MAANDALIZI ya sherehe za maadhimisho ya miaka 35 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM) yameingia dosari baada ya Makamu Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi wa chama hicho ngazi ya Taifa, Dogo Mbarouk , kugombana hadharani na mwenyekiti wa Jumuia hiyo ngazi ya mkoa wa Mwanza, Ezekiel Bahebe.
Maandalizi hayo yameingiwa dosari siku chache kabla Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kuwasili jijini hapa wakati wowote leo kwa ajili ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jumuia hiyo zimeliambia FikraPevu kuwa ugomvi huo uliibuka Februali Mosi mwaka huu, majira ya mchana katika ofisi ya jumuiya hiyo mkoa wa Mwanza.
Habari zinasema vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Dogo kuwasili jijini hapa kwa ajili ya maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa cha Chama Cha Mapinduzi; sherehe ambazo mwaka huu zitafanyika kitaifa mkoani hapa.
“ Ugomvi huo ulitokea baina ya viongozi hao baada ya Dogo kufoka kwamba kwa nini miradi ya Jumuia ya wazazi mkoani Mwanza inasuasua; kitendo ambacho mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi mkoani hapa (Ezekiel Bahebe) alikipinga kwa madai kwamba Dogo anaingilia majukumu ya mkoa” chanzo cha habari kilidai kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Chanzo chetu cha habari kinadai kuwa Bahebe alimweleza Dogo pasipo uoga wowote kuwa kwa wadhifa wake, hapaswi kuhoji juu ya miradi ya mkoa na kwamba kufanya hivyo ni kuvuka mipaka ya majukumu yake.
Inadaiwa kwamba Dogo ambaye yuko mkoani hapa kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 35 tangu kuzaliwa kwa CCM, alikutana na kikwazo hicho baada ya kusomewa taarifa fupi ya Jumuia.
Kwa mujibu wa habari, taarifa hiyo iliyosomwa na Katibu wa Jumuia ya wazazi wa CCM mkoani hapa, Habiba Haji, mbele ya Makamu mwenyekiti huyo ilidai utekelezaji wa baadhi ya miradi ndani ya Jumuia hiyo umekwama kutokana na ukata.
Alipoulizwa, Bahebe alisema” Taratibu ziko wazi kwamba ipo mipaka katika majukumu ya kiongozi wa Taifa na Mkoa; lakini hata hivyo ninaomba ukamuulize katibu wangu kuhusu kilichotokea jana “
Alikiri pia kwamba Dogo yuko mkoani hapa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM.
“ Ni kweli jana( yaani juzi Februali Mosi) tulikuwa na kikao na Makamu Mwenyekiti; mwenyekiti wangu wa mkoa , Ezekiel Bahebe alikuwepo na walihitilafiana kidogo tu na Makamu mwenyekiti wa Jumuia ngazi ya Taifa” alikiri Katibu wa Jumuia hiyo ngazi ya mkoa wa Mwanza, Habiba Haji.
Alikiri kwamba hitilafu hiyo ilitokana na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya Jumuia ngazi ya mkoa.
Ingawa hakuwa tayari kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, Katibu huyo alikiri kwamba utekelezaji wa baadhi ya miradi ya Jumuia hiyo unasuasua kutokana na kukosekana kwa fedha.
“ Hata hivyo, Dogo anatarajiwa kutembelea miradi yetu iliyoko katika wilaya ya Geita na baadaye atatembelea mradi wetu wa shule ya sekondari Bulima ambapo atapata fursa ya kuzungumza na wazazi kabla ya Februali 5 ” alisema Katibu huyo.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kesho Jumapili anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 35 tangu kuzaliwa kwa chama hicho, Februali 5 mwaka 1977, siku ambayo mwaka huu imeangukia katika siku ya kuzaliwa kwa zmt
Taarifa hii imendaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza
Hivi kama viongozi kama akina Bahebe wanaoonesha kuwa wanajua misingi, kanuni na miiko ya chama kwa kuzuia Dogo asihoji kuhusu miradi ya jumuia ya wazazi Mwanza, kwanini UELEWA huo na misimamo hiyo wasiitumie kuondoa ubadhilifu na uongozi mbovu unaopigiwa kelele na wanachama na watu wengi ulioko kwenye chama hicho?
kwanini umuhimu wa kufuata taratibu na miiko ya chama unatumika kwa masuala manyonge tu?
kwa nini hawa wazee wasivae ujasiri wakasafisha chama kwa ngazi zote?