WANANCHI wa mikoa ya Mbeya, Rukwa, Katavi, Iringa, Njombe na Ruvuma wametakiwa kujitokeza kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Wito huo umetolewa na meneja wa kitengo cha damu salama kanda ya Nyanda za juu kusini Dr. Baliyima Lelo alipokuwa katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi.
Dr. Lelo alisema kuwa kundi kubwa linaloongoza kwa kutumia damu hiyo salama ni wajawazito, watoto wadogo chini ya miaka mitano wakifuatiwa na majeruhi wa ajali.
‘’Matumizi makubwa ni kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano wanaoumwa Maralia na watu wanaopata ajali na upasuaji wa kawaida’’ alisema Dr. Lelo.
Meneja wa kitengo cha damu salama kanda ya nyanda za juu kusini Dr. Bliyima Lelo
Alisema watu wanaoruhusiwa kuchangia damu ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 18-65 na jambo hilo analitaja kuwa ni la kizalendo kwasababu damu ya kuongezewa mwanadamu haipatikani kwenye miti bali kwa watu wenyewe.
Alipoulizwa kama katika kanda hiyo anayoiongoza inatimiza malengo ya shirika la afya duniani WHO ambayo yanataka kila mwaka damu ikusanywe unit 45,000.
Alifafanua kuwa kwa mwaka 2012 malengo hayo hayakuweza kutimia ambapo walikusanya unit 18,000 tu.
Baadhi ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo katika upatikanaji wa damu alisema ni pamoja na misingi ya imani ambapo baadhi ya imani za dini haziruhusu waumini wake kutoa wala kuogezewa damu.
‘’Tuhuma za kuwauzia damu salama baadhi ya wagonjwa/ndugu zao zinazoelekezwa kwa baadhi ya watumishi wa hospitali nchini zinazohusika kutoa huduma za kuwaongezea wagonjwa damu salama ni kikwazo cha wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari’’alisema Dr. Lelo.
Kwa upande wake afisa tawala wa kitengo hicho katika kanda hiyo (Zonal Administrator) Sariah Kundael alisema kitengo hicho kipo chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii na kilianzishwa mwaka 2005.
Katibu tawala wa kitengo cha damu salama kanda ya nyanda za juu kusini Sariah Kundael
Alisema kitengo cha damu salama kinahusika katika kukusanya damu, kuipima, kusambaza na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wananchi kujitolea damu.
‘’Damu hiyo inapimwa kwa kuangalia magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa homa ya Ini, kaswende na virusi vya Ukimwi (VVU)’’ alisema Kundael .