Ushirikina unavyopelekea Mauaji ya wanawake Mara

Shomari Binda

Mauaji ya wanawake mkoani Mara hususani wilayani Butiama hufanywa kwa sababu za kijinga na zisizo na ukweli za haja ya kupata samaki wengi kwa kutumia viungo vya mwanamke ambavyo hudaiwa kuvuta samaki.

Wauaji hawa wengi wao ni wale wanaojishughulisha na uvuvi wakiwa na imani wanapomuua Mwanamke  na kuchukua baadhi ya vitu kwenye mwili wake kama kinembe, nywele za ukeni, ili wapate samaki wengi wakienda kuvua.

Imani hizo zimefanya wanawake kuishi kwa wasiwasi na kuwafanya kushindwa kwenda kwenye shughuli zao za kuwaongezea kipato zikiwemo shughuli za kilimo.

Licha ya jitihada za Serikali na viongozi wa dini ili kukomesha mauaji hayo, kwa mujibu wa taarifa za kipolisi katika kipindi cha miezi 3 tayari Wanawake Zaidi ya 15 wameuawa.

Wakati mwandishi wa makala haya anafika kijiji cha Kigera Etuma, Tarafa ya Kusenyi wilayani Butiama ndio kwanza taarifa za mauaji ya Catherine Mandela(21) zinatolewa. Taarifa za awali zilioonesha kwamba mwanamke huyo kauawa kwa imani za kishirikina.

“Huyu ni Mwanamke wa pili katika kipindi cha mwezi mmoja kuuawa katika eneo letu katika mazingira ambayo naweza kusema ni imani za kishirikina na uhitaji wa utajiri wa haraka kwa wanadamu usiomuogopa Mungu,”anasema mzee Maiga Maingu wa Kijiji cha Kigera Etuma.

Anasema imani za kishirikina ndio chanzo kikubwa cha mauaji hayo huku wanaotajwa kutekeleza mauaji hayo ni wale wanaojishughulisha na uvuvi kwenye kambi za uvuvi wakiamini Wanawake wanamvuto wa kuvuta samaki kwenye mitego.

Maingu ambaye ni mvuvi mstaafu anasema hataki kuamini imani hiyo ya kutumia baadhi ya viungo vya Mwanamke kama njia ya kufanya upatikanaji wa samaki wengi kwenye shughuli za uvuvi.

Anasema kwa sasa imani hiyo imeshika kasi na Wanawake wengi wamekuwa wakiuawa kutokana na Imani hiyo nakuomba jitihada mbalimbali zifanywe ili kuwaweka wanadamu kwenye imani safi na kuachana na ukatili wa kuua wanawake kwa imani potofu.

Mzee Masatu Mfungo wa Kijiji cha Esiri Kata ya Kigera Etuma anasema kutokana na kuibuka kwa mauaji hayo ya Wanawake kumewafanya Wanawake kwenye Kijiji hicho kuogopa kwenda kwenye shughuli za kilimo.

Anasema katika kipindi cha miaka ya nyuma matukio kama hayo yalikuwa hayapo na kila mmoja alifanya shughuli zake kwa kujiamini lakini leo imekuwa tofauti huku hofu ikitawala miongoni mwa jamii.

“Katika kipindi cha nyuma tumekuwa tukifanya shughuli za uvuvi na tumekuwa tukipata samaki kutokana na shughuli hiyo bila kuweka Imani za kishirikina lakini leo imekuwa tofauti.

“Kuna masuala ambayo wavuvi wa leo wanakosea na kupelekea mangamizo ya samaki na hivyo kukosekana kwa hiyo wanapoingiza Imani za kishirikina kwa kukosekana huko na kuwaua Wanawake nashindwa kuelewa tunaenda wapi.

“Leo hii tunasikia kunafanyika uvuvi haramu wa kutumia mabaruti ambayo yanafukuza na kuangamiza samaki ziwani kisha mtu anataka apate samaki wengi hii haiwezekani watu wanapaswa kupata elimu juu ya suala hili na sio kujiingiza kwenye Imani za kishirikina,”anaelezea mzee Mfungo.

Katika Kijiji cha Nyegina Kata ya Nyegina wilayani Butiama aliuawa Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mkaguru Magee akiwa shambani kwake na kisha kufukiwa kwenye shamba hilo .

Wakielezea kifo cha Mkaguru,wananchi hao wanadai marehemu alikuwa mtu shupavu licha ya umri wake wa miaka inayokadiliwa 60-70 alizimudu shughuli za kilimo na aliuawa akitekeleza shughuli zake za kilimo shambani kwake.

“Kwa kweli walimuua kinyama mama Mkaguru na tunavyosikia ni watu wanaosukumwa na imani za kishirikina hasa wanaofanya shughuli za uvuvi kwa kweli inauma sana tunaviomba vyombo vya dola vifuatilie suala hili.

“Hivi kweli jeshi la polisi na vyombo vingine vyaa dola vinashindwa kukomesha hali na kupelekea kuendelea kutokea kwa mauaji ya Wanawake bila hatia na watu kwa kutafuta maslahi yao?,anasema na kuuliza Bwimbo Mgaya wa Kijiji cha Nyegina.

Ukweli ni kwamba mauji ya kikatili kwa Wanawake wilayani Butiama yapo na jeshi la polisi limekuwa likitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kutokea kwa mauaji haya.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara  John Gabriel Tupa alipambana kuhakikisha mauaji dhidi ya Wanawake Butiama yanakomeshwa .Ilielezwa kuwa kabla ya Mkuu huyo wa mkoa kukutwa na umauti alikuwa ameagiza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ili kuzungumzia mauaji ya Wanawake yanayoendelea Butiama.

Ni imani kwamba Serikali ya mkoa wa Mara kupitia vyombo vyake vya usalama itamuenzi aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara John Tupa kwa kukomesha mauji dhidi ya Wanawake yanayotokana na imani za ushirikina.

Elimu muafaka kuhusu uvuvi na athari za uvuvi haramu zinatakiwa kutolewa ili watu wasikubaliane na maneno ya waganga wa kienyeji kuhusu utoaji kafara kwa ajili ya kupata samaki. Kuna imani potofu nyingi ambazo zinaweza kukomeshwa kwa wahusika kuwataja wanaowapa elimu ya mauaji kwa misingi ya kupata mali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *