HUWEZI kuzungumzia historia ya Uhuru wa Msumbiji pasipo kutaja eneo la Mkenda lililopo Kijiji cha Nakawale Kata ya Muhukuru mkoani Ruvuma.
Eneo hilo lililopo kiasi cha kilometa 124 kutoka Songea mjini kwa kizazi kipya ni eneo ambalo huenda likaonekana halina umuhimu wowote ule, lakini kwa wazee wanaofuatilia historia za majirani wa Tanzania ni kijiji chenye historia iliyozama katika vichwa.
Pengine ni kutokana na ukweli huo kijiji ncha jirani mara tu ukivuka mpaka wa Tanzania na |msumbiji kuna hifadhi nzuri inayoelezea mipango ya kwanza ya mashambulio dhdii ya Wareno kutokea mto Ruvuma.
Kwa namna yoyote ile eneo hilo ambalo ni kitongoji ni muhimu katika historia ya Msumbiji na hata Tanzania lakini ukiachia mbali maelezo ya wakazi wenye umri mkubwa hakuna jitihada zozote zinazoonekana kufanywa kuhifadhi historia mwanana katika ukuombozi wa Afrika hasa taifa la Msumbiji.
Hili ni eneo ambalo wapigania uhuru wa Msumbiji waliokuwa wakiongozwa na Rais wa chama cha Frelimo wakati huo miaka ya 1960 Eduardo Mondrane, walipoanzia safari yao yenye furaha na majonzi papo hapo, safari ya kwenda kuanza mapambano ya kumng’oa Mreno.
Inaelezwa na wakazi wa eneo hilo kuwa hapo ndipo wapigania uhuru wa Msumbiji katika miaka ya 1968 wakiongozwa na Rais wa chama cha Frelimo Eduardo Mondlane na mkuu wa majeshi Samora MaChel waliweka kambi kabla ya kuingia eneo la Congreso.
Ilibidi wafanye kituo hapa kujipanga na kutuma watu wa mwanzo kuangalia mahali ambapo walikuwa watengeneze kambi nyingine ya kujipanga wakati wa kusubiri kuanza kwa mashambulio.
Ilikuwa ni kazi kubwa lakini, viongozi ambao ndio wapiganishaji walikuwa na muda mwingi wa kuchora namna watakavyoendesha vita ya Msumbiji na mahali pa kujihami baada ya mapigano ya mwanzo.
Pamoja na kwamba kwa sasa kuna daraja la Mkenda linalounga Tanzania kwa upande wa Songea na Congress kwa upande wa Msumbiji, Mkenda yenyewe imebaki ‘mahame’ katika historia kwani siku zinavyoenda, simulizi zinavyozidi kuchakachuliwa eneo hilo linabaki katika roho za waliokumbana na kashkash ya kwanza ya vita vya Msumbiji na kizazi kipya hakina cha kufanya.
Ukivuka Mkenda na kuingia Msumbiji , hali ni tofauti sana.Wao wameweka kumbukumbu za tukio la siku ya kwanza baada ya kuvuka mto Ruvuma.Katika eneo hilo la Congreso zipo mpaka nyumba zilizokuwa zikitumika kulala viongozi mbalimbali pamoja na magogo waliyokuwa wakikalia wakati wa mikutano ya kwanza ya mipango vita.
Alexandre Jalarne mtunza makumbusho hayo ya Taifa ya Msumbiji katika eneo la Congresso akielezea kwa maringo na kujiamini alisema kuwa viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi hiyo wamekuwa wakifika katika makumbusho hayo kwa ajili ya kuangalia kumbukumbu mbalimbali zilizohifadhiwa kiasili.
Lakini watu hawa hawapati ulazima wa kuvuka mpaka kuja Tanzania hasa kutokana na kwamba hakuna mahali pa kuona wapi akina Machel walikuwapo kabla ya kuvuka mipaka na kuingia Msumbiji kuanza kazi ya kumkabili Mreno.
Hali ya eneo hilo haijabughudhiwa ukiiangalia kwa makini, kwani hata mtu wa kawaida ukifika hapo unaweza kabisa ‘kunusa’ kwa kutumia akili uwepo wa majemedari hao wa zamani wakati wakipanga fyeko la kwanza kwa Wareno.
Katika mazungumzo kuelewa siri ya eneo hilo kubaki bado na harufu ya majemedari hao pamoja na miaka mingi kupita,Jalarne alisema kuwa kinachosaidia eneo hilo kubakia katika hali ya uhalisia ni jinsi wananchi wa nchi hiyo wanavyoheshimu na kuogopa sheria za nchi hiyo ambazo ni kali.
‘’ Sheria zetu ni kali sana katika uhifadhi wa mali asili, tena unaweza kujikuta umehukumiwa kunyongwa kama utabainika kukata miti katika hifadhi kama hizi, ndio maana unaona miti inaanguka yenyewe na hakuna hata mtu wa kukata kuni’’ Alisema.
Alisema kuwa Wapigania uhuru wa Msumbiji walifanya mkutano wao wa kwanza Juni 22 hadi 25 mwaka 62 mkutano wa kujadili jinsi ya kupata uhuru mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Mtunza makumbusho huyo alisema kuwa ilipofika mwaka 1968 wapigania uhuru wa nchi hiyo walifika katika kijiji cha Mkenda na kuweka kambi kabla ya kuingia Congreso kwa ajili ya kufanya mkutano wake wa pili kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda kutafuta Uhuru wao nchini Msumbiji.
Ukiangalia kwa undani zaidi utaona kuwa Eneo la Mkenda lingeweza kuwekwa kumbukumbu ya kitaifa kutokana na historia hiyo muhimu kabla Msumbiji haijapata uhuru wake mwaka 1975.
Pamoja na kubeba historia kubwa ya nchi jirani na kujitolea kwa watanzania kupitia wakazi wake wa Mkenda na jirani eneo hili halina hata chembe ya ukubwa wa historia yake katika vichwa vya wapigania uhuru na hata haow alioshiriki katika mapambano hayo.
Hata hivyo, historia hiyo ambayo ilistahili kufanyiwa kazi na kuenziwa inakwamba zaidi kutokana na eneo hilo kutoendelezwa kwa namna yeyote . Ukifika eneo hili miundombinu yake ni duni, mawasiliano hakuna jambo linalowalazimu wananchi wa eneo hilo kutumia mtandao wa simu wa nchini msumbiji.
Mwalimu Salvius Nindi ni miongoni mwa wakazi wa kitongoji cha Mkenda anasema ni kama vile wako katika kisiwa kutokana na kutokuwa na huduma muhimu kama mawasiliano na miundombinu mibovu hasa ya barabara.
Hali hiyo huenda ndiyo inayofanya hata watu kutoka Msumbiji wenye hamu ya kuja kuangalia mwanzo wa harakati hizo kushindwa kufanya hivyo.
Kuwepo kwa makumbusho eneo hilo ambayo yanaweza kuungwa na mapambano ya wana Frelimo kumng’oa Mreno kwa kuunganisha na maeneo mengine kama makazi ya Mondlane yaliyopo wilaya ya Temeke, Dar es salaam, kambi za kufunza wapiganaji za Nachingwea .
Hali hiyo ingeliwezesha watanzania nao kuuona ushiriki wao katika kumng’oa Mreno.
Na kwa kuweka makumbusho na kuboresha miundombinu katika maeneo hayo nchi ingeweza kujipatia pato kubwa la taifa kutokana wananchi wengi wa Msumbiji kufuatilia historia yao ambapo wangelifika Mkenda na maeneo mengine yaliyoungwa katika njia ya mapambano ya uhuru wa Msumbiji.
‘’ Kungekuwa na makumbusho ya Taifa hapa serikali ingeweza kupata fedha nyingi, si mnaona mimi nilijenga nyumba ya kulala wageni na sasa najenga nyumba ya kitalii, kama serikali ingewekeza ingepata pato kubwa’’ alisema Mwalimu huyo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Saidi Mwambungu yeye alisema kuwa serikali inafanya jitiada za kuboresha miundombinu katika maeneo yote yenye vivutio vya utalii ili kuweza kuwavutia watalii.
Alisema kuwa tayari serikali imejenga daraja kubwa la Mkenda linalounganisha nchi hizo mbili lengo likiwa ni kurahisha mawasiliano na pia kuunga udugu wa nchi hizi mbili ulioanzia katika mapambano ya kudai uhuru wa Msumbiji.
Pamoja na kukiri kwamba taifa limechelewa sana kufikiria kuunganisha makumbusho ya Msumbiji na Mkenda kwa ajili ya majukumu ya kutoa simulizi la kweli la historia ya maeneo hayo katika kudai Uhuru wa Msumbiji, bado masuala hayo yanaweza kufanyiwa kazi na Makumbusho ya taifa na hivyo kuunga makumbusho ya Mkenda na yale ya Congress.