Umoja wa Ulaya waigomea Tanzania, Botswana biashara ya pembe za ndovu

Jamii Africa

Nchi 32 za Afrika ikiwemo Tanzania zimeutaka Umoja wa Ulaya (EU)  kusitisha biashara ya pembe za ndovu ili kuokoa tembo waliosalia barani humo.

Makubaliano hayo yalifikiwa nchini Botswana hivi karibuni katika kongamano la Ujangili wa Tembo na Biashara  Haramu ya Wanyamapori  ambalo lilijikita kuimarisha sheria na ulinzi wa wanyama hao ambao wako katika hatari ya kutoweka duniani.

Kongamano hilo liliongozwa na marais, Yoweri Museveni wa Uganda, Ali Bongo wa Gabon na Ian Khama wa Botswana ambapo waliandika ombi la pamoja na wawakilishi wa nchi nyingine 29 wakiitaka EU kufunga soko lake la pembe za ndovu.

Kulingana na kundi la watetezi la Avaaz,  Umoja wa Ulaya ni msafirishaji mkubwa wa pembe za ndovu duniani ambaye anafuata sheria za kimataifa lakini wana wasiwasi kuwa biashara hiyo ikiachwa iendelee itachochea ujangili katika nchi za Afrika.

Kuna mahitaji makubwa ya pembe za ndovu barani Asia hasa China lakini ili kuwalinda wanyama hao mwaka jana nchi hiyo ilipiga marufuku  biashara zote za zinazohusiana na pembe za ndovu.

“Tunachoona Ulaya imekuwa ni kituo cha kupokea na kusafirisha pembe za ndovu  kinyume na sheria”, alisema Mkurugenzi wa kampeni wa Avaaz, Bert Wander. “Ni muhimu hii biashara ikafungwa ikiwa tunataka kuwalinda wanyamapori”.

                               Askari Wanyama pori akisimamia uchomaji wa pembe za ndovu katika Hifadhi ya Taifa ya Nairobi Machi 3, 2015

Inaelezwa kuwa Umoja wa Ulaya umekataa kuachana  na biashara hiyo kwa kile kinachodaiwa kuwa sio viongozi wote wa Afrika wanataka biashara hiyo ikomeshwe.

 Naye Waziri wa Mazingira wa Botswana, Tshekedi Khama alisema “Sababu ya EU kutakiwa kufunga biashara hiyo ni kwasababu China imefunga”.

Kulingana na Avaaz, Uingereza ndio msafirishaji mkubwa wa pembe za ndovu miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya. “Siwezi kusema zaidi kuhusu Uingereza…lakini fanya jambo zuri funga biashara ya pembe za ndovu”, alisema Khama.

 

Mauaji ya Tembo

 Utafiti uliofanywa mwaka 2016 unakadiria kuwa mpaka sasa kuna tembo 352,000 ambapo idadi hiyo imepungua kutoka milioni 1.3 mwaka 1979. Takwimu za sensa ya Tembo zinaeleza kuwa idadi ya Tembo barani Afrika imepungua kwa 30% kati ya mwaka 2007 na 2014. Tanzania ilikumbwa na anguko kubwa la idadi ya Tembo ambapo inakadiriwa kuwa wamepungua kwa 80%.

Sheria za kimataifa zinaruhusu nchi kusafirisha pembe za ndovu ikiwa zimethibitishwa kuwa zilifanyiwa kazi au kutengenezwa kabla ya 1976.

 Bidhaa za zamani za pembe za ndovu zilizotengenezwa kabla ya 1947 kama mipira (billard balls), vifaa vya muziki na chesi zinakubalika kisheria na hazihitaji cheti kulingana na muda vilipotengenezwa. Lakini wanaharakati wanasema dhana hiyo inatengeneza mpenyo wa mauaji ya tembo ili kuingia kwenye soko halali.

 Mwaka 2014, Tanzania ilianzisha Operesheni Tokomeza Ujangili katika mapori ya akiba nchini ili kupambana wanavamizi ambao walikuwa wakiua wanyama pori wakiwemo tembo ili kujipatia pembe  ambazo zinahitajika sana katika bara la Asia hasa nchini China.

Operesheni Tokomeza iliongozwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) iliyolenga kukomesha ujangili, lakini kukaibuka malalamiko kuwa baadhi ya watuhumiwa waliteswa na hata kupoteza maisha. Hatua hiyo ilimfanya Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, asimamishe operesheni hiyo ingawa aliahidi awamu ya pili ingerejeshwa.

Operesheni hiyo ilisaidia kupunguza vitendo vya ujangili, hasa wa tembo na faru ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka.

Mwaka 2016, majangili walidungua helikopta kwa risasi na kumuua rubani Rodgers Gower (37), raia wa Uingereza. Tukio hilo lilitokea katika Pori la Akiba la Makao, Meatu mkoani Simiyu.

Hata hivyo, mwaka uliofuata wa 2017 Wayne Lotter, Mkurugenzi wa taasisi ya kuhifadhi wanyamapori ambaye amekuwa akipokea vitisho mbalimbali aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Mhifadhi huyo wa wanyama pori aliuawa eneo la Masaki jijini Dar es Salaam wakati akitoka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere akiwa kwenye gari kuelekea kwenye makazi yake. Watu wawili, mmoja akiwa na silaha alifungua kioo cha gari na kumpiga kwa risasi Lotter ambapo alipoteza maisha.

Lotter alikuwa Mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la PAMS, linalotoa huduma za uhifadhi na msaada wa kupambana na ujangili kwa jamii na serikali za Afrika. Tangu shirika hilo lianzishwe nchini Tanzania mwaka 2009 alikuwa ameshapokea vitisho vingi vya kuuawa kuhusiana na kazi yake. Baadhi ya watu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kudaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Shirika la PAMS lilifadhili na kukisaidia kikosi kazi (NTSCIU) kilichoundwa kupambana na ujangili ambapo katika harakati hizo walifanikiwa kumkamata mfanyabiashara mkubwa wa pembe za ndovu, Yang Feng Glan ambaye anajulikana kama “Queen of Ivory”  na majangili wengine ambao walikuwa wakiendesha shughuli zao kwenye mbuga mbalimbali nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *