Watoto wachanga 5,995 kuzaliwa mwaka mpya nchini Tanzania, asilimia 37.3 hufariki kabla ya kutimiza mwezi mmoja

Jamii Africa

Inakadiliwa kuwa watoto wachanga 5,995 wamezaliwa katika siku ya mwaka mpya wa 2018 nchini Tanzania lakini asilimia 60 ya watoto hao hufariki kabla ya kutimiza mwaka mmoja wa kwao.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) ya mwaka 2018 inaeleza kuwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika zinaongoza duniani kuwa na idadi kubwa ya watoto waliozaliwa siku ya kwanza ya mwaka mpya.

“Watoto waliozaliwa Mashariki na Kusini mwa Afrika watakuwa sawa na asilimia 12 ya watoto wachanga wanaokadiriwa kufika 386,000 watakaozaliwa kote Duniani katika Siku ya Mwaka Mpya”, inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaiweka Tanzania katika nafasi ya pili kuwa na watoto wengi waliozaliwa siku ya mwaka mpya baada ya Ethiopia na kufuatiwa na nchi za Uganda, Kenya na Angola.

“Takribani asilimia 58 ya vizazi hivi vitatokea katika nchi tano katika kanda hii, huku idadi ya juu zaidi ya vizazi hivi katika Siku ya Mwaka Mpya ikikadiriwa kuwa: Ethiopia 9,023, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (5,995), Uganda (4,953), Kenya (4,237) na Angola (3,417)”, inafafanua taarifa hiyo.

Idadi hiyo ya watoto wanaozaliwa itaendelea kuongezeka kila mwaka ambapo kufikia 2050 watoto bilioni 1.8 watazaliwa barani Afrika, hii ni zaidi ya ongezeko la watoto milioni 700 katika wale waliozaliwa ndani ya miaka 35 iliyopita kutoka 1980 hadi 2014.

Hata hivyo, matumaini ya watoto hao kuishi zaidi ya miaka mitano hufifia kwasababu ya kufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano kutokana na huduma duni za afya ya mama na mtoto katika maeneo mengi ya Afrika.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, “Takribani watoto 270 wenye umri chini ya miaka mitano hufa kila siku nchini Tanzania, na hasa kutokana na vyanzo vinavyoweza kuzuilika kama vile malaria, ugonjwa wa mapafu, na kuhara. Asilimia 60 ya vifo hivi hutokea ndani ya mwaka wa kwanza wa kuzaliwa”, na kuongeza kuwa,

“Kadhalika, mwezi wa kwanza wa kuzaliwa bado umeendelea kuwa na changamoto kubwa ambapo asilimia 37.3 ya vifo vya watoto wachanga wenye umri chini ya miaka mitano hutokea ndani ya mwezi wa kwanza wa kuzaliwa”.

 

Chanzo cha vifo vya watoto wachanga

Vifo vya watoto wachanga husababishwa na vyanzo vinavyozuilika na kutibika kama vile kuzaliwa njiti (kabla ya muda), matatizo wakati wa uzazi, maambukizi kama vile bacteria na homa ya mapafu.

Mwaka 2016 pekee, nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, zilichangia asilimia 38 ya vifo vyote vya watoto wachanga. Licha ya hatua kubwa zilizopigwa kuokoa maisha ya watoto barani humo, vifo vya watoto bado viko juu na kuna changamoto kubwa za kuzikabili ili kutoa nafasi kwa vizazi vinavyobashiriwa na kuzuia nchi zenye viwango vya juu vya kuzaliana kutokuwa chini zaidi ya vigezo vya kimataifa vya matunzo ya akina mama, watoto wachanga na watoto.

 

Mikakati ya kuokoa maisha ya watoto wachanga

Katika miongo miwili iliyopita, kumekuwa na maendeleo makubwa duniani katika kuokoa maisha ya mtoto, ambapo idadi ya vifo vya watoto kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano imepungua kwa nusu hadi kufikia milioni 5.6 katika mwaka 2016.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania amesema watoto wa Tanzania wana nafasi kubwa zaidi kuishi kuliko wakati mwingine wowote baada ya kutimiza umri wa miaka mitano kutokana na hatua kubwa iliyopigwa na serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto.

“Utekelezaji unaofanywa na serikali wa program za afya zenye matokeo makubwa kama vile utoaji wa mara kwa mara wa chanjo, nyongeza ya Vitamini A, kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kuimarisha udhibiti magonjwa yanayowaandama zaidi watoto, umesaidia kuokoa maisha ya watoto kote nchini”, amesema Zaman na kubainisha kuwa,

“Lengo letu la pamoja ni kuimarisha jitihada na kumfikia kila mama, kila mtoto mchanga na kuwapa huduma bora ya afya,”  

Mikakati hiyo itahakikisha kwamba watoto wanazaliwa katika mikono ya wataalamu na akina mama wanapata matunzo ya kutosha na kamilifu kabla, wakati na baada ya kujifungua.

 

Kampeni ya ‘Kila Mtoto Aishi’

Mwezi Februari mwaka huu, UNICEF itazindua kampeni ya ‘Every Child Alive’ (Kila Mtoto Aishi) ambayo inahimiza upatikanaji wa ufumbuzi wa matunzo ya gharama nafuu na bora ya afya kwa kila mama na mtoto mchanga.

Ufumbuzi huu ni pamoja na upatikanaji kwa uhakika wa maji safi na salama na umeme katika vituo vya afya, uwepo wa mhudumu wa afya mwenye mafunzo wakati wa mtoto kuzaliwa.  Kuzuia maambukizi katika kitovu, kunyonyesha mtoto ndani ya saa la kwanza mara baada ya kujifungua, mtoto kuwa karibu na mama yake kiasi cha kugusana, yaani mama kumkumbatia mtoto wake.

 

Wito kwa jamii

“Katika Mwaka huu Mpya, azimio la UNICEF ni kusaidia kumpa kila mtoto zaidi ya saa moja, zaidi ya siku moja, zaidi ya mwezi mmoja wa kuishi,” amesema Leila Pakkala, Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Tunatoa wito kwa serikali na washirika kuendeleza na kupanua juhudi zao ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto kwa kuleta ufumbuzi uliothibitishwa na wenye gharama ndogo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *