Imeelezwa kuwa tabia ya kujipiga picha mwenyewe (selfie) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ni ugonjwa wa akili ujulikanao kitaalamu ‘Selfitis’ ambapo mgonjwa wa tatizo hili hugunduliwa kwa idadi ya picha alizopiga na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham Trent na Shule Kuu ya Utawala iliyopo nchini India ndio waliogundua ugonjwa huo wa ‘Selfitis’ baada ya taarifa kulipotiwa na vyombo vya habari mwaka 2014 ambazo zilitolewa na Chama Cha Marekani cha Tiba ya Akili kuwa kujipiga picha mara kwa mara ni moja ya dalili za kupata ugonjwa wa akili.
Watafiti hao walipoiona habari hiyo walifanya utafiti zaidi na kuthibitisha kuwa watu wengi wanaopenda kujipiga picha wana maradhi hayo. Walitumia njia ya kupima tabia ijulikanayo kama ‘Selfitis Behaviour Scale’ ambayo inaweza kupima dalili za ugonjwa huo kama upo kwa mtu.
Kipimo hicho cha tabia kilitokana na sampuli ya watu 400 ambapo waligawanywa kwenye makundi matatu ili kuangalia tabia zao za upigaji picha kwa kutumia simu za mkononi.
Washiriki wote walitoka nchi ya India ambako kuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na idadi kubwa ya watu wanaofariki kutokana na kujipiga picha ‘Selfie’ kwenye maeneo hatarishi kama majengo marefu, kwenye madaraja na mito.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye Jalida la International Journal of Mental Health and Addiction ambapo limebaini makundi 3 ya watu wenye dalili za ugonjwa wa akili wa ‘Selfitis’. Ugonjwa huo hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine kulingana idadi ya picha anazojipiga na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii. Makundi hayo ni:
•Kundi la 1- Hawa hujipiga picha mara tatu kwa siku lakini hawaziweki kwenye mitandao ya kijamii.
•Kundi la 2- Hawa hujipiga picha mara tatu kwa siku na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
•Kundi la 3- Hawa hawawezi kujizuia na hujipiga picha wakati wote na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii zaidi ya mara sita kwa siku.
Tabia ya kujipiga picha huanza taratibu kutoka hatua ya kwanza na mazoea yakizidi mtu hufika hatua ya tatu ambayo huathirika kisaikolojia na hujipiga picha kwa wingi na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kupata faraja kwa wanaomzunguka kwasababu anaamini hawezi tena kuishi bila kujipiga picha.
Wanafamilia wakijipiga picha ‘selfie’
Sababu zinazowasukuma watu kujipiga picha
Ziko sababu sita zinazowashawishi watu ambao wameathirika na ugonjwa wa akili wa selfitis ambapo hutafuta; kuongeza kujiamini, kukubalika na kusikilizwa, kuboresha msawazo wa mawazo, kutengeneza kumbukumbu ya eneo alilotembelea, kuongeza ukaribu na ushindani kwa watu wanamfuatilia kwenye mitandao ya kijamii.
Dk. Mark Griffiths, Mtaalamu wa tabia za binadamu Idara ya Saikolojia Chuo Kikuu cha Nottingham Trent, ambaye alishiriki katika utafiti huo anasema katika ripoti yake kuwa “Miaka michache iliyopita habari ilikuwa inasambaa kwenye vyombo vya habari ikitaka maradhi ya selfitis yaorodheshwe miongoni mwa magonjwa ya akili. Haikumaanisha kuwa selfitis haikuwepo. Tumethibitisha kuwa maradhi hayo yapo kwa kutumia kipimo cha tabia kubaini dalili za selfitis”.
Mtafiti mwingine, Dk. Jonarthanan Balakrishnan anasema; “Watu wenye maradhi hayo wanakosa ujasiri, wanajitahidi kuwa sehemu ya watu wanaowazunguka na wanaonyesha tabia za urahibu kama watu wengine. Ni matumaini kuwa tafiti nyingine zitafanyika ili kuelewa jinsi watu wanavyoingia kwenye hizo tabia na nini kifanyike kuwasaidia wale ambao wameathirika zaidi”
Hata hivyo, kuna maradhi mengine ya akili ambayo yanahusishwa na watu kuogopa kuwa karibu na simu ‘normophobia’. Wataalamu wa mawasiliano wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za kukuwa kwa teknolojia duniani.