DPP anyang’anywa mamlaka ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa

Jamii Africa
DR CONGO: Padri wa Kanisa Katoliki, amekamatwa na Askari wa Polisi baada ya kumalizika kwa misa aliyokuwa akiiongoza - Serikali na Kanisa hilo nchini humo wako katika mzozo kutokana na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo kuhamasisha maandamano ya kumpinga Rais Kabila - Rais Kabila(46) amekuwa madarakani toka mwaka 2001 huku Serikali yake ikikosolewa kwa ufisadi, ukandamizaji wa Haki za Binadamu na uzembe. - Aidha, muda wa kukaa madarakani kwa Rais huyo ulimalizika Desemba mwaka 2016 kwa mujibu wa Katiba lakini ameendelea kubakia madarakani hali ambayo inasababisha umwagikaji damu katika Jamhuri ya Kidemokrasia Ya Kongo

Mahamaka ya Rufani imemwondolea Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kisheria ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa wa makosa mbalimbali kabla ya kesi zao kutolewa uamuzi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Wakili wa Kujitegemea, Jeremiah Mtobesya kufungua kesi ya kikatiba  kwenye Mahakama Kuu kupinga kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinampa mamlaka DPP ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa bila kutoa sababu.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2015,  Mtobesya alidai kuwa kifungo hicho kinavunja Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Ibara ya 13(a) ambayo inatoa haki kwa mshtakiwa kusikilizwa na kupewa nafuu za kisheria kabla ya hukumu kutolewa.

Disemba 22 Mwaka 2015, Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika Kesi ya Kikatiba Na 29 /2015, Shabani Lila ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa, Kihiyo na Ruhangisa ambaye alistaafu Ujaji kwa hiari mwaka 2017, ambapo jopo hilo lilikubaliana na hoja za mlalamikaji Mtobesya kuwa Kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinakwenda kinyume na Ibara hiyo ya Katiba ya nchi.

Ibara ya 13(a) ya Katiba ya Tanzania inaeleza, “Wakati Haki na wajibu kwa mtu yeyote inapohitajika kufanyiwa maamuzi na Mahakama au chombo kingine chochote kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na Haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia Haki ya kukata Rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya Mahakama au Chombo hicho kingine kinachohusika

Hata hivyo, mwaka 2016, Mwanasheria Mkuu wa serikali alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani nchini na kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu akiomba utenguliwe  kwasababu nne ambazo miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Mahakama ilikosea kusema hati ya kufunga dhamana ya mshitakiwa inayowasilishwa mahakamani na DPP inamnyima mshitakiwa haki ya kuipinga hati hiyo katika chombo kingine.

Kesi hiyo iliendelea kusikilizwa kwa zaidi ya mwaka mmoja ambapo Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali hoja za Mwanasheria Mkuu wa serikali na kuupa ushindi upande wa mlalamikiwa ambaye alitumia haki yake kulinda katiba.

Kwa Mujibu wa hati yake ya Madai iliyoambatanishwa na kiapo Chake Juni 30 mwaka 2015 Mutobesya alidai kuwa Ibara 26(2) ya Katiba ya nchi inasema;"Kila mtu ana Haki , kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria, kuchukua Hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi".

Mahakama ya Rufani kupitia nakala ya hukumu  iliyosainiwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, John Kahyoza, Januari 31 Mwaka huu, inasema jopo la Majaji 5 walioketi Dar es Salaam wakiongozwa na Jaji Bernard Luanda wamesisitiza kuwa Kifungu 148(4) cha CPA kinakwenda kinyume na Ibara ya 13 (6)(a) ya Katiba ya nchi.

Hukumu ya kesi inapatikana hapa – AG vs. MTOBESYA, Civil Appeal No. 65 of 2016 (CA at Dar es Salaam)

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania (2015) ilipendekeza kumwondolea Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kuzuia Mahakama na Polisi kutoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa sababu ya usalama au maslahi ya Jamhuri lakini mamlaka hiyo imeendelea kutumika.

 

Watu walionyimwa dhamana kwa amri ya DPP

Ofisi ya DPP imekuwa ikitumia kifungu cha 184 (4) cha CPA kuzuia dhamana kwa baadhi ya washtakiwa wakiwemo wanasiasa ambao wamekuwa wakituhumiwa kutoa kauli za kichochezi.

Mwaka 2016, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alinyimwa dhamana zaidi ya mara tatu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akishtakiwa kwa makosa ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Mnamo mwaka 2015, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Sheikh Issa Ponda alinyimwa dhamana na Mhakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro wakati anakabiliwa na kesi ya uchochezi.

Kwa mujibu wa Mahakama hiyo ilisema kuwa DPP aliwasilisha hati ya zuio la dhamana na kwamba hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutengua hati hiyo mpaka kesi ilipomalizika.

Hata hivyo, hukumu hiyo inaibua changamoto ya mgongano wa kisheria ambapo ili kukidhi mahitaji ya kikatiba, sheria hiyo inaweza kufanyiwa mabadiliko?

 

Lema anena

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, “Wakili Jeremiah Mtobesya amefanya kazi nzuri. Kwa watu waliopita magereza na kwenye mashauri mbali mbali mahakamani watakubaliana na mimi kuwa kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai. kilitumika kukandamiza haki kwa washitakiwa kwa nyakati nyingi tofauti”.

Kwa upande wake, Irenei Kiria ameandika “Nadhani kuna watu wako rumande kufuatia DPP kuzuia dhamana. Mahakama ya Rufaa imeamua 31.01.2018 kuwa mamlaka hayo ya DPP (Section 148.4 of the CPA) ni kinyume na Katiba, ni batili. Tusome hii hukumu ni tamu sana”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *