WANANCHI wa kijiji na kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, wamekosa huduma ya matibabu kwa siku nane mfululizo katika zahanati ya kijiji hicho baada ya watumishi wa zahanati hiyo kusitisha huduma za utowaji wa matibabu.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Makala haya na kuthibitishwa na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,umebaini kuwa watumishi wa zahanati hiyo wamesitisha huduma za utoaji wa matibabu katika zahanati hiyo na kwenda kuhudhuria semina jijini mwanza.
Kadhalika Zahanati hiyo inakabiliwa na mazingira machafu kutokana na vyoo vinavyotumiwa na akina mama wajawazito pamoja na wale wanaokwenda kliniki kujaa kinyesi pamoja na vile vinavyotumiwa na wahudumu.
Hii ndiyo zahanati ya Mwadui-Lohumbo iliyofungwa kwa siku 8 na wagonjwa kukosa huduma.
Zahanati hiyo inayohudumia zaidi ya wananchi 5000 wa kijiji hicho inao watumishi wawili wanaotoa huduma za kiafya,ambapo kuna muuguzi mmoja na Nesi mmoja tu,hali ambayo imekuwa ikisababisha pia utoaji wa huduma kuwa hafifu.
Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Japhet Makelele amestushwa na taarifa za kufungwa kwa zahanati hiyo kwa siku nane mfululizo,hali iliyosababisha usumbufu kwa wagonjwa katika upatikanaji wa huduma za matibabu.
“Hizi ni taarifa ngeni sana kwetu,ndiyo kwanza nasikia kutoka kwenu,silijui,lakini kama ni kweli basi hii ni hatari sana kwa maisha ya watu,hii zahanati inategemewa na watu iweje ifungwe kwa siku 8 mfululizo?!….’’ alisema na kuhoji Kaimu mganga huyo wa wilaya.
Alisema “tunashukuru kwa taarifa tunakwenda kufanyia kazi mara moja,lakini ninachojua mimi ni kwamba pale kuna watumishi wawili ambao hata hivyo hawatoshelezi ikama,lakini wamekuwa pia wakipishana katika kuhudhuria mafunzo ya namna ya usambazaji wa dawa za binadamu mwanza….’’.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Kulwa Kija alisema wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa huduma za kiafya katika zahanati hiyo,kutokana na uchache wa watumishi hao.
“Pamoja na kwamba ni wachache sana kwa sababu wako wawili,lakini wamekuwa wakifunga huduma saa 9:30 kila siku na kuwaacha wagonjwa bila kupata huduma….’’ Alisema Kija.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakilazimika kuwakimbiza wagonjwa wao mjini Shinyanga umbali wa zaidi ya kilomita 40 ili kunusuru maisha yao.
Naye Bi Amina Dotto akizungumzia hali hiyo alisema wiki iliyopita watoto wao wameshindwa kupata vipimo vya Kliniki kutokana na kutokuwepo kwa huduma hiyo katika zahanati hiyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Japhet Makelele alikiri kuwepo na upungufu wa watumishi latika zahanati hiyo,na kuongeza kwamba hilo ni janga la Kitaifa na hasa katika wilaya hiyo.
“Tatizo la upungufu wa watumishi katika idara ya afya ni janga la kitaifa,na hasa hapa kwetu Kishapu hili ni tatizo kubwa sana,na tena kwenye zahanati hiyo kuna uafadhali kuna zahanati nyingine hapa kwetu zina mtumishi mmoja…..’’ alisema Kaimu Mganga mkuu huyo wa wilaya.
Alitaja baadhi ya zahanati zenye mtumishi mmoja mmoja (Medical Atendat) kuwa ni Nyenza,Bulima,Ngema,Ikonda,Seseko,Kisesa,Mwagidalala na Beledi.
Kuhusu suala la uchafu wa mazingira ya zahanati hiyo,Bwana Afya wa wilaya hiyo Daniel Madaha alisema endapo itathibitika kwamba mazingira yake ni machafu hali inayoatarisha usalama wa afya za wagonjwa,idara ya afya italazimika kuifunga.
“Sheria zetu za afya ziko wazi,tunakwenda huko tukibaini na kujiridhisha kwamba mazingira yake ni machafu,tutaifunga mara moja nah ii si mara ya kwanza kufunga zahanati kwenye wilaya hii,tumewahi kuzifungia nyingine….’’ Alisema Madaha.
Kwa mujibu wa Bwana Afya huyon wa wilaya mwaka jana mwezi Septemba ofisi yake ililazimika kuzifungia zahanati nne zikiwemo Ilebelebe,Kinampanda na Beregi kutokana na kuwa katika mazingira machafau yaliyohatarisha afya a wagonjwa.
“Tulizifunga kama sheria inavyosema hadi baada ya wiki tatu hadi nne zilizofanyiwa usafi ikiwa ni pamoja na kuchimba vyoo,kwa hiyo hata hicho tutakifunga,kwa sababu inaonekana ni uzembe wa watumishi lakini na wananchi kwa ujumla….’’ Alisisitiza Madaha.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Nicholaus Besisila akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake hivi karibuni,alisema ofisi yake haijapata taarifa za hali hiyo na kuahidi kulifuatilia na kisha kuchukua hatua.
“Kama kweli jambo hilo lipo,hilo ni kosa kubwa sana,huwezi kufunga zahanati eti kwa sababu unakwenda semina,hili ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu kufanya hivyo ni kwamba unakuwa umeweka rehani maisha ya wagonjwa wanaokwenda kupata huduma…’’ alisema Basisila.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Kishapu Lothen Simkoko alipoulizwa juu ya kuwepo kwa taarifa hizo alionesha mshangao mkubwa,na kuahidi kwenda kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kufuatilia na kujionea hali hiyo.