Mbunge wa CCM Busega kuunganishwa kesi ya njama za mauaji ya aliyekuwa Mbunge?

Jamii Africa

HATIMAYE tuhuma nzito zinazomkabili Mbunge wa Jimbo la Busega Wilayani Magu mkoani Mwanza, Dk. Titus Kamani (CCM), za kula njama kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni (CCM), zimewasilishwa rasmi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa hatua zaidi za kisheria.

Taarifa za kiuchunguzi zinaeleza kwamba, kuwasilishwa kwa DPP jalada hilo la tuhuma za jinai dhidi ya mbunge Kamani, ni hatua muhimu ya kuanza kushughulikiwa kisheria.

Habari hizo zilizothibitishwa na ofisi ya mwanasheria wa Serikali Kanda ya Mwanza, zinaeleza kuwa jalada la tuhuma hizo dhidi ya Dk. Kamani ziliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka hivi karibuni, na kwamba huenda mbunge huyo akaunganishwa mahakamani na watuhumiwa wenzake wanne, Desemba 20 mwaka huu, siku ya kutajwa tena kesi hiyo.

Watuhumiwa wengine wa kesi hiyo ambao tayari walishafikishwa mahakamani ni Dismas Zacharia Ndaki, Erasto Kazimili Kombe, Queen Joseph Bogohe na Ellen Joseph Bogohe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa (CCM), mkoa wa Mwanza.

Kaimu mwanasheria wa Serikali Kanda ya Mwanza, Seth Mkemwa alithibitisha jana ofisini kwake, na kusema kwamba, tayari ofisi yake ilishapeleka jalada la tuhuma za mbunge huyo kwa DPP kwa hatua zaidi za kisheria.

“Ni kweli hili jalada la tuhuma za mheshimiwa Mbunge wa Busega tulishalipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tunatarajia DPP atalituma jalada hilo Mwanza kabla ya Desemba 20 mwaka huu. Na sisi tutafuata maelekezo, kama atatakiwa kufikishwa mahakamani tutamuunganisha na wenzake wanne hapo Desemba 20”, alisema Mkemwa na kuongeza

“Katika hili tunaweza kumuita mheshimiwa mahakamani kwa njia ya Samasi, kufuatwa na polisi popote alipo iwapo atakaidi amri au kuitwa hata kwa njia ya simu. Ngoja lirudi jalada halafu tuone nini cha kufanya”.

Mbunge huyo wa Jimbo la Busega, Dk. Kamani anatuhumiwa kula njama za kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Chegeni miezi ya mwanzoni mwa mwaka huu, na kwamba upo huenda kiongozi huyo akafikishwa mahakamani kuhusiana na tuhuma hizo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mei 31 mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani hapa liliiandikia barua Ofisi ya Bunge kumwamuru haraka Dk. Kamani kuja Mwanza kwa ajili ya mahojiano maalumu na polisi juu ya tuhuma hizo za jinai, ambazo ametajwa kuhusika kutaka kumuua Dk. Chegeni.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya jeshi la polisi, yenye kumbukumbu No. MZR/CID/SCR/105/2011/4 iliyotumwa kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri, ikimtaka Dk. Kamani kuja kutoa maelezo polisi katika Jalada No. MW/IR/2607/2011-MR-CC.28/2011 lililofunguliwa kwa kosa la kula njama za kuua.

Iwapo mbunge huyo wa Busega, Dk. Kamani atafikishwa mahakamani hapo Desemba 20 mwaka huu, atakuwa ni mtuhumiwa wa tano katika kesi hiyo ya kula njama kutaka kumuua Dk. Chegeni.

Hata hivyo, mbunge huyo hajapatikana kuzungumzia tuhuma hizo dhidi yake.

Na Sitta Tumma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *