Licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutoa kauli ya kibaguzi dhidi ya nchi za Afrika, inaelezwa kuwa bado wananchi wa bara hilo wanaukubali uongozi wa rais huyo.
Wakati akiingia madarakani mwaka 2016, Rais Trump aliahidi kutekeleza sera za kimataifa za kujitenga na kutanguliza maslahi ya Marekani mbele ambapo siku chache zilizopita alishangaa Marekani kupokea wahamiaji kutoka katika nchi za Afrika huku akitumia neno ‘shithole’ (tundu la choo) akimaanisha ni nchi za Afrika Haiti na El Salvador na kwamba Marekani haihitaji wahamiaji kutoka katika nchi hizo, badala yake inataka wahamiaji kutoka Norway.
Dunia imesimama na kupinga sera za Trump na kuitaka Marekani kuheshimu misingi ya demokrasia ili kudumisha diplomasia na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Kura ya maoni iliyoratibiwa na mtandao wa Gallup (2018) inaonyesha nchi za Afrika zina ukubali kwa asilimia 51 utawala wa Marekani unaongozwa na Rais Trump dhidi ya asilimia 20 ambao hawaukubali.
Hata hivyo, kukubalika kwa utawala wa Marekani kumeshuka kwa asilimia 10 katika nchi 11 za Afrika na inatabiriwa kuwa kukubalika huko kutashuka zaidi siku zijazo ikiwa Trump ataendelea kutekeleza sera za kibaguzi dhidi ya mataifa ya Afrika.
Kura hiyo ambayo ilishirikisha watu 1,000 kutoka nchi 134 ili kufahamu maoni yao juu ya utawala wa Ujerumani, Marekani, Urusi na China, ilibaini kuwa kukubalika kwa Marekani chini ya Trump kumeshuka kwa pointi 18 ukilinganisha na uongozi wa Barack Obama. Trump alipata asilimia 43 nyuma ya uongozi wa Vladimir Putini wa Urusi na Xi Jinping wa China.
Sababu kubwa ya Trump kutokukubalika ni hatua yake ya kuimarisha mahusiano na Israel ukilinganisha mtangulizi wake Obama ambaye hakuonyesha waziwazi kuisaidia nchi hiyo. Ikumbukwe kuwa Trump alikuwa Rais wa kwanza kulitambua jiji la Yerusalemu kuwa mji mkuu wa Israeli na kutangaza kuhamishia ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi katika jiji hilo.
Rais Donald Trump wa Marekani (katikati) akiteta jambo na rais wa Urusi, Vladimir Putin (kushoto)
Maamuzi hayo ya Trump yaliukasirisha ulimwengu kwasababu Yerusalemu imekuwa na mgogoro wa kisiasa kutoka kwa Palestina na Israeli ambapo kila nchi inadai kuwa jiji hilo ni makao makuu yake.
Trump ameendelea kupingwa hata ndani ya Marekani, Gallup inaonyesha umaarufu wake umeshuka kutoka asilimia 49 mwaka 2016 hadi 20% mwaka 2017. Pia kukubalika kwa Marekani kwa nchi za Ulaya pia kumeshuka baada ya Trump kubariki uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya na kupinga vikali Marekani kuwa mfadhili mkuu wa Shirika la NATO. Ni asilimia 25 tu ya wananchi wa Ulaya ndio wanaikubali Marekani ikilinganishwa na 44% ya mwaka 2016.
Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) tayari wamelaani sera za Trump na kumtaka kuheshimu jumuiya za kimataifa katika kudumisha diplomasia na amani ya dunia.