Uongozi Tanga wakwamisha kupatikana kwa mashine ya tiba Bombo hospitali

Jamii Africa

UONGOZI wa Mkoa wa Tanga unakwamisha kupatikana kwa vifaa vya tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kutokana na ukiritimba.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kuwa kukosekana kwa baadhi ya mashine za uchunguzi wa afya kunatokana na “uzembe” wa baadhi ya watendaji wa mkoa huo kushindwa kuamua masuala kadhaa.

FikraPevu imebaini kuwa hospitali hiyo haina mashine inayofanya kazi ya MRI CT-Scan.

Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya watu binafsi, taasisi na mashirika kadhaa yamekuwa na utayari wa kusaidia kupatikana kwa mashine hiyo pamoja na zingine, lakini wanakatishwa tamaa na uongozi wa mkoa.

Mmoja wa maofisa wa Jumuia ya Madhehebu ya Bohora ameithibitishia FikraPevu kuwa waliahidi kutoa mashine hiyo, lakini serikali ya mkoa imeshindwa kuwahakikishia kupata mtaalamu wa kuitumia na jengo la kuiweka.

“Mimi sio msemaji, katibu wetu yupo Nairobi (Kenya), lakini ninachokuthibitishia ni kweli tuliahidi, lakini serikali imeshindwa kuleta mtaalamu na kutupatia eneo ili mashine za afya tunazotaka kusaidia zifungwe, hatuwezi kupeleka vifaa mahali na vikaharibika kwa haraka, ni bei kubwa,” aliiambia  FikraPevu.

Hospitali ya Rufaa ya Bombo inahudumia wagonjwa wanaotoka hospitali za zilaya za Pangani, Kilindi, Handeni, Korogwe, Mkinga, Muhenza na Lushoto.

Licha ya upungufu wa vifaa hivyo vya tiba, hospitali hiyo inadaiwa kushindwa kupokea msaada wa mashine ya MRI CT-scan iliyotolewa na dhehebu la Kiislamu la Jumuia ya Mabohora mkoani Tanga kwa miaka miwili sasa kwa kisingizio cha kukosa mtaalamu na eneo kwa ajili ya kujenga eneo kuhifadhia mashine hiyo.

Daktari mmoja ambaye aliongea na FikraPevu na kuomba asitajwe jina amesema, mashine hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaosumbuliwa kwa magonjwa mbalimbali.

Mashine hiyo ni ya kisasa katika kuchunguza na kubaini matatizo ya afya kwenye mishipa, mifupa na matatizo mengine kwenye ubongo.

“Hiki ni kifaa muhimu, unapokuwa na MRI CT- Scan, huwezi kufanya makosa katika kumpa mgonjwa maelekezo au kumtibu, ni vifaa vya kisasa zaidi kuliko hata X-ray,” alisema.

Takwimu za ajali zilizotolewa mwaka 2016, mkoani Tanga zinaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba, 2016, jumla ya watu 80 walifariki katika ajali za barabarani na kusababisha majeruhi 102, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi.

“Majeruhi wengi wangeweza kusaidiwa, wengine wangetibiwa vizuri, wasipate ulemavu wa kudumu, lakini kuna upungufu wa dawa, na vifaa muhimu kama mashine za kuchunguza afya,” anaongeza.

Matatizo yanayosababishwa na uhaba wa vifaa tiba na dawa ni makubwa, kwani sio tu yanatishia uhakika wa huduma kwa mgonjwa anapokuwa katika hospitali ya rufaa, lakini pia yanapunguza ari ya kufanya kazi kwa watoa huduma.

Hali hii inawathiri wananchi wengi hasa wale wasio katika mfumo wa bima za afya na wale wenye bima zenye wigo mdogo wa hospitali za kupata tiba.

FikraPevu imemuona mama aliyejitambulisha kwa majina – Mwanamkuu Rajab, aliyetoka Bombo akilia baada ya mgonjwa wake, aliyewasili hapo kwa ajili ya kujifungua, kukosa baadhi ya vifaa na dawa za maandalizi ya kujifungua.

Taarifa zinaeleza kuwa kilio cha mama huyo kilizidi baada ya kupata taarifa kuwa mgonjwa wake amejifungua, lakini mtoto akiwa amefariki.

Mama huyo alikosa hata pesa ya kununua pamba kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa wake. Pamba iliyokuwa ikihitajika inauzwa Sh. 5,500, nje ya lango la hospitali hiyo.

Mwingine aliyekumbana na kadhia ya kutopata dawa hospitali hiyo ni Mbwambo Ally, ambaye alikuwa anatafuta dawa kwa ajili ya ndugu yake kuongezewa damu, dawa hiyo kwa mujibu wa maelekezo aliyopewa kwenye duka la dawa inauzwa Sh. 9,500.

Mbwambo kama ilivyo kwa wagonjwa wengi, hakuwa na pesa ya kununua dawa hiyo.

Uongozi wa hospitali ya Bombo, haukupatikana kuzungumzia masuala hayo baada ya mwandishi kuelekezwa kwanza aende ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Zena Said kwa ajili ya kupewa kibali ili masuala hayo yaweze kupatiwa ufafanuzi na uongozi wa hospitali.

Aidha, mwandishi alishindwa kupata ridhaa hiyo baada ya kuwambiwa na wasaidizi wake kuwa Zena alikuwa nje ya ofisi kikazi na wao hawakuwa na mamlaka yakutoa kibali cha mganga mkuu wa Bombo kuhojiwa hadi pale mwandishi atakapoleka maswali kwa maandishi  yasomwe ili aruhusiwe au la.

Uongozi wa mkoa wa Tanga ulipiga marufuku kwa waandishi kuingia maeneo ya hospitali kwa lengo la kupata taarifa, bila ruhusa ya maandishi kutoka kwa maofisa tawala wa wilaya ama mkoa.

Hata hivyo, kwa kutambua hilo, mwandishi wa habari hii aliamua kujifanya mgonjwa ndipo akafanikiwa kuingia Hospitali ya Bombo kubaini matatizo kadhaa ndani ya hospitali.

Pamoja na makatazo hayo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, mara kadhaa amekuwa akisisitiza kuwa waandishi wa habari hawatakiwi kuzuiwa kuigia ofisi za umma kwa kupata habari.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *