiyo alimkariri Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Welle Ndikilo.
RC Ndikilo ambaye alifanya ziara ya kikazi wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Februari 25 mwaka huu, alikutana na watumishi wa halmashauri hiyo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Misungwi, ambapo alikuwa akizungumza kwa kutumia ripoti za wakaguzi ikiwemo ya CAG zinazobainisha ukweli wa kuwepo ufisadi katika halmashauri hiyo inayoongozwa na madiwani wa CCM.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Ofisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Mwanza, Meja Mutash, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Doroth Mwanyika, Mkuu wa wilaya hiyo, Mariam Seif Lugaila, OCD wa Misungwi pamoja na maofisa wengine wa Serikali, RC Ndikilo aliahidi kumshauri Waziri Mkuu, Mizngo Pinda aivunje halmashauri hiyo ya Misungwi, ili ianze upya.
Waandishi wengine, Peter Katulanda pamoja na Fredrick Katulanda nao wameanza kuundiwa njama hizo za kuuawa, kubambikizwa kesi mbaya na kukamatishwa rushwa kwa nguvu kwa madai yale yale kwamba wamekuwa wakiandika na kufichua mambo ya ufisadi unaoikabili halmashauri hiyo.
Kufuatia hali hiyo, tayari kwa ujumla wao waandishi hao wameshatoa taarifa hizo za kuanza kuundiwa njama chafu za kutaka kuuawa dhidi yao kwa vyombo vya dola mkoani Mwanza.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza