Uwanja wa ndege Chato: Rais Magufuli anamuiga Mobutu aliyejenga uwanja wa Concorde kijijini kwake?

Daniel Mbega

SERIKALI ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko, na safari hii imeamua kuubadili mji wa Chato, nyumbani kwa Rais John Magufuli, kuwa ‘mji wa mfano’ kwa kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa, akimuiga mtawala wa zamani wa Zaire, Joseph-Desire Mobutu, maarufu Mobutu Sese Seko Nkuku Ngbendu Waza Banga.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba, uwanja huo utakuwa na eneo la kurukia ndege (runaway) wenye urefu wa meta 3,000 (sawa na kilometa 3) na upana wa meta 45, ukiwa na tofauti ndogo na uwanja wa ndege wa Gbadolite (urefu kilometa 3.2 na upana meta 60) kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliojengwa na Dikteta Mobutu Sese Seko mwaka 1972 ili kuruhusu midege mikubwa ya Concorde kutua na kuruka.

Na inaelezwa kwamba tayari shughuli za awali zimeanza kufanyika Chato tangu serikali ilipotangaza zabuni kwa ajili ya kusafisha eneo husika.

Uamuzi huo wa kujenga uwanja Chato umekuja wakati Serikali imeshatangaza kuhamishia makao yake makuu Dodoma kama ilivyokuwa imeamuliwa mwaka 1973, hatua ambayo ilianza kwa mbwembwe nyingi na kupongezwa na Watanzania kwamba walau serikali hii imethubutu kufanya kile ambacho kilikuwa ‘mtaji wa kisiasa’ wa baadhi ya watawala.

Hata hivyo, zoezi hilo limepoa kama siyo kuzimika licha ya kwamba tayari baadhi ya wizara zimekwishahamia huko, sababu kuwa ikiwa kukosekana kwa nyumba za watumishi.

Kulingana na wataalam wa masuala ya anga, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kupokea ndege zenye ukubwa wa Boeing 738, B733, B737 na Airbus 320 na A319 ambazo tangu Tanganyika ipate Uhuru mwaka 1961 hazijawahi kutuwa Iringa, Songea, Kigoma, Tabora, Musoma na Tanga, miji ambayo ndio mikubwa nchini Tanzania.

Katika kipindi ambacho uchumi wa taifa bado haujatengemaa, ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege katika mji wa Chato wenye wakazi 17,508 tu (kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012) unaonekana ni uamuzi usiozingatia maslahi mapana ya taifa.

Wakati Dikteta Mobutu alipoamua kujenga Uwanja wa Gbadolite katika Jimbo la Nord-Ubangi, mwendo wa saa 5 na dakika 16 kutoka mji huo hadi kijijini Lisala (umbali wa 332km) alikozaliwa Mobutu mwenyewe, Gbadolite kilikuwa kijiji kidogo ndani ya msitu mnene chenye watu 1,500 tu, ambapo kwa maslahi yake ya kutaka umaarufu, akaubadili kuwa mji mkubwa akijenga hekalu lake kubwa, hoteli ya kitalii ya nyota tano iliyoitwa Motel Nzekele ambayo viongozi maarufu duniani kama Mfalme wa Ubelgiji, Rais wa Ufaransa Francois Mitterrand na Papa John Paul II walipata kulala.

Haijulikani kama uamuzi wa serikali ya Rais Magufuli umelenga maendeleo ama tu unataka kufanya jambo la kukumbukwa kwa kuanzisha ‘majiji’ mapya kama ilivyokuwa kwa Gbadolite (maarufu kama Versailles of the Jungle – yaani ‘Versailles ya Msituni’ wakifananisha na Hekalu la Versailles nchini Ufaransa).

Ama haijulikani kama anataka Chato chini ya utawala wake iwe kama majiji ya Astana nchini Kazakhstan, Naypyidaw nchini Myanmar, Oyala huko Guinea ya Ikweta au mji wa ndoto zisizotimia za Dikteta Adolf Hitler wa Germania.

Kwa kurejea uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma, wengi wanaona ni vyema fedha za kujenga uwanja mpya zingetumika kupanua ama kujenga uwanja mkubwa mjini Dodoma ambako ni dhahiri kunahitajika safari za ndege za moja kwa moja badala ya wageni wa nje wa kiserikali kutua Dar es Salaam na kutafuta usafiri mwingine.

Hata hivyo, inafahamika kwamba ni mji wa Astana pekee (zamani ukijulikana kama Akmolisnk, Akmoly na baadaye Akmola) ambao historia yake inatokana na ukweli kwamba ulikuwa ni sehemu ya makazi ya Wacossac wa Siberia waliokimbia utawala wa Yermak Timofeyevich katika Jimbo la Siberia huko Urusi wakati wa karne ya 16.

Lakini miji mingine iliyotajwa hapo juu imeanzishwa katika tawala za kidikteta ambazo zimekuwa na ndoto ya ‘kuacha historia’ kwamba zilifanya jambo la pekee.

Mji wa Naypyidaw ulibadilishwa kuwa makao makuu ya Myanmar kutoka mji wa Yangoon mnamo Novemba 6, 2005 wakati wa utawala wa mkono wa chuma wa Jenerali Than Shwe, ambaye aliitawala nchi hiyo kwa takriban miaka 19 tangu 1992 hadi 2011 alipomwachia ‘mtu wake’ Thein Sein.

Oyala (ambao pia unafahamika kama  Djibloho) ni mji ambao kwa sasa unajengwa ili kuwa makao makuu yajayo ya Jamhhuri ya Guinea ya Ikweta kutoka mji wa Malabo.

Mahali unapojengwa mji huo katika Jimbo la Wele-Nzas ni takriban kilometa 53.8 kutoka Acoacan alikozaliwa ‘rais wa milele’ Teondoro Obiang Nguema Mbasogo.

Licha ya uamuzi huo kupigiwa kelele na wapinzani, lakini Mbasogo, ambaye amemteua mwanaye Teodoro Nguema Obiang Mangue kuwa makamu wa kwanza wa rais, anaona unafaa na anaendelea na ujenzi katika taifa ambalo amelitawala kwa miaka 37 tangu alipompindua baba yake mkubwa Francisco Macías Nguema, Agosti 1979.

Historia inatuonyesha namna ndoto za Hitler za mwaka 1937 kutaka kuijenga upya Berlin ili kuwa mji mkuu wa aina yake duniani katika Dola ya Ujerumani na kuuita Germania zilivyoshindwa.

Binafsi sitaki kuamini kwamba, uamuzi huu wa kujenga uwanja wa kimataifa wa ndege unataka kuibadili Chato kama Gbadolite au mojawapo ya miji niliyoielezea hapo juu, kwa sababu hauna maslahi mapana ya kitaifa.

Tunafahamu sababu za Mobutu kuamua kujenga hata ikulu yake kule kwao Gbadolite kwa sababu ya migogoro iliyokuwepo kabla na baada ya uhuru ambapo asingethubutu kuweka himaya, kwa mfano, Lubumbashi kwenye Jimbo la Shaba, ambako Wacongo na Wazungu walikuwa wakijichotea rasilimali watakakvyo.

Na ili kulitawala taifa hilo la pili kwa ukubwa baada ya Algeria, akaamua kutojenga barabara na yeye akatumia zaidi usafiri wa anga kila alipotaka kuizunguka Zaire.

Leo hii inapojengwa uwanja wa ndege wenye njia ya mruko (runaway) sawa na ile ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKNI jijini Dar es Salaam inatia mashaka kuona kama huu siyo upendeleo kwa sababu tu Rais anatokea huko.

Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam una njia mbili za kurukia; moja kubwa ina urefu wa meta 3,000 (3km) na upana wa meta 46, wakati ile ndogo inayotumika mchana peke yake na kwa ndege ndogo ina urefu wa meta 1,000 (1km) na upana wa meta 30.

Kwamba Rais Magufuli anataka kuona midege mikubwa ya Air Bus (toleo la baadaye baada ya Concorde) na Bombardier ikitua Chato hata kama hakuna biashara zozote kubwa? Ni suala ambalo linaweza kujadiliwa kwa kuzingatia uchumi wa taifa letu ulivyo, vinginenvyo hakuna umuhimu wa kutumia mabilioni ya shilingi kujenga uwanja huo wakati uwanja mdogo wa kawaida ungetosha kujengwa wilayani.

Kutoka Chato hadi makao makuu ya mkoa wa Geita mjini Geita ambako ndiko kwenye shughuli nyingi za uchumi hasa uchimbaji wa madini ni takriban 181.2km kwa barabara na kwa anga ni 58 kilometa tu na inachukua mwendo wa dakika 6 tu kwa ndege.

Mchangiaji mmoja kwenye mtandao wa JamiiForums amesema: “Niliwahi kutua kwenye Uwanja wa Geita pale Mchauru, huu una hata Location Indicator ya ICAO na unafahamika kama HTRU, hawa wana hata "Control Tower". Kutoka Geita pale Mgodini hadi Chato ni kama 100km na ushee. Sijajua kwanini wanapeleka uwanja mkubwa hivi Chato. Sidhani baada ya mkuu JPM kutoka madarakani uwanja huu utatumika kibiashara.”

Aidha, kutoka Mwanza hadi Chato ni umbali wa 455km kwa barabara na 129km kwa anga na mwendo wa takriban robo saa kwa ndege, kwanini basi gharama hizo zisitumike kupanua uwanja wa Mwanza ili uwe wa kimataifa badala ya kuanzisha uwanja mpya? Tayari majirani walio mkoani Kagera wamekumbuka na kuanza kuhoji juu ya ahadi ya siku nyingi ambayo tayari ilishaanza kufanyiwa hadi tafiti, ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Omukajunguti.

Tunafahamu jinsi fedha za Wacongo zilivyopotea bure kwani tangu Mobutu alipong’olewa madarakani Ijumaa ya Mei 16, 1997 na Laurent Desire Kabila, uwanja wa ndege wa Gbadolite, ikulu yake na majengo mengine ya umma yamegeuka magofu na uwanja wenyewe umeota vichaka.

Leo hii ndege kama Bombardier zinaweza kutua Chato wakati bado yuko madarakani, lakini serikali ina uhakika gani uwanja huo utaendelea kuwa na pilika nyingi utakapokuja utawala wa rais mwingine?

Hivi tuamini, kwa staili ya sasa ya serikali, kwamba kila mtawala atakayeingia ataanza kutoa kipaumbele ‘nyumbani kwake’ hata kama hakuna maslahi mapana ya umma?

Wananchi wanaotoa maoni yao kupitia JamiiForums, wanasema hayo ni matumizi mabaya ya rasilimali kwa viongozi hata kama serikali ya awamu hii imelenga kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali.

“Hili lilitokea kwa (Waziri Mkuu mstaafu) Mizengo Pinda, alijenga uwanja mzuri sana Mpanda na wenye tarmac nzuri sana, lakini baada ya kutoka yeye (madarakani) umebaki malisho ya ng'ombe na mbuzi wa Mpanda. Na kwa sasa una hadhi ya "Airstrip" sababu hauna hata Control Tower, hakuna ndege za kibiashara zinazokwenda huko. Kampuni ya Auric Air ilikuwa na safari zake Mpanda, lakini sasa wamesitisha karibu mwaka na ushee. Ulijengwa kwa mabilioni ya fedha. This was one of the "White Elephant" projects of our time,” anasema mmoja wa wachangiaji hao.

Aidha, wanasema uwanja kama ule wa Mpanda ungeweza kujengwa katika eneo lenye lenye pilika nyingi za kibiashara ungeleta manufaa makubwa, ingawa pia haukuwa uamuzi mbaya kuujenga kwa nia ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Wanasema kwamba, serikali ingeweza kujenga Heliport huko Chato ili kumwezesha Mheshimiwa Rais Magufuli kutua wakati akienda mapumziko kama ilivyofanywa pale Msoga  wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete.

“Ni ukweli Rais anahitaji usafiri wa anga aendapo likizo au mapumziko nyumbani, lakini si kwa kujenga Airport Chato. Hivi kweli Chato unajenga njia ya mruko yenye kiwango cha lami,” amehoji kwa mshangao msomaji mwingine.

Akaongeza: “Kuna viwanja tunapaswa kuviboresha maana vina shughuli nyingi za ndege, uwanja kama Songea umechakaa na kila siku kuna ndege moja ya abiria inakwenda, uwanja wa Iringa huu una ndege karibu mbili kwa siku, uwanja wa Kigoma ambao hata ndege za wakimbizi na UN hutua, japo wao kwa kusaidiana na UNHCR wamejenga uwanja Kasulu.”

Wananchi wengi wanaeleza kwamba, kama serikali ni kutangaza rasilimali zikiwemo za utanii hasa Nyanda za Juu Kusini, ni vyema wakapanua viwanja vya Iringa, Morogoro na Ruvuma ili kuwezesha ndege za moja kwa moja kutua badala ya kwenda kujenga uwanja ‘kijijini’.

Wanasema kwamba, ni vizuri kuupanua pia uwanja wa ndege wa Kigoma na Tabora ili kuweka mtandao mzuri wa usafiri wa anga.

“Kuhoji kwetu, si hujuma na shutuma kwa aliye na mamlaka, bali ni tabia ya binadamu kuuliza kile anachoona kinampa utata,” anasema mmoja wa wachangiaji hao.

Hata hivyo, taarifa kutoka serikalini zinaeleza kwamba, hatua ya serikali ya sasa ni kuboresha miundombinu yote baada ya kutengeneza mtandao wa barabara, ambapo sasa wanalenga usafiri wa anga pamoja na reli.

Tayari serikali imekwishanunua ndege mbili aina ya Dash-8 Q400 kutoka Canada na kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, malengo ya serikali ni kuwa na ndege saba katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Katika ununuzi wa ndege hizo za awali, serikali imesema imetoa fedha taslimu ambapo ndege hizo zimefungwa injini za Jet.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *