ZANZIBAR: Umoja wa Ulaya wataka Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK), CUF waandamana!

Jamii Africa

Umoja wa Ulaya(EU) umeishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupendekeza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Van de Geer amesema kuwa anategemea mkwamo wa kisiasa kati Serikali ya Zanzibar na Chama Kikuu cha Upinzani Visiwani humo, CUF utatatuliwa siku za karibuni.

Balozi de Geer amesema kuwa Umoja huo uko kwenye mazungumzo na Serikali ya Rais Magufuli na wanategemea Rais ataanzisha majadiliano kutatua mgogoro uliopo na hatimaye CUF kuingizwa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilifikia tamati baada ya Uchaguzi wa Marudio, tarehe 20, Machi 2016 baada ya CUF kususia uchaguzi huo kwa madai kuwa wa Oktoba 25, 2015 uliofutwa walishinda na wa marudio ulikuwa hauko kisheria na usingekuwa huru na haki.

Umoja wa Ulaya umepunguza mahusiano yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein tangu Ujumbe wa waangalizi wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya uliokuwa ukiongozwa na Bi. Judith Sargentini kupinga Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20, 2016.

Chama cha CUF ambacho kinaonekana kiko tayari kwa ajili ya mazungumzo ingawa Serikali ya Zanzibar imewahi kukaririwa ikisema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK) ilishazikwa, japokuwa inatambuliwa na Katiba ya Zanzibar.

Chama cha Mapinduzi Zanzibar kimesema kuwa ni vigumu kufanya na majadiliano na Chama cha CUF wakati chama hichi kilishatangaza kutoitambua Serikali ya Zanzibar. CCM imeitaka CUF kusubiri mpaka uchaguzi mkuu wa 2020.

Baadhi ya Wabunge wa CCM Zanzibar na Wanasiasa wamewahi kukaririwa wakisema watapeleka hoja Bungeni wa kuitaka Serikali ya Zanzibar kuanzisha mchakato wa kura ya maoni(Referendum) kuuliza wananchi kama bado wanakitaka kipengele cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Mwezi Septemba mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Mpendaye, Mohamed Said Mohamed(CCM) alipeleka hoja Bungeni na kuungwa mkono na wenzake akitaka kipengele cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kiondolewe kwenye Katiba hata hivyo hoja yake ilishindwa.

Japokuwa kuna shinikizo kubwa kutoka kwa makada wa CCM wanaotaka kubadilishwa Katiba na kuondoa kipengele cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK), bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) ina kigugumizi.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa Vyama vingi mwaka 1992, mara zote uchaguzi Visiwani Zanzibar umekuwa na ushindani mkali na uchaguzi unapomalizika lazima kuzuke mgogoro kati ya vyama vikuu vya CCM na CUF.

Chaguzi za Mwaka 1995, 2000 na 2005 zilifuatiwa na migogoro huku CUF mara zote ikiamini kuwa ilishinda na CCM ilifanya udanganyifu kwenye kura.

Mwaka 1997, wanaharakati wa Chama cha CUF walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi, ilipofika mwaka 1999 Jumuiya ya Madola iliingilia kati mgogoro Zanzibar kati ya CCM na CUF na kuzalisha kitu kilichoitwa Muafaka 1.

Juhudi za Muafaka 1 zilishindwa na kuzalisha Muafaka 2 ambapo pia juhudi hizo zilishindwa kufikia maridhiano mpaka mwaka 2005 Rais Kikwete lipoingia madarakani na kuanzisha mazungumzo yaliyoanzisha mpango kazi uliokuja kuzaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK).

Julai mwaka 2010 Wazanzibari walipiga kura ya maoni na asilimia 68.7 walikubali kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

maandamano_cuf_dec16

Wakati hayo yakiendelea, Vijana wa Chama cha CUF huko Unguja wameandamana leo wakidai wanataka kujua hatma ya maamuzi yao baada ya Uchaguzi 2015.

Vijana hao walimiminika Makao Makuu ya chama hicho huko Mtendeni wakimtaka kiongozi wao, Maalim Seif Sharif Hamad atoe kauli kuhusu muhstakabali wa 'nchi yao'.

Msomaji, ni nini hatma ya Zanzibar? Tupe maoni yako…

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *