Maambukizi ya Mfumo wa upumuaji yanachangia asilimia 10.5 ya watoto wanaotibiwa hospitalini

Jamii Africa

Matumizi ya nishati ya asili katika shughuli za binadamu yamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira, lakini nishati hiyo inatajwa kuathiri zaidi afya za watoto hasa maambukizi  katika mfumo wa upumuaji na kuchangia ongezeko la vifo vya watoto walio na umri wa miaka mitano.

Katika nchi zinazoendelea ambazo zipo zaidi Afrika, matumizi ya nishati asilia ikiwemo mkaa, kuni, kinyesi cha wanyama na mabaki ya mazao yamekuwa kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na nchi zilizoendelea ambazo kwa sehemu kubwa zinatumia nishati mbadala.

Nishati hiyo hutumika kwa ajili ya kupikia, kuongeza mwanga na joto ndani ya nyumba, lakini matokeo yake hutengeneza hewa chafu ya ukaa ambayo inaathiri mfumo wa upumuaji hasa mapafu.

Zaidi ya watu bilioni 2 duniani hutumia nishati asilia kama chanzo kikuu cha nishati katika nyumba zao ambapo asilimia 30 ni watu wanaoishi mjini ambao hutumia zaidi mafuta ya taa na mkaa na asilimia 90 ni watu waliopo vijijini ambao hutumia kuni, vinyesi vya wanyama na mabaki ya mazao.  Kutokana na matumizi makubwa ya nishati asilia duniani, matumizi haya huchangia asilimia 76 ya uchafuzi  wa hewa inayotengenezwa ndani ya nyumba za watu. 

Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Umea kitengo cha Afya ya Jamii kilichopo nchini Sweden mwaka 2011 unaonyesha kuwa  dalili za maambukizi ya mfumo wa upumuaji kwa watoto huwa ni  kukohoa, kupumua kwa shida, maumivu kwenye koo la hewa, kifua kubana, kutokwa na kamasi, matatizo ya masikio, kupumua kwa haraka, kutembea kwa shida na homa.

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa nyumba nyingi za Tanzania hasa maeneo ya vijijini hazina mfumo mzuri wa kutoa hewa ukaa inayozalishwa na matokeo yake sehemu kubwa ya hewa hiyo hubaki ndani ya nyumba na kuathiri mfumo wa upumuaji kwa watoto kuvuta hewa chafu. Pia watoto ni waathirika wakubwa kwasababu wanatumia muda mwingi kukaa jikoni na mama zao kuliko makundi mengine.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza mwaka 1993 watoto milioni 3 walio chini ya miaka mitano walikufa kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa na wengine milioni 1.1 walifariki kutokana na kupata maambukizi  yanayoambatana na  ugonjwa huo.

Inaelezwa kuwa matumizi ya nishati asilia ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya mfumo wa upumuaji (Acute Respiratory Infection) ambayo yanaongoza kusababisha  vifo vya watoto walio chini ya miaka 5 ambao wanalazwa hospitalini kutokana na magonjwa mbalimbali ya utotoni hasa katika nchi zinazoendelea.

Mpango wa Taifa wa Kuzuia Maambukizi ya Mfumo wa Upumuaji  katika uchunguzi wake uliofanyika katika vituo 14 vya afya unaonyesha kuwa asilimia 10.5 ya watoto waliopelekwa kutibiwa katika vituo hivyo walikuwa na dalili za maambukizi ya mfumo wa upumuaji ambapo asilimia 50 walikuwa watoto walio chini ya umri wa mwaka mmoja.

 

 Watoto walio katika hatari ya Kuambukizwa

Ugonjwa huo una mahusiano ya moja kwa moja na hali ya kipato cha familia, ambapo watoto wanaoishi katika familia masikini wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa magonjwa ya mfumo wa upumuaji ikizingatiwa kuwa nishati asilia ni chanzo kikubwa cha mwanga na kupikia.

Nyumba nyingi za vijijini zimeezekwa kwa nyasi huku zikiwa na madirisha madogo ambayo hayapitishi hewa kwa urahisi. Vilevile kwa wakazi wa mjini baadhi yao hawazingatii ujenzi wa nyumba zenye mfumo mzuri wa kutolea hewa.  

Utafiti huo Chuo Kikuu cha Umea  (2011) unafafanua kuwa watoto kutoka familia maskini ambao walikuwa wanakohoa ni asilimia 31.4, familia zenye kipato cha kati ni 28.5% na familia zenye kipato kikubwa ni 21.4%. Pia matokeo yanaonyesha kuwa watoto kutoka familia maskini walikuwa wanakohoa mara 1.7 zaidi ya wale wa familia tajiri.

Inaelezwa kuwa uwezekano wa watoto  wanaotoka katika familia masikini kuendelea kusumbuliwa na magonjwa ya mapafu ni mkubwa ikiwa hatua hazitachukuliwa ili kubadilisha mazingira wanayoishi ambayo hayawahakikishii usalama wa afya zao.

 

 Jinsi ya Kukabiliana na Maambukizi

Ili kuzuia maambukizi hayo kabla hayajasambaa kwa watoto wengi, serikali imeshauriwa kutengeneza sera ambayo inayotoa muongozo wa ujenzi wa nyumba bora ambazo zinakuwa na mfumo mzuri wa kutoa hewa na matumizi sahihi ya nishati za asili.

Pia  juhudi zinahitajika kuwawezesha wanawake na watoto kiuchumi ili kutengeneza kipato cha familia kitakachochea matumizi ya nishati mbadala ya gesi ambayo madhara yake kwa afya za binadamu ni madogo. Mabadiliko hayo ni muhimu yaende sambamba na elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi za kujikinga na magonjwa ya mfumo wa upumuaji katika maeneo mengine ya uzalishaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *