Wizara ya Afya isipochukua hatua za haraka, itakuwa ni ndoto kuzuia vifo vinavyotokana na uzazi

Belinda Habibu

Kilio cha upungufu wa vifaa tiba,wataalamu hawatoshi na miundo mbinu ya hospitali,kituo cha afya na zahanati kuwa mibovu ni moja ya sababu ya kuongezeka kwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua ;na kuwalinda watoto wasipate maambukizi ya virusi vya ukimwi wakati wanazaliwa itakuwa ndoto.

Katika zahanati ya kijiji cha Magalata na Mwadui Lohumbo, wilaya ya Kishapu mkoa wa shinyanga ni miongoni mwa zahanati nyingi katika nchi yetu ambazo hazina mashine ya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi,ina wafanyakazi wawili,hakuna dawa za kutosha wala nyumba za watumishi wa afya na zipo miundo mbinu yake ni mibovu.

Muuguzi wa zahanati ya Magalata, Zuhura Suleimani aliyekuwepo hapo toka mwaka 1997, alisema kuna wakati wanawazalisha akina mama bila kufahamu hali zao za kiafya zikoje; kwa kuwa vitendanishi vya VVU hukosekana lakini kwa sasa vimeletwa baada ya muda mrefu kukosekana.
“Mazingira ya kazi yana changamoto nyingi, hatuna mashine ya kupima hata malaria, tunasikiliza historia ya mgonjwa tu”aliongeza nesi huyo.
Alisema hapa hatuna daktari toka mwaka 2006 aliyekuwepo alikwenda kusoma na hakurudi,na tupo manesi wawili tu na mmoja akiwa na dharura basi hali inazidi kuwa mbaya zaidi.

“Kama sasa mwenzangu yuko likizo na amekwenda semina pia nimebaki peke yangu,wakija akina mama wawili tu kwa mfano wanahitaji kuzalishwa sijui kitatokea nini kwa mwanamke mmoja ambaye sitaweza kumuhudumia si kwa kupenda bali nikiwa namuhudumia mwenzake,alisema Zuhura.
Ameongeza anakaa km moja kutoka zahanati hiyo kwa kuwa hakuna nyumba hata moja ya muhudumu wa afya,usafiri wa hapa ni changamoto sana,akiletwa mama kama nitakuwa nyumbani basi inakuwa hekaheka ya kumkimbilia.

Muuguzi Zuhura aliongeza suala la kadi ya akina mama pindi wanapokuwa wajawazito na kuhitaji kujaziwa hali ya maendeleo ya mimba huwa zinakosekana kwa kipindi kirefu,na kunilazimu kuchora katika daftari.

“Kama wamekuja wanne itabidi wasubiri tu mpaka nimalize kuchora kama kadi halisi ilivyo, katika daftari zao, hunichukua hata saa nne na zaidi kumaliza”alisema nesi huyo.

Alisema akina mama wengi wanajifungulia nyumbani hasa wale tunaowaambia wanavidokezo vya hatari kuwa waende hospitali kuu, kwa sababu ya gharama na umbali wa zaidi ya km 100 kuifikia,hivyo huamua kuzalia nyumbani.

Aliendelea kusema dawa za kukata damu zilizoshauriwa kuwepo katika zahanati, (Egometric) pindi mama anapojifungua huwa zinakosekana mara kwa mara tena kwa kipindi kirefu na hii ni hatari tunaweza kumpoteza mama.

Pamoja na jitihada zake hizo akiwa na mwenzie, wanafanya usafi wa zahanati, ikiwemo kudeki, kufyeka na kufua mashuka ya wagonjwa na kuwatibu wagonjwa wengine wote wanaoumwa malaria,kushona vidonda, kuhara, kliniki kwa akina mama na kuzalisha ,kutoa chanjo kwa watoto na magonjwa mengine.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Burugu Mipawa alisema kutokana na hakuna basi, na barabara kuwa mbovu, hakuna madaraja ya uhakika kipindi cha mvua, ukipanda boda boda hadi Munze ni sh.elfu 50 na ukifika shinyanga mjini kwa gari la kukodi basi sh.250,000/=.

Akiwafundisha fellows wa mwaka 2012, katika ukumbi wa Tanzania Media Fund, Dr. Moke Magoma kutoka ‘Evidence for Action’ alisema ni lazima kila upande uwajibike kwani mimba si ugonjwa maandalizi yanaweza kufanyika.

“Kwa upande wa familia lazima wajiandae kumpokea mtoto anayekuja kwa kuhakikisha mama anakula vizuri,anapumzika na kuwahishwa sehemu ya kutolea huduma ya afya mapema, iwe hospitali,kituo cha afya ama zahanati,”alisema Dr. Magoma.

Ameongeza mama akifika hospitali, ama kituo cha afya ama zahanati basi akute mahitaji yote,dawa zipo,wahudumu wa afya wapo waliohitimu mafunzo hasa, damu ipo,hii inawahusu zaidi upande wa serikali, na tunaweza kusema sasa tunapunguza vifo vya akina mama kwa vitendo.

Katika zahanati ya Mwadui Lohumbo hakuna tofauti sana na ile ya Magalata,hapa pana muuguzi mmoja na daktari mmoja,na wakati nikiwa hapo kwa wiki nzima walikuwa wameifunga zahanati hiyo na kwenda semina.

Jirani na zahanati hii yupo muuguzi mkunga aliyestaafu ila aliwahi kufanya kazi hapo toka mwaka (1980-1997) aliyejulikana kwa jina la Elizabeth Bushesha, alisema mazingira ya kazi ya sasa na ya zamani katika kutoa huduma hii ya afya ni tofauti.

“Enzi zetu dawa zilikuwepo, na mazingira ya kazi kwa ujumla wake yalikuwa mazuri, hapa pana nyumba ya wauguzi, kiukweli ni gofu sasa mimi nilikaa humu na mwenzangu wakati nikiwa kazini”alisema Elizabeth.

Ameongeza hapa kijijini tupo wauguzi wakunga wawili tuliostaafu, kutokana na mazingira ya kutokuwa na wahudumu wa afya wa kutosha, tumeamua kujitolea kuzalisha akina mama.

“Hatulipwi na serikali kama ukitoa huduma hii kwa mama basi ndugu zake ama mume, waamue kukupa asante kama elfu mbili, ama tano na kwa wengine wenye hali mbaya kiuchumi basi tunazalisha bure” alisema nesi huyo.

Alisema akina mama wanaokaa mbali huwa wanaletwa kituoni hapo na boda boda ama baiskeli na kama kuna dharura basi inabidi sisi tupande usafiri huo kumfuata mama anayehitaji kujifungu na kumsaidia.

Changamoto kubwa iliyopo ni upungufu wa vifaa tiba kama mashine ya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi hakuna,na wakati mwingine hakuna ‘gloves’ ni hatari sana kwa watu wote watatu, mama, muuguzi na mtoto anayezaliwa kuweza kupata maambukizi.

Alitoa wito kwa serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na hasa vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watu, hospitali kubwa ziko mbali na hakuna usafiri wa kufika huko kwa urahisi.

Akizungumzia suala la upungufu ama kutokuwepo kwa vifaa tiba,mganga mkuu wa wilaya ya Kisarawe Dr. Mwendo Msengi alisema katika hospitali yake kwa mwaka jana madaktari wanne waliacha kazi kwa sababu ya kuona hawafanyi kazi waliyoisomea kutokana na ukosefu wa dawa,vifaa vya kazi ili hali wagonjwa wapo wengi wenye magonjwa mbalimbali.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya Dr.Japhet Makelele alisema ni kweli kwa zahanati ya Mwadui Lohumbo hakuna mashine ya kupima virusi vya UKIMWI, ingawa ilikuwepo hapo awali sababu iliharibika na ilipoagizwa nyingine kwa kipindi hicho zilikuwepo feki nyingi na serikali ilibidi iagize zingine.

“Mashine ya sasa inagharama na zinakuja chache tunaagiza 100, tunaletewa 40 kinachofuata zahanati zingine zinakosa”alisema kaimu huyo.
Kutokuwepo kwa mashine hizo kunaweza kuongeza idadi ya watoto wenye virusi vya ukimwi ambapo wangeweza kukingwa.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mwadui DDC, ambayo iko karibu na zahanati hiyo, Magreth John alisema katika shule yake kuna watoto wawili ambao wameathirika na ugonjwa wa ukimwi na wanatumia dawa (ARVs) tayari, mmoja yuko darasa la pili na mwingine yuko darasa la nne.

Aidha, ukitaka kujisaidia katika vyoo vya zahanati hii huwezi, ni bora ukaingia porini, vyoo vimejaa, vimechakaa majengo toka enzi ya mkoloni, choo cha kina mama nacho kimejaa na hata cha wafanyakazi wa afya wa zahanati hiyo hakifai kimezungukwa na nyasi ndefu.

Afisa mtendaji wa kijiji hicho Musiba Atanasi anasema hafahamu kama zahanati hiyo vyoo vyake havifai kwa matumizi na wala kujua kama mganga na muuguzi hawapo kituoni hapo kwa wiki nzima, ingawa umbali wa kutoka ofisi ya kijiji na zahanati hii ni mita 200 tu.

Kaimu mganga mkuu Dr. Makelele tena alisema kwanza kutokuwepo kwa wahudumu wa afya katika zahanati ya Mwadui Lohumbo kwetu ni “breaking news” hatukuwa tunafahamu, ila tunajua sasa hivi mmoja anatakiwa aende semina ya dawa kule Mwanza kwa siku tatu akirudi mwingine aende.

Ameongeza itabidi tufuatilie tujue nini kilitokea mpaka wote wasiwepo kwa wiki sasa, wakati utaratibu ni huo nilioutaja hapo awali.

Kuhusu hali ya kujaa vyoo vya zahanati hiyo kaimu afisa afya wa wilaya Daniel Madaha amesema walishaweka mkakati kati ya wananchi na wahudumu wa afya kupitia kamati za afya za vijiji, ninachoweza kusema kuna uzembe kidogo kati yao umefanyika.

“Wananchi kupitia mfuko wa afya ya jamii (NHIF) wanachanga fedha nyingi sana na matumizi yake ni itumie katika ukarabati mdogo mdogo kama wa vyoo,kununua dawa na vifaa,”aliongeza afisa Madaha.

Ameongeza sharia ya afya ya mwaka 2009, inasema kama hali ya mazingira ya zahanati,kituo na hata hospitali kama si mazuri, kama usafi wa vyoo inanipa mamlaka ya kuifunga, lakini kwanza natoa notisi ya siku 14 kama hakuna kinachoendelea naifungia kutoa huduma.

“tumeshafunga zahanati tatu mwaka jana (2012) mwezi wa tisa, kwa sababu ya kutokuwa na vyoo,nazo ni zahanati ya Hilebelebe, Kinampanda na Beledi,kwa wiki mbili na ndani ya siku 10 walijenga vyoo”alisema afisa huyo.

Kaimu mganga mkuu Makelele aliongeza tena, kwa kusema unajua hatuwezi kufanya kazi wilaya nzima bali tunategemea wenzetu walio katika vituo hivyo kutueleza changamoto zao,wakikaa kimya hatuwezi kujua.

Alipoulizwa hakwenda kujisaidia siku ambayo walikaa kutwa nzima wakitoa mafunzo katika zahanati hiyo, kaimu mganga mkuu huyo alisema hapana, sikwenda kujisaidia,tungekuwa tumeona hali hiyo.

Kwa kuwa wafanyakazi wa zahanati hiyo hawakuwepo kwa wiki nzima na namba zao hazikupatikana kijijini hapo, wangeweza kutuambia ni mara ngapi wameripoti tatizo hilo iwe serikali ya wilaya ama kuu.

Uchunguzi kuhusu hali ya huduma katika zahanati hiyo ya Mwadui Lohumbo ulianza kufanyika tangu mwezi oktoba mwaka jana (2012), na kubaini hali ya kujaa kwa vyoo, uchakavu ulikuwa ni ule ule kama ilivyo wakati huu.

Kwa upungufu wa wahudumu wa afya katika zahanati hizo kaimu huyo alisema zinashabihiana na zahanati za Nyenze,Bulima , Ngeme, Ikonda, Seseko ,Kisesa, Mwajidalala na Beledi kwa kuwa zinaongozwa na mhudumu wa afya aliyepewa mafunzo na ni mmoja kwa kila zahanati.

“Suala la upungufu wa watumishi wa afya ni janga la kitaifa na wilaya ya Kishapu imeathirika sana”aliongeza kaimu huyo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umegundua kwa hospitali,kituo cha afya ama zahanati za mijini kama jiji la Dar es Salaam, wafanyakazi wa afya wanazamu za kuingia kazini,wengine asubuhi wanatoka jioni na wengine hukesha na kutoka asubuhi tofauti na vijijini.
Kama alivyosema kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu kuwa zipo zahanati 10 zinazoendeshwa na wahudumu wa afya waliopewa mafunzo,wanaojulikana kitaalaam kama ‘medical attendant’.

Hali iliyopo katika zahanati hizo mbili pia imekutwa katika zahanati ya Ifinga mkoani Ruvuma na ile ya Kiegei wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Katika kituo cha afya cha Kinesi wilaya ya Rorya, hakuna shimo la kutupa ‘placenta’ na mama aliyejifungua hukabidhiwa atajua anatupa wapi,wodi ziko mbili watu wote hulazwa humo humo.

Katika kituo cha afya cha Iguna,hakuna ‘gloves’ kuna vitanda 12 na kuhitajika zaidi ya 20,hakuna mashine ya kupima damu pia.

Katika hospitali ya Butiama nyumbani kwa Mh.baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuna mifuko ya kuhifadhia damu kama mama mjamzito ama yeyote akitaka kuongezewa damu,itabidi ndugu zake wakanunue katika maduka ya dawa waulete ndipo awekewe.

Katika utafiti uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Sikika, na kutolewa katika jarida lake la tarehe 3/9/2011, unaonyesha katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, ilibaini tatizo kubwa la makazi kwa wahudumu wa afya, ambao wanalazimika kuishi katika vibanda vya nyasi, badala ya kujengewa nyumba zenye hadhi ya mtumishi wa afya ikiwa ni motisha kwa watumishi hao.

Sera ya afya ya mwaka 1990 na ikapitiwa mwaka 2007, inasema msisitizo wake, ulikuwa ni kuinua hali ya afya kwa wananchi wote na kipaumbele kilitolewa kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuugua ambayo ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wanawake wajawazito na wananchi wote. Aidha, sera ililenga kuweka mfumo wa huduma za afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.

Sera hii pia imeongeza katika kipengele cha (iii),cha mafanikio yake,kuwa, uwezo, uzoefu na mifumo ya kutoa huduma ya mama na mtoto na ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza yakiwemo maradhi makuu kama vile malaria, kifua kikuu na UKIMWI umejengwa na kuimarika.

Pia imeendelea kueleza katika moja ya mapungufu yake kufikia malengo yaliyokusudiwa, kipengele cha (ii) kimesema, kuna uhaba wa wataalam wa kada mbalimbali, vifaa, dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika sekta ya Afya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *