WAKATI mkoani Mbeya wakunga wa jadi wakizidi kudharauliwa na kukatazwa kuzalisha wajawazito, halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara imewapa mafunzo wakunga wa jadi 202 kwa ajili ya kuzalisha wajawazito wanaokwenda kujifungulia kwao.
Akizungumza na waandishi wa habari wa masuala ya afya nchini, mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani Bunda Daines Limo alisema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na kujua umuhimu wa wakunga hao ambao wamekuwa kimbilio la wajawazito wengi.
‘’Jamii inawatambua na kuwathamini hivyo nasi hivi karibuni tulitoa mafunzo kwao ikiwa ni pamoja na kuwaeleza umuhimu wa kuvaa glovu wakati mjamzito anapojifungua ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali vikiwemo virusi vya ukimwi(VVU).
Alisema katika wilaya hiyo kuna vijiji 106 tayari wamewapa mafunzo wakunga wawili wawili kila kijiji na kuwa na wakunga wa jadi 202 wanaotambulika na kusaidia huduma ya kujifungua wajawazito ambao wapo mbali na vituo vya afya na hospitali.
Naye Muuguzi mkuu wa hospitali ya wilaya ya Bunda Adelaida Masige alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya kuboresha mawasiliano kati ya wataalamu wa afya wilayani na wakunga wa jadi, taarifa za wanawake wanaojifungulia nyumbani na kwa wakunga zinapatikana tofauti na awali ambapo serikali haikuwa na mfumo wa kuwatambua.
Baadhi ya wajawazito na akima mama wanaonyonyesha wanaoishi katika maeneo ya Bukama, Makongoro kata ya Nyamuswa, Nyabuzumu na kijiji cha Kambubu kata ya Nyamang’uta walisema kuwa kutokana na huduma zisizoridhisha katika vituo vingi vya afya na hospitali teule ya wilaya hiyo(DDH), wanaona ni bora kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
‘’Mimi uzao wangu huu ni wa nane lakini nina watoto watano walio hai na wengine nilijifungulia kwa mkunga wa jadi Mama Nyangi Kisizile kwasababu hospitalini kuna matusi na fedheha nyingi na wala hatusaidiwi’’ alisema Anna Japhet(35) mkazi wa Kijiji cha Kambubu.
Naye mjamzito Agness Baraka (23) anasema mimba aliyonayo ni ya nne lakini ana mtoto aliye hai mmoja na kwamba anahudhuria kliniki lakini bado halidhishwi na huduma za hospitalini hivyo anaona bora kujifungulia kwa mkunga wa jadi ama nyumbani kama alivyojifungua mtoto wake wa kwanza.
‘’Ukienda hospitali mfano kule DDH, wanasema kuwa mjamzito anayepaswa kusaidiwa kujifungua ni yule mwenye mimba ya kwanza lakini tuliowahi kuzaa wanatulazimisha tujifungue wenyewe bila msaada wao na kama hauna pesa unaweza kufa’’ anasema Anna.
Mkunga wa jadi Veronica John Leopard(64), alisema kuwa yeye ni mmoja wa wakunga wanaosaidia wajawazito kujifungua katika wilaya ya Bunda na hata hospitali wanamjua lakini halidhishwi na huduma zinazotolewa na kituo cha afya cha Ikizu maana kila kitu ni pesa na hivi karibuni alimpeleka mwanaye kujifungulia katika kituo hicho na kujionea huduma zisizoridhisha.
Mganga mkuu wa wilaya hiyo Dr. Rainer Kapinga alisema kuwa ni vema jamii wananchi wakaendelea kuhamasishana kwenda kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali ili kupunguza wimbi la vifo vya wajawazito wanaojifungulia nyumbani bila msaada wowote.
Utafiti unaonesha kuwa katika kijiji hicho kuna wakunga wa jadi watatu ambapo eneo la Mugara wilayani humo linaongoza kwa wajawazito kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
Takwimu zinaonesha kuwa akina mama 185 walijifungulia kwa wakunga wa jadi waliopata mafunzo na akina mama 71 walijifungulia kwenye zahanati ya Mugara mwaka 2009.
Ingawa wakunga wa jadi wanapuuzwa na kudharaulika na wasomi wengi katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo mkoani Mbeya, ukweli wa utafiti unaonesha kuwa kujifungulia kwa wakunga wa jadi hasa waliopata mafunzo kunapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la vifo vya akina mama wajawazito.