WANANCHI wa eneo la Tegeta Machakani jijini Dar es Salaam wamewazomea askari wa kikosi cha Zimamoto baada ya kuchelewa kufika kufanya kazi yao ya kuzima moto kwenye nyumba moja mtaani kwao.
"Haohao haooo haooo," hii ndiyo sauti iliyosikika ikiwapokea askari hao walipofika kuzima moto ambao umeteketeza nyumba hiyo.
Akizungumza na FikraPevu katika eneo la tukio, Albert Kashumba, mkazi wa eneo hilo na jirani wa nyumba iliyoteketea, amesema Zimamoto wamefika baada ya saa 1.30 baada ya kuanza kwa moto huo.
Amesema hawakutarajia kuona kikosi hicho kuchukua muda mrefu kiasi hicho hata baada ya kupigiwa simu.
Mmoja wa askari wa kikosi hicho ambaye alikuwa amezongwa na wananchi ameiambia FikraPevu kwamba wananchi wanasema "uongo."
"Sisi tumewahi sana kufika, hatujapokea simu yoyote ya wananchi isipokuwa tumepigiwa na Tanesco ndiyo tukaja, hawa wananchi wanalalamika bure na hatujapokea simu yao hakika," alisema.
FikraPevu imefika mapema eneo la tukio hata kabla wananchi hawajaanza kuzima na ilishirikiana na wananchi kupiga simu Zimamoto, lakini haikupokelewa.
Namba ya kuwapigia Zimamoto ni 114. Hata hivyo wananchi wengi walikuwa wakipiga namba 112, ambayo ni ya Polisi.
Mwenye nyumba hiyo ametambulika kwa jina moja tu la Dada "Guiness", baada ya moto kupamba moto alizimia na sasa yuko hospitali ya Rabininsia, iliyoko Tegeta.