Ugonjwa wa kifafa washambulia kijiji kizima

Albano Midelo

Wananchi wa Kijiji cha Mtua ambacho kinapakana na pori la wanyamapori la Liparamba wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wapo katika hatari baada ya ugonjwa wa kifafa kushambulia karibu kijiji kizima.

Uchunguzi umebaini kuwa  katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 1,600 watu 200 wanadaiwa wanaugua kifafa ambapo kila nyumba kuna mgonjwa mmoja wa kifafa na baadhi ya nyumba zina wagonjwa wawili hadi watatu hali ambayo inasababisha wananchi wa kijiji hicho kuhitaji msaada mkubwa kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa lengo la kukinusuri kijiji hicho.

Kijiji cha Mtua kipo katika kata ya Mpepai ambapo  inadaiwa ugonjwa huo ulianza  kuwashambulia watu wachache mwaka  1996 ambapo hivi sasa umeenea katika kiwango cha kutisha ukilinganisha na vijiji vingine vya Lipilipili,Kihungu na Changarawe, hivyo  kukifanya kijiji hicho kuongoza katika wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Samweli Matembo ni  mwenyekiti wa kijiji cha Mtua anasema tatizo la kifafa ni kubwa katika kijiji hicho ambapo idadi ya wagonjwa inazidi kuongezeka siku hadi siku na kusisitiza kuwa wananchi wengi wanaamini ugonjwa huo ni wa kurithi na kwamba inadaiwa ugonjwa huo unasababishwa na ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo haijaiva vizuri,imani za kishirikina,unywaji wa pombe kupita kiasi na kuoa au kuolewa katika ukoo ambao umeaathirika.

“Tatizo hilo lilianza polepole  mwaka 1996 na linazidi kuongezeka kwa kasi ambapo hivi sasa wananchi wanashindwa kufanya kazi zao za kiuchumi na kubakia masikini kutokana na  muda mwingi kutumia nyumbani kuwaangalia wagonjwa wa kifafa ambao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu hasa kwenye moto na maji,hivi sasa wagonjwa wanatumia dawa za hospitali lakini bado tatizo ni kubwa,tunawaomba watalamu wajitahidi kufika hapa ili watusaidie’’, anasema mwenyekiti mstaafu wa kijiji John Nchimbi.

Kondrad Nyika mzee wa miaka 70 anasema katika nyumba yake wapo wagonjwa wa kifafa watatu akiwemo mke wake ambaye anasema kifafa kilimuanza wakati anapika ugali ambaye hivi sasa anatumina dawa za hospitali na hali yake inaendelea vizuri na kwamba  watoto wake wawili bado wanaendelea kuugua kifafa bila kupata nafuu licha ya kutumia dawa za hospitali.

wanakijijiBaadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtua wilayani Mbinga wakimwelezea mwandishi wa habari hizi kuhusu tatizo la ugonjwa wa kifafa lilivyoathiri kijiji kizima kutokana na kila nyumba kuwa na mgonjwa wa kifafa

John Nchimbi anasema idadi kubwa ya wanafunzi wa shule ya msingi Mtua  wanadaiwa wanaugua ugonjwa wa kifafa hali ambayo inasababisha wengi kuwa watoro na kuacha shule hata wale ambao wanasoma wameathirika na kushinda kufuatilia masomo kutokana na ugonjwa huo kuathiri ubongo.

Denis Nchimbi

Denis Nchimbi mwanafunzi anayeugua kifafa aliungua moto baada ya ugonjwa kumuanza akiwa jirani na moto na wazazi wake walikuwa shambani

Lauriano Komba mkazi wa kijiji cha Mtua anasema wagonjwa wa kifafa 33 hadi sasa wanadaiwa wameungua na moto  baada ya kuanguka kifafa wakiwa peke yao na kusisitiza kuwa kifafa kilichopo katika kijiji hicho ni cha ajabu  kwa kuwa katika vijiji vingine idadi ya wagonjwa hawazidi wane ambapo katika kijiji hicho karibu kila nyumba kuna mgonjwa.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Maria Komba, Juliana Hyera na  Flora Nchimbi walisema wanashinda kwenda shambani kutokana na muda mwingi kuutumia kuwaangalia watoto wao wanaugua kifafa kuhofia kuangukia kwenye moto au maji endapo ugonjwa huo unawaanza bila kuwa na mwangalizi.

Takwimu za ugonjwa wa kifafa katika mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa  katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2009 kulikuwa na wagonjwa 1072 kati yao wanaume 639 na wanawake 433 ambapo wilaya ya Mbinga  inaongoza kwa  wagonjwa 337,Songea manispaa 309,Songea  vijijini 217,Namtumbo 62 na Tunduru 147 takwimu hizi ni wale walioripoti kwenye vituo vya afya.

Baadhi ya wanawake katika kijiji cha Mtua baada ya kutoa maoni yao kuhusu tatizo ka kifafa linavyowaandama

Mratibu wa magonjwa ya akili na kifafa mkoa wa Ruvuma Talumba Gullum anasema wagonjwa wengi wa kifafa hawajitokezi kwenye vituo vya afya na hasa waliopo vijijini ambao kutokana na kukosa elimu sahihi dhidi ya ugonjwa huo wanaamini  ugonjwa huo ni ushirikina na wa aibu hali inayowafanya wagonjwa kuwaficha majumbani na tatizo kuongezeka.

Kulingana na watalaamu wa afya kifafa (Epilepsy) kinatokea kunapokuwa na mapungufu katika seli za ubongo na kwamba kunapokuwa na hitilafu katika huu mfumo  kifafa kinaweza kutokea ambacho dalili zake ni kuona maluwe luwe (aura), kiasha kupoteza fahamu, kuanguka na kutupa miguu na/au mikono, kukaza mdomo, kutoa povu na wakati mwingine na kutoa haja ndogo au kubwa.

Hata hivyo watalamu wa ugonjwa huo wanasisitiza kuwa kifafa sio ugonjwa wa kuambukiza, mara nyingi unakuwa kwenye familia kwa kurithi toka kwa mzazi au wazazi, na kwamba wakati mwingine inaweza tokea baada ya kuumia ubongo kutokana na ajali, kiharusi (stroke), kuumia wakati wa kuzaliwa (birth injuries) na kwamba  Kifafa cha aina hiyo  ni tofauti na ‘dege dege’ kwa watoto au kifafa cha mimba (Eclampsia).

Kulingana na wataalamu kifafa hakitibiki na mgonjwa kupona  kabisa bali kuna dawa za kupunguza au kuzuia kifafa kutokea mara kwa mara na kwamba dawa hizo zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali ambapo  mgonjwa atakunywa kwa maisha yake yote ambapo dozi inategemea na hali ya mgonjwa anapoonwa mara kwa mara kwenye kliniki zao maalum.

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *