Bajeti yakwamisha malipo ‘baada ya matokeo’ kwa walimu, AZAKI yajitokeza kuwalipa

Jamii Africa
Milola’s new teacher begins lessons by teaching the student’s their ABC’s.

Utulivu na usikivu wa mwanafunzi akiwa darasani ni hatua muhimu ya kupata maarifa kutoka kwa mwalimu anayemfundisha. Lakini  shule zina utaratibu wa kutoa majaribio na mitihani kwa wanafunzi ili kubaini matokeo ya ufundishaji.

Matokeo mazuri ya wanafunzi ni hamasa kwa mwalimu kuendelea kufundisha wanafunzi wake lakini kama wanafunzi hawafikii malengo ya ufaulu yaliyowekwa humuweka mwalimu njiapanda.  Hali hiyo hutegemeana na mazingira yenyewe ya kujifunzia na kufundishia.

Mwalimu akiwekewa mazingira wezeshi uwezekano wa kutimiza majukumu yake ni mkubwa na matokeo ya wanafunzi katika mitihani huwa mazuri. Lakini njia hiyo pekee haiwezi kuleta matokeo mazuri zaidi kama mwalimu hajahamasika na kuwa na hali ya kufundisha.

Kwa kutambua hilo serikali ilianzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa wanafunzi na shule zote za msingi nchini ili zisaidie kutatua changamoto mbalimbali. Mkakati huo wa serikali ulianza 2016 ambapo fedha za ruzuku hupelekwa moja kwa moja katika shule husika. Ni juhudi za kupongezwa ikizingatiwa kuwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa imeongezeka.

Mpango huo unatoa ruzuku ya jumla kwa shule, ambapo huwaacha walimu ambao wanajitolea kufundisha licha ya kuwa mazingira magumu katika shule zao ili kuwasaidia wanafunzi kupata matokeo mazuri ktika mitihani na majaribio ya darasani.

Ni matarajio ya serikali kuwawezesha walimu wote kitaaluma lakini ufinyu wa bajeti hukwamisha mipango ya serikali kumfikia kila mwalimu ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kupata matokeo ya kuridhisha kwa wanafunzi wake.

               Wananchi wakifuatilia utolewa wa ripoti ya utetekelezaji wa mradi wa KiuFunza jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Taasisi ya Twaweza kupitia mradi wa KiuFunza (Kiu ya Kujifunza) ambao unatekelezwa kwa miaka 5 unalenga kumfikia mwalimu mmoja mmoja ambaye anaonyesha juhudi za makusudi kuwafundisha wanafunzi wafikie malengo yao. Mradi huo ni mahususi kutoa motisha ya fedha kwa walimu ambao wanafunzi wao wameonyesha matokeo mazuri katika ufundishaji.

Lengo hasa ni kuongeza ufanisi na hali ya walimu kufundisha ili kupata matokeo mazuri kwa wanafunzi wa shule zilizochaguliwa. Mradi huo unafanyika kwa majaribio katika shule 67 kwenye Wilaya 11 za Geita, Kahama, Karagwe, Kigoma, Kinondoni, Kondoa, Korogwe Vijijini, Lushoto, Mbozi, Sumbawanga Vijijini na Mbinga.

Katika kipindi cha 2015-2016 mradi huo ulianzisha kipengeleza cha mashindano ya wanafunzi ili kupima uelewa wao wakiwa darasani. Wanafunzi waliohusika ni wale wa darasa la I, II, III hasa katika masomo ya Kiswahili na hesabu.

Kuanzishwa kwa mradi huu kunatokana na utafiti uliofanywa na Twaweza mwaka 2013 na kubaini kuwa, “katika mfumo uliopo hivi sasa hakuna uwajibikaji wa kutosha katika suala la ujifunzaji. Zaidi ya hapo, malipo kwa wasimamizi na walimu hayategemei utendaji wao. Kutokutilia maanani suala la utendaji na motisha inaweza kwa kiwango fulani kuonyesha ni kwanini ongezeko la bajeti ya elimu haichangii kuboresha matokeo ya ujifunzaji”,

Mradi uliweka mkakati ambao unamuwezesha mwalimu kupata kiasi fulani cha fedha ikiwa wanafunzi wake wameonyesha matokeo mazuri katika mashindano ya kupima uelewa.

Ripoti ya mradi wa KiuFunza inaeleza kuwa, “malipo kwa utendaji bora (mashindano) hutumia vipimo viwili kwa kila mwanafunzi. Kwanza hupima kiwango alichopo mwanafunzi mwanzoni mwa mwaka na pili hupima kiwango alichofikia mwishoni mwa mwaka,

Matokeo ya kwanza hutumika kuwaweka watoto kwenye makundi kutokana na uwezo wao. Kila kundi huwekwa wanafunzi wenye uwezo unaofanana. Makundi hayo ndiyo msingi wa mashindano kwa walimu. Wanafunzi kwenye kila kundi ambaye atafaulu kwa kiwango cha juu kwenye jaribio la pili atampatia mwalimu wake bahshishi kubwa”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema baada ya mwaka mmoja walibaini matokeo chanya ya utolewaji wa motisha kwa walimu ambapo kiwango cha ujifunzaji kiliongezeka ikilinganishwa na kipindi ambapo motisha ilikuwa haitolewi.

“Matokeo ya kujifunza katika madarasa ya I, II, III, yalikuwa mazuri; tulibaini kuwa viwango vya ufaulu wa Kiswahili na Hesabu viliongezeka kwa asilimia 20 katika kipindi cha mwaka mmoja”, anasema Eyakuze na kuongeza kuwa,

“Motisha kwa walimu inaweza kuwa na matokeo chanya ya kuwavutia watu wenye vipaji/uwezo kuwa walimu”.

 

Mafaniko yaliyopatikana katika nchi zingine

Mradi wa majaribio wa KiuFunza uliwahi kutekelezwa katika nchi ya Brazil hasa jimbo la Pernambuco, ambapo  mpango wa motisha uliwafikia walimu 50,000 katika shule 950 na kuleta matokeo chanya.  Pia nchi ya Chile ilifanikiwa kutoa matisha kwa  walimu baada ya kupata matokeo mazuri kwa shule zote za msingi 6,500 zinazoendeshwa na serikali zilishiriki katika mradi wa majaribio ya hisabati na lugha.

 

Changamoto ya kutoa motisha ya fedha kwa walimu

Kulingana na tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa mpango huu wa motisha kwa walimu haujafanikiwa katika baadhi ya nchi kama Kenya, India na Israel kwasababu motisha ilikuwa kidogo kinyume na matarajio ya walimu.

Mwalimu Joseph Mbando mmoja wa watafiti wa mradi wa KiuFunza anasema changamoto iliyopo kwa serikali ya Tanzania kutoa motisha kwa walimu ni ufinyu wa bajeti inayoelekezwa katika sekta ya elimu kila mwaka.

“Bahshishi za KiuFunza ambazo zililipwa kwa walimu wa madarasa ya I, II na III pekee, ilikuwa ni karibu asilimia 3 ya bajeti ya sasa kwa kila shule”, ameeleza Mwalimu Mbando.

Kwa upande wake, Prof.  Marjorie Mbilinyi mwanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) amesema utafiti huo wa Twaweza umeangazia suala la msingi lakini wanapaswa kuangalia motisha zingine ikiwemo kutoa mafunzo na kuwatambua walimu kwa kazi zao.

Pia ameshauri  juhudi hizo zilenge kutathmini mazingira ya kufundishia na kuhimiza serikali kuboresha miundombinu ya shule na nyumba za walimu ili kuongeza hali na bidii ya kufanya kazi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *