Arusha, Machi 04, 2012 (EANA) – Wataalamu wa Masuala ya Amani na
Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamepitisha azimio la
kuanzisha Baraza la Wazee wa Busara EAC kwa ajili ya kuzuia na kutoa
suluhisho la amani la migogoro ndani ya kanda.
Wataalamu hao waliidhinisha namna Baraza hilo litakavyofanya kazi zake
katika kikao chao kilichofanyika mjini Bujumbura, nchini Burundi hivi
karibuni, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki
(EANA).
Baraza hilo la Wazee litatoa maelekeza kwa kanda kuhusu kuendesha
diplomasia ya kuzuia migogoro na kutafuta suluhisho muafaka pindi
inapotokea.
Baadhi ya migogoro iliyomo kwenye vichwa vya wataalumu hao ni pamoja
na ule wa hivi karibuni unaohusiana na ghasia baada ya uchaguzi mkuu
nchini Kenya, mgogoro wa visiwa vya Migingo, ghasia za Zanzibar kabla
na baada ya uchaguzi na ghasia nchini Uganda, baada ya uchaguzi mkuu.
‘’Tunahitaji viongozi wenye busara na kuheshimika na wasiopendelea
yeyote (wanaume kwa wanawake) kutoka nchi wananchama wa EAC ambao
wanaweza kuingilia kati kuzima mambo kabla ya kufikia katika hatua ya
mgogoro kamili,’’ afisa mmoja aliyehudhuria mkutano huo aliieleza
EANA.
Kwa mujibu wa vifungo vya Mswada wa Awali, Baraza hilo limepewa
mamlaka ya kutoa ushauri kwa mkutano wa wakuu wa nchi, baraza la
mawaziri na katibu mkuu wa EAC katika masuala yote yanayohusiana na
kukuza na kulinda amani,usalama na utulivu katika jumuiya hiyo ikiwa
ni pamoja na kukuza na kulinda pia haki za binadamu , heshima kwa
utawala wa sheria na pia masuala muhimu ya kuelekea katika mtangamano
wa shirikisho la kisiasa.
‘’Baraza linaweza, kama linaona kuna umuhimu, na pia katika hali
ambayo linafikiri inafaa, kujitangazia lenyewe juu ya suala lolote
linalohusiana na kukuza na kulinda amani, usalama na utulivu Afrika
Mashariki na mambo mengine yanayohusiana nayo,’’ inasomeka sehemu ya
mswada huo wenye kurasa 12.
Baraza hilo litakuwa na mjumbe mmoja kutoka kila nchi mwanachama wa
EAC, mwenye kuheshimika sana na huru, mwenye hadhi na ambaye amewahi
kutoa mchango wa pekee katika masuala yanayohusu amani, usalama na
maendeleo katika ngaza za kitaifa, kikanda, bara na kimataifa.
Wajumbe hao pia hawatakiwi kushika wadhifa wowote wa kisiasa muda
wanapoteuliwa kutumikia Baraza hilo.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshughulikia Shirikisho la
Kisiasa, Beatrice Kiraso alisema Baraza hilo la Wazee, litaipatia
kanda hiyo, uwezo wa kuendeesha diplomasia ya kuzuia uwezekano wa
kutokea migogoro itakayoweza kuleta ghasia katika hatua za awali na
kama ikiwa imeshatokea basi litaweza kuidhibiti na kuimaliza kwa
amani.
Mswada wa Baraza hilo utawasilishwa mbele ya Baraza la Pamoja la
Kisekta juu ya Ushirikiano katika masuala ya Ulinzi, Usalama baina ya
nchi na Uratibu wa Sera ya Mambo ya Nje kwa ajili ya kufikiriwa na
kupitishwa kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Imeandaliwa na Dennis Bizimana, EANA