SIKU YA WANAWAKE DUNIANI : Wadau watoa mwelekeo mpya kuimarisha usawa wa kijinsia

Jamii Africa

Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanamke ambayo hutoa nafasi ya kutathmini changamoto na mafanikio yaliyofikiwa katika kutambua haki za wanawake na mchango walionao katika maendeleo ya dunia.

Siku ya Wanawake Duniani iliridhiwa na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1975 na kuanza kuadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka ikiwa na lengo la kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake na umuhimu wa kuheshimu usawa wa kijinsia.

 Uamuzi huo ulikuwa ni matokeo ya kuimarika kwa mfumo dume katika jamii mbalimbali ulimwenguni ambapo uliwakandamiza wanawake na kuwanyima fursa ya kupata maendeleo endelevu. Tangu wakati huo harakati na kampeni mbalimbali zimekuwa zikiratibiwa kuilemisha jamii kuheshimu na kulinda haki na usawa wa kijinsia kwa watu wote.

Umoja wa Mataifa kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) inasisitiza usawa wa kijinsia na unazitaka nchi wahisani kupitia taasisi zake za utendaji kuwahusisha wanawake katika utekelezaji wa sera, mipango na maadhimio muhimu ya kijamii na kitaifa ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uendelezaji wa rasilimali za taifa.

Maazimio ya UN yanatokana na ukweli kwamba bado wanawake na wasichana katika maeneo mbalimbali duniani wananyanyasika na kunyimwa haki zao za msingi na fursa muhimu kujiletea maendeleo.

Takwimu za SDG’s (2015) zinaonesha kuwa tangu mwaka 2005 hadi 2016 katika nchi 87, asilimia 19 ya wanawake walio na umri miaka 15 na 49 waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kupigwa au ngono na waume zao. Mwaka 2012 pekee karibu nusu ya wanawake ambao walikuwa waathirika wa mauaji ya kimataifa waliuawa na ndugu zao wa karibu ukilinganisha na asilimia 6 ya waathirika wa kiume.

Inaelezwa kuwa bado wanawake wengi wanatumikishwa kwenye kazi ngumu na kulipwa ujira mdogo. Takwimu hizo zinaeleza kuwa wastani wa muda anaotumia mwanamke katika kazi za nyumbani na kutunza watoto ni mara tatu zaidi ya mwanaume. Muda huo unaotumiwa na wanawake katika shughuli za nyumbani unazidisha pengo la kijinsia na kuwakosesha wanawake mapato kwa ajili ya maendeleo yao.

Duniani kote uwakilishi wa mwanamke katika safu za uongozi na maumuzi bado uko chini ambapo kwa mwaka 2017 uwakilishi huo kwenye mabunge ya nchi ulikuwa ni asilimia 23.4 juu kidogo ya asilimia 10 mwaka 2000.

Hata kwenye nafasi za juu uongozi wa mashirika ya umma na binafsi  bado wanawake hawana uwakilishi mzuri. Katika nchi 67 zilizokuwa na data tangu mwaka 2009 hadi 2015, pungufu ya theluth moja (1/3) ya nafasi za wakurugenzi na meneja zilishikiliwa na wanawake.

Kwa tathmini hiyo juu ya hali ya wanawake duniani katika baadhi ya sekta, utagundua kuna umuhimu wa kuongeza msukumo wa kisiasa na kisheria wa kupambana na mifumo inayomkandamiza mwanamke na kuhimiza usawa katika matumizi ya rasilimali za nchi.

 

Taasisi na Wadau watoa mwelekeo mpya

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga amesema katika taarifa yake kuwa wakati dunia inasheherekea siku ya Wanawake inapaswa kutafakari vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa wanawake na kuungana kwa pamoja kupinga unyanyasaji wa aina zote kwa wanawake.

Amesema jamii inatumia muda mwingi kushughulikia kesi za ukatili badala ya kufanya shughuli za maendeleo ili kuinua uchumi.

“Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Pilisi nchini, makosa ya ubakaji na kunajisi yaliyoripotiwa yameongezeka kutoka 6,985 Novemba mwaka 2016 mpaka 7,460 mwaka 2017, ukatili unawakumba hasa wanawake na watoto na kuzorotesha ukuaji wa maendeleo kiuchumi kwani jamii inatumia muda mwingi kufuatilia kesi za ukatili wa kijinsia badala ya kufanya shughuli za maendeleo kuinua uchumi”, imeeleza ripiti hiyo ya Edda Sanga.

Amebainisha kuwa siku ya leo iwe mahususi, “kuwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za kimataifa, kikanda na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake katika kuhakikisha haki za wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa zinapatikana na kulindwa”.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika taarifa yake kimesema kitaendelea kupambana na mitazama hasi juu ya wanawake kwa kutoa elimu juu ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia kwa umma na kuwawezesha moja kwa moja wanawake kutekeleza majukumu yao kwa misingi ya haki na usawa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile amesema tangu ulipofanyika Mkutano wa Wanawake wa Beijing mwaka 1995  maendeleo mengi yametokea ambapo kabla ya mwaka 1995 wanawake wa Tanzania walikuwa hawamiliki mali kutokana na sheria iliyokuwepo lakini wakati huu wamewezeshwa na wanaonekana kwenye safu za uongozi, ujasiriamali, biashara na hata kumiliki mali.

Amewata wanawake watambue nafasi waliyonayo katika sheria za nchi  na kuzitumia vizuri katika kupata haki zao za msingi ikiwemo umiliki wa mali ili kuwaongezea nguvu za kiuchumi zitakazowasaidia kuboresha maisha ya familia zao.

“Kikubwa kama Chama cha Wanasheria tumejaribu kuhamasisha jamii hasa wanaume kuandika wosia kuhakikisha wanawake, waume zao wanapofariki wanaweza kuzipata haki zao vizuri. Lakini tumejaribu kuongea na wanawake ambao wako katika ndoa kuhakikisha wanapofanya manunuzi ya kitu chochote kinachohusiana na familia kama kujenga nyumba, wanavyonunua magari wanaweka majina yao mawili kwa pamoja”, amesema Tike na kuongeza kuwa,

“Changamoto ziko nyingi lakini ushauri tumekuwa tukiotoa kwa wanawake kwamba mwisho wa siku haki zao waweze kuzipata”.

Kauli mbiu ya ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu ni "Wakati ni sasa: Wanaharakati Mijini na Vijijini kubadilisha maisha ya wanawake".

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *