Wapuuza thamani ya kondomu, waivaa mikononi

KONDOMU ya kike ni kifuko cha plastiki kinachovaliwa na mwanawake katika sehemu zake za siri (ukeni), lengo likiwa ni kukabiliana na magonjwa yanayotoakana na vitendo vya ngono.

Kifuko hicho pia ni muhimu kwao ikiwa wanapenda kuwakabili wanaume wasiopenda kutumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ya zinaa, ikiwamo ugonjwa wa Ukimwi na mimba.

Licha ya umuhimu wake kwa binadamu, ukosefu wa elimu sahihi ya matumizi ya kondomu za kike pamoja na bei kubwa, kumesababisha matumizi yake kushindwa kushamili katika jamii ikilinganishwa na kondomu za kiume ambazo zinatumika zaidi kutokana na urahisi wa kupatikana na urahisi wa bei.

Kondomu za kike iliyopo zaidi Tanzania, maarufu kwa jina la Lady Pepeta, zilikusudiwa kutumika kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini hivi sasa zinatumiwa kama urembo na wanawake katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Wakati wataalamu wa afya, wasambazaji na wafanyabiashara wa kondomu wakijiliuza sababu za muitikio mdogo wa matumizi ya kondomu za kike "Lady Pepeta", kutonunuliwa kwa wingi na kutotumiwa kama ilivyo kwa kondomu za kiume, kumbe kondomu hizo zimegeuzwa matumizi na kuwa bidhaa za urembo.

Hayo yamebainika katika Uchunguzi uliofanywa na blogu ya mwandishi wa makala haya katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya, ambapo wanawake wengi hasa mabinti wamekuwa wakinunua kondomu hizo kwa shilingi 100 na kubadilisha matumizi yaliyokusudiwa.

Wakizungumzia matumizi hayo baadhi ya wanawake wamesema kuwa baada ya kushindwa kuzitumia kondomu hizo, walibaini kuwa ndani yake kuna bangili ambayo inafaa kuvaliwa mkononi na isigundulike kama imetoka kwenye kondomu ya kike.

“Nimeshawahi kufanya hivyo na hadi sasa ninavyoongea na wewe nina bangili nyumbani kama kumi hivi za aina hiyo na nikizivaa hakuna anayeweza kutambua kuwa ni bangili za kondomu, kwa hiyo hilo suala ni la kawaida wala siyo la kushangaa,”anasema Joyce Mwakibinga.

Mwanamke huyo anaeleza kuwa kilichomfanya kubadilisha matumizi ni kutokana na kuwa kondomu za hizo za kike ni ngumu kuzivaa kutokana na jinsi zilivyotengenezwa na kwamba zinahitaji muda mrefu wa kujifunza kuvaa na maandalizi ya kuvaa pia huchukua muda mrefu.

Mkazi Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mariam Siyoni anasema ana miaka mitatu akiwa anavaa bangili za kondomu za kike na kwamba hajawahi kuzitumia anapokutana na mwenzi wake.

“Kama nahitaji kutumia kondomu natumia ile ya kiume kwa kumshawishi mwenzangu kwani siyo ngumu kuitumia, lakini hii ya kike ni ngumu na hata wakati mwingine mwanaume anakataa, hivyo tunaendelea kutumia kama bangili kwa kuvaa mkononi lakini siyo kwa matumizi kama ilivyotarajiwa,”anasema.

Mkuu wa oparesheni kanda ya nyanda za juu kusini wa Shirika la Population Service International (PSI) linalosambaza kondomu za kike, Elia Ndutila anasema alifika maeneo ya Kabwe na Kilando, Sumbawanga mkoani Rukwa kufanya uchunguzi na kubaini kuwa wanawake wengi wa Kabila la Wasukuma wamekuwa wakitumia bangili iliyopo ndani ya kondomu ya kike kwa kuivaa mkononi kama urembo.

“Miaka mitatu iliyopita PSI tulipata taarifa za kutumika kwa bangili ya kondomu za kike kama urembo, ndipo nilipokwenda katika maeneo hayo na kukuta wanawake wengi wanazichukua kondomu na kuzitoa bangili hizo na kuzichemsha ambapo inabadilika rangi na kuwa ya kijani na kuivaa mkononi,”anasema.

Anasema kuwa shirika la PSI liliacha kusambaza kondomu ya kike kwa muda wa miaka mitatu iliyopita na kwamba hali ya utumiaji wa kondomu ya kike ni hafifu kutokana na mlolongo wake wa kuivaa haupo kirafiki kwa mtumiaji.

“Hivyo kutokana na hali hiyo ya kutotumika kwa wateja, hata kibiashara inakwama kwani imeshindwa kuliteka soko kama ilivyo kwa kondomu za kiume, " anaongeza.

Ndutila, anasema kwamba kwa mwaka uliopita, usambaji ulikuwa ni katoni tano ambapo kila katoni ina kondomu 180, hivyo jumla ya kondomu za kike 900 zilisambazwa, huku idadi kubwa ikitumika kwa mapambo.

Anabainisha mikoa saba pekee iliyoko kwenye mpango wa kusambaziwa kondomu za kike ambayo ni pamoja na Iringa, Mbeya, Shinyanga, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza,Tabora na Dodoma.

Mfanyabiashara wa duka la dawa na muuzaji mkuu wa kondomu za kike na za kiume maeneo ya nyanda za juu kusini, Imtiaz Bhojan anasema kuwa amewahi kusikia saula hilo la kubadili matumizi ya kondomu za kike kutoka kwa mfanyakazi wake ambaye alimthibitishia kuwa wanawake wanatumia kama bangili, badala ya kutumia kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kujikinga na maambukizi ya virusi ya ukimwi, magonjwa mengine ya zinaa na mimba.

Bhojan anakiri kupokea taarifa nyingi juu ya ugumu wa matumizi ya kondomu za kike, huku akibainisha kuwa wanaume wanapaswa kuwashawishi wanawake kutumia kondomu zao ili wasibadilishe matumizi yake halisi.

Anasema kuwa katika biashara yake, wateja wake wakubwa ni kampuni ambazo hulazimika kuweka kondomu za kike na kiume maeneo ya kazi, lakini kwa mtu mmoja mmoja hakuna anayefika dukani hapo kwa ajili ya kununua kondomu hiyo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Mbeya Dk. Julius Sewangi anasema kuwa kondomu za kike zilipoingia zilichangamkiwa kwa kiasi kikubwa, lakini baada ya muda mfupi hali ilibadilika na kuanza kutotumiwa kama ilivyotarajiwa. Kuhusu kubadilishwa matumizi, anakiri kuwepo kwa hali hiyo huku akitoa mwito kwa jamii kuacha kugeuza matumizi mazuri ya kondomu izo kwa urembo.

“Ni lazima jamii itambue kuwa suala la kuepuka maambukizi ya virusi vya Ukimwi siyo la kuchezea, hivyo ni vyema kila mwananchi kwa kushirikiana na serikali ahakikishe anawajibika kupunguza maambukizi hayo kwa kufuata taratibu na kanuni ikiwa ni pamoja na kutumia kinga kwa matumizi sahihi na sio kufanyia mzaha kama ilivyo sasa,”anasema

Takwimu za sasa zinaonesha kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika Mkoa wa Mbeya yamekuwa yakipungua mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2004 yalikuwa asilimia 13.5, mwaka 2008 asilimia 9.2 na mwaka 2013 ni asilimia 9.0.

Dk. Sewangi anasema kuwa sababu ya kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi Mbeya ni pamoja na kuendesha kampeni ya tohara kwa wanaume, jitihada mbalimbali zinazofanywa kuhamasisha watu kubadili tabia, mpango wa kuzuia maambukizi kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto na matumizi ya dawa za kupunguza mi vya Ukimwi.

Anasema mkakati uliopo ni kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na maambukizi mapya kwa kuwakumbusha wananchi mara kwa mara njia za kutumia ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya kondomu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *