Marejea kumaliza tatizo la mbolea nchini

Albano Midelo

TATIZO la wakulima kutegemea ruzuku ya mbolea za chumvi chumvi ambazo  zinauzwa kwa bei ya juu na kuleta madhara makubwa katika udongo linaweza kumalizika kabisa iwapo serikali itaweka msukumo katika matumizi ya mbolea ya marejea.

Historia inaonesha kuwa kilimo mseto kwa kutumia mradi wa kurutubisha ardhi kwa kutumia mbolea ya marejea ulianzishwa mwaka 1942  Peramiho mkoani Ruvuma na padre Otmar Morger OSB wa kanisa katoliki ambapo mwaka 1963 mbolea ya marejea ilitumika kuzuia magugu na kulishia mifugo na mwaka 1983 ilianzishwa benki ya mbegu za marejea Peramiho.

Mwaka 1987 baada  ya kuona umuhimu wa marejea katika kurutubisha ardhi kilianzishwa kituo cha mradi wa kurutubisha  udongo kwa kutumia marejea  Peramiho(MRUMA) kituo ambacho hadi sasa kipo kinaendelea kusambaza mbegu za marejea pamoja na  kutoa elimu ya kutumia mbolea ya marejea kwa wakulima katika nchi nzima.

Shamba la marejea

Gabriel Mhagama ni mkuu wa kituo cha MRUMA  anasema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho hadi hivi sasa watalaamu na wasomi kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wamekuwa wafika kufanya utafiti kuhusu mbolea ya marejea na kwamba tafiti zao zimeonesha mbolea hiyo ina uwezo wa juu katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ukilinganisha na mbolea za kemikali.

Hata hivyo Mhagama anasema utafiti uliofanywa katika kituo cha MRUMA tangu mwaka 1942 umebaini kuwa mimea ya porini aina marejea inachukua nafasi ya kwanza kwa kurutubisha ardhi na mkulima akitumia mbolea hiyo ana uwezo wa kuzalisha mazao mara dufu zaidi ya kutumia mbolea za viwandani.

Utafiti uliofanywa na kituo cha kilimo Uyole Mbeya umegundua kuwa mkulima kwa kutumia mbolea ya viwandani anaweza kutumia  mifuko nane yenye thamani ya shilingi 480,000 kwa shamba la hekta moja ambazo sawa na ekari mbili na nusu na kupata mahindi chini ya gunia 14 tu ambapo kwa kutumia kilo 20 za mbolea za marejea ambayo sawa na shilingi 16,000 mkulima anaweza kulima hekta moja  na kupata magunia 68 ya mahindi yenye uzito wa kilo 100.

Kulingana na Mhagama kituo chake cha MRUMA mwaka 1992 kiliweza  kutoa mbegu za marejea tani 65 ambazo zilisambazwa kwa wakulima katika mikoa yote nchini na kwamba mafunzo ya marejea  tangu mwaka 1987 hadi 2011 yameweza kutolewa kwa vikundi vya wakulima 3200 katika nchi nzima.

“Karibu nchi zote zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara zinachukua tani za mbegu za mbolea za marejea kutoka hapa Peramiho baada ya kubaini umuhimu wa mbolea hiyo,hadi sasa tumesambaza mbegu za mbolea za marejea katika nchi 121 duniani zikiwemo nchi za bara la Ulaya,Marekani,Australia  na Brazil, katika nchi hizo pia tunapeleka vitabu vinavyotoa elimu ya marejea’’,anasisitiza.

Mhagama anabainisha kuwa marejea  ni mbegu zinazofanana na  mbegu za ufuta ,baada ya kupandwa   na kuota ni lazima kufyeka marejea yenyewe baada ya wiki mbili hadi  mwezi mmoja na kuyageuza kwa kuchanganywa na udongo ili yaoze iwapo unataka kulima mazao katika shamba hilo ndani ya mwaka huo.

Kulingana na Mhagama mbolea ya marejea ndiyo majibu ya mkulima ambaye hawezi kumudu kununua mbolea ya viwandani kwa kuwa mbolea hiyo  hurutubisha na kudumisha rutuba ardhini,vijidudu viitavyo bacteria hutoboa mzizi wa marejea na kusababisha vijinundu ambavyo ni nyumba yao na bacteria hao hutangua hewa aina ya naitrojen kama mbolea kwa kulishia mimea.

“Siku zote tunawambia watu kwanini wanang’ang’ania kulima mazao kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi wakati zinawaumiza,badala ya kuchukua mbolea ya marejea ambayo hayana gharama yametolewa porini,watu wamekusanya na kuyaleta katika kituo chetu hapa Peramiho, mbegu za marejea hivi sasa zimeenea nchini kote”,anasema Mhagama.

“Wakulima ili wafanikiwe katika mbolea ya marejea wanatakiwa kubadili mazao kwa mfano mwaka wa kwanza katika ekari moja anapanda marejea,mwaka wa pili anapanda mahindi mwaka wa tatu anapanda mtama mwaka wa nne anapanda marejea pia anaweza kuchanganya mazao mwaka wa kwanza anapanda marejea na kahawa,mwaka wa pili marejea na jamii ya kunde,mwaka wa tatu marejea na mihogo na mwaka wa nne marejea ,migomba na  miti”,anasema.

Utafiti zaidi umebaini kuwa mbolea ya marejea  hupunguza na kuzuia magugu shambani,marejea ni malisho kwa wanyama pia majani yake ni mboga na mabua hutumika kwa ajili ya matandiko ya wanyama,marejea pia huzuia wadudu waharibifu.

Miaka ya 1983 mbolea ya marejea ilianza kutumiwa na wakulima wengi katika sehemu mbalimbali nchini ambapo wakulima na vikundi vya wakulima walifika katika kituo cha MRUMA Peramiho kujifunza kuhusu uzalishaji wa mbolea hiyo  hali ambayo ilisababisha maelfu ya tani za mbegu za marejea kununuliwa na kwenda kuzalishwa.

“ Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere alikuwa ni mfuasi mkubwa wa mbolea ya marejea ambapo mama Maria Nyerere hadi sasa bado anaendelea kutumia mbolea ya marejea na mara kwa mara anaagiza vitabu vingi  vinavyozungumzia mbolea ya marejea pamoja na kilimo mseto hivi karibuni amenunua tani mbili za marejea ambazo tumempelekea  nyumbani kwake Butiama”,anasisitiza Mhagama.

Hata hivyo Mhagama anasema  idadi ya watanzania wanaotumia marejea ni wachache kutokana na serikali kutoa uhamasishaji zaidi katika matumizi ya mbolea za viwandani licha ya madhara yanayoletwa na mbolea hizo kwenye udongo.Anawataja watumiaji wakubwa wa marejea kuwa  ni wakulima kutoka nje ya nchi ambapo hapa nchini watumiaji ni vikundi vya wakulima na watu binafsi.

“Serikali kupitia wizara ya chakula na kilimo haijaonyesha ushirikiano na kituo chetu,Baba wa Taifa wakati wa uhai wake alifika hapa na kufurahia kazi inayofanywa na kituo chetu,Mkuu wa mkoa wa zamani na mbunge wa Songea hayati Dk,Lawrence Gama alihamasisha wakulima kutumia marejea,lakini hivi sasa licha ya umuhimu wa marejea hatupati ushirikiano wowote na serikali,wakulima kutoka nchi mbalimbali wanatualika kwenda kutoa elimu ya marejea pia wanaagiza mbegu kutoka hapa ’’,anasisitiza.

Hayati Dk.Gama akiwa mbunge wa Songea mjini mwaka 2001 aliuliza swali  namba 505 katika wizara ya kilimo na chakula kuhusu  mbolea ya marejea Bungeni akitaka serikali isimamie zoezi la uzalishaji na usambazaji wa mbolea hiyo ili watanzania wengi waweze kuitumia katika kilimo badala ya kuendelea na mbolea ya viwandani.

Hata hivyo  mkuu wa mradi wa mbolea ya marejea anasema  pamoja na maelezo mazuri ya ufafanuzi kuhusu uzalishaji na usambazaji wa mbolea hiyo yaliyotolewa katika wizara ya kilimo na chakula mwaka 2001  yakionyesha namna kituo kilivyozalisha na kusambaza mbegu kwa wakulima katika mikoa yote nchini, jambo la kusikitisha tangu wakati huo hadi sasa hakuna ufuatiliaji wowote wala hatua za kuhakikisha wakulima nchini wanahamasishwa kutumia mbolea ya marejea.

“Vikundi mbalimbali vya wakulima ambavyo vimetambua siri ya mbolea ya marejea vimekuwa vinaniita kutoa elimu ya uzalishaji pamoja na kilimo hai kwa mfano juzi nilikuwa mkoani Morogoro kwa siku tisa,mwezi uliopita nilikuwa mkoani Mbeya wilayani Mbozi nikitoa elimu ya marejea kwa wakulima raia wa Uswis waliniita kwa gharama zao, kila mwaka,kila mwezi nakwenda katika mikoa mbalimbali nchini kutoa elimu hii”,anasema Mhagama.

Mtaalamu huyo wa marejea anasema dhana ya kilimo kwanza ambayo inasisitizwa  na Rais Jakaya Kikwete pamoja na waziri mkuu Mizengo Pinda, inaweza kuwa endelevu na kupata mafanikio makubwa endapo watanzania watatumia mbolea ya marejea ambayo inapatikana bure,inazalisha mara dufu  na ni endelevu kwa udongo.

“Nakuomba waziri mkuu Mizengo Pinda utembelee katika kituo chetu za kuzalishia mbolea ya marejea  Peramiho Ruvuma, ikiwezekana nipeni nafasi hata ya nusu saa tu katika Bunge la Muungano ili niweze kutoa elimu hii kwa wabunge wote naamini wabunge watahamasisha wapiga kura wao kuachana na mbolea za viwandani na kuanza kutumia mbolea ya marejea inayotosheleza mahitaji ya wakulima katika nchi nzima”,anasisitiza

Ametoa rai kwa baadhi ya watu wanaodai kuwa mbolea ya marejea haitoshelezi kwa wakulima katika nchi nzima kuwa ni upotoshaji wa makusudi kwa kuwa mbolea hiyo inapatikana kwa wingi ambapo hivi sasa imesambazwa karibu nchi zote za kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na mabara mengine duniani na kwamba watanzania ndiyo wamekuwa nyuma kutumia mbolea hiyo kutokana na upotoshaji licha ya kwamba inazalishwa hapa nchini.

“Mbolea ya samadi ni kweli haiwezi kutosheleza mahitaji ya wakulima katika nchi nzima,lakini mbolea ya marejea inatosheleza kwa mahitaji ya wakulima katika nchi mbalimbali kwa kuwa inazalishwa kwa mbegu kisha kusambazwa kwa wakulima pamoja na kupatiwa elimu ya uzalishaji wa mbegu na matumizi yake’’,anasisitiza.

Hotuba ya msemaji mkuu kambi upinzani wizara ya kilimo,chakula na ushirika Meshack Opulukwa  Bungeni mwaka huu inabainisha kuwa mbolea ya chumvi chumvi ni eneo lenye rushwa na siasa nyingi  hivyo ameishauri wizara ya kilimo kutoa ruzuku kwa mbolea zisizo za kemikali na kuhakikisha kuwa mbolea hizo zinapatikana kwa wingi kwa wakulima badala ya   kutafuta makampuni ya kuleta mbolea za viwandani zenye madhara katika mazingira.

Hotuba hiyo inaitaka serikali kuangalia upya msukumo inaotoa katika matumizi za viwandani ili itoe msukumo kama huo katika kilimo hai hasa katika mikoa ambayo matumizi ya mbolea za  viwandani hazijaanza kuleta madhara kwenye udongo kutokana na ukweli kuwa gharama ya kuihuisha ardhi iliyoharibika kuwa kubwa .

Hata hivyo hotuba hiyo imesisitiza kuwa wizara  ya kilimo bado haijachelewa kwani kilimo hai bado kina nafasi kubwa ya kukifanya kishamiri hapa nchini na kwamba  hivi sasa ni muda muafaka wa kuangalia viwanda vikubwa vya mbolea duniani vinavyofanya biashara ya kuendelea kuzifanya nchi zinaendelea kuwa masikini.

Sera ya Taifa ya mazingira ya mwaka 1997 kuhusu sekta ya kilimo katika kifungu cha 46 inalitaja lengo kuu ni kuhakikisha upatikanaji wa chakula na kuondoa umasikini kwa njia ya uendelezaji wa mifumo ya uzalishaji,teknolojia na shughuli ambazo hazileti madhara kwa mazingira katika kilimo.

Malengo mahususi ambayo yametajwa katika sera hiyo ni kuboresha rutuba ya ardhi,kutilia mkazo uzalishaji wa mazao mbalimbali katika eneo moja,kukuza kilimo cha mseto,ili kuzidisha michakato ya kibiolojia katika ardhi inayilimwa kwa kupanda mazao mchanganyiko,kubadilisha mazao na kilimo misitu.

Waziri wa kilimo ,chakula na ushirika Profesa Jumanne Maghembe akizungumza bungeni Dodoma wakati anafanya majumuisho ya wizara yake mwaka huu alisema hakuna nchi yeyote duniani iliyoweza kufanya mapinduzi ya kijani kwa kutumia mbolea za mboji au samadi ambapo alisisitiza kuwa mapinduzi ya kijani katika kilimo yanaletwa na mbolea za kemikali.

Amesisitiza kuwa sio kweli kwamba mkulima anapotumia mbolea za kemikali kila mwaka anaharibu udongo kwa kuwa nchi ambazo zimefanikiwa kufanya mapinduzi ya kijani katika kilimo ulimwenguni kama vile Marekani ya kaskazini,Ulaya Magharibi na nchi za Asia kama China na India zimetumia mbolea za kemikali kwa miaka mingi.

“Nchi ya Holand imetumia mbolea za kemikali kwa miaka 500 mfululizo na inaendelea kutumia hadi leo lakini inapata mazao mengi kila mwaka na inatumia kilo za naitrojeni 500 kwa hekta na udongo wake kwa miaka 500 sasa haujaharibika,katika Bara la Afrika nchi inayoongoza kwa matumizi makubwa ya mbolea ya kemikali ni Afrika ya kusini inayotumia kilo za naitrojeni 50 kwa hekta,Malawi inatumia  kilo 14 kwa hekta na Tanzania inatumia kilo nane tu kwa hekta,sisi wabunge tuwahimize wananchi wetu kuongeza matumizi ya mbolea za kemikali  ili kuweza kuongeza uzalishaji na kuleta mapinduzi ya kijani’’,alisisitiza.

1 Comment
  • Great!

    I am in need of 10kgs of marejea seeds.

    My Postal address is:

    P.O.Box 723

    Bukoba.

    Let me know in which account can I deposit the price value (including postage): account name and number. Iwill greatiful to receive some information in regard to best application of marejea in maize and vegetable farming.

    Regards

    Mutahyabarwa

    0255754740247

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *